Mwanasheria Mkuu amgeuka Pinda; Awataka polisi wasitumie nguvu kubwa kudhibiti raia
*Awataka polisi wasitumie nguvu kubwa kudhibiti raia
MWANASHERIA
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amelitaka Jeshi la Polisi
nchini, kuacha kutumia nguvu zilizopita kiasi, pindi linapokuwa
likituliza ghasia.
Amesema, pamoja na kwamba jeshi hilo linaruhusiwa kisheria kutumia nguvu
wakati wa kutuliza ghasia, nguvu hizo hazitakiwi kuzidi kipimo kwa kuwa
kufanya hivyo ni kuvunja sheria.
Jaji Werema alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akifungua
mkutano wa mawakili wafawidhi wa Serikali, wakuu wa upelelezi wa makosa
ya jinai wa mikoa na vikosi vingine vya polisi.
“Sheria inaruhusu polisi kutumia nguvu katika baadhi ya maeneo, lakini utaratibu lazima ufuatwe.
“Tusitumie nguvu kubwa kupita kiasi, polisi mmejifunza kutumia mabomu,
bunduki na mmejifunza pia kutumia bunduki na kulenga shabaha, usimpige
mtu kichwani, hilo ni kosa, lenga kwenye mguu,” alisema Jaji Werema.
Kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaonekana kwenda kinyume na
kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda dhidi ya
wanaokaidi maagizo ya polisi.
Katika maelezo yake wakati akijibu swali na papo kwa papo aliloulizwa
wakati wa Bunge la Bajeti lililopita, Waziri Mkuu Pinda, aliruhusu
polisi wawapige raia pindi wanaposhindwa kutii sheria.
Wakati huo huo, jana Jaji Werema alilitaka Jeshi la Polisi nchini pamoja
na wanasheria wa Serikali, kuacha tabia ya kuwabambikia kesi raia
badala yake watafute ushahidi wa kutosha.
Alisema kama wanamfahamu mhalifu, wanatakiwa kutumia akili kwa kumkamata
kwa kufuata utaratibu wala siyo kumbambikia kesi isiyo na ushahidi.
“Katika baadhi ya kesi tusimkamate mtu kama hatuna ushahidi wa kutosha,
tunamkamata mtu siku ya Ijumaa ili tumkomeshe akae ndani halafu Jumatatu
anatoka.
“Unamjua mtu ni mhalifu, lakini unashindwa kumkamata matokeo yake
unambambikizia kesi ya mauaji, sio vizuri, tuache tabia hiyo,” alisema.
Alisema kwamba, kama polisi na wanasheria watafanya kazi kwa kufuata
utaratibu, utafika wakati wananchi watajenga imani na vyombo vya dola
kwa kuwa watumishi hao watakuwa wakizingatia maadili ya kazi yao.
Alitaka pia uwepo ushirikiano wa kutosha kati ya wapelelezi na
wanasheria wa Serikali, kwa kuwa bila kufanya hivyo, hakutakuwa na
mafanikio katika utendaji kazi wao.
“Kipindi hiki ni kigumu, tunahitaji kushirikiana zaidi kuliko kipindi
chochote kingine, wapelelezi na waendesha mashtaka ushirikiano wenu siyo
kitu cha hiari bali ni lazima, kwani kama hamshirikiani, hatuwezi
kushinda vita dhidi ya uhalifu,” alisema.
Jaji Werema alisema ingawa mawakili wa Serikali wana mamlaka ya kuondoa
kesi mahakamani, hawatakiwi kufanya hivyo bila kuwasiliana na kamanda wa
upelelezi wa mkoa husika, ili kujenga uwazi na kuondoa mianya ya
rushwa.
Aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika kutunza
majalada ya kesi na kuhakikisha wapelelezi hao na mawakili wa Serikali
wanafanya uamuzi wa haraka.
Alisema kwamba, kitendo cha watumishi hao kuchelewa kutatua malalamiko
ya wananchi, kinawafanya wananchi wakose imani na vyombo vya dola na
hivyo kuwapo ukiukwaji wa sheria kwa wananchi.
“Jinsi tunavyotenda kazi zetu, tunaweza kusababisha dola kuchukiwa,
halafu ikichukiwa tuwalaumu waandishi, mimi nawaambia, watuandike tu
kama tunakosea.
“Tuwe makini pia na mawasiliano yetu kwenye magazeti, sisi ni dola,
tusiwasiliane kupitia magazeti, tusitupiane lawama, tuwe na mawasiliano
mazuri kati ya ofisi ya DPP (Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka), Ofisi ya DCI
(Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) na siyo
kuwasiliana kupitia magazeti,” alisema.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
(DPP), Elizer Feleshi, alisema ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya usalama, imepokea agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka
wahalifu kujisalimisha na wapo tayari kulitekeleza.
“Tunawaasa wahalifu watumie vizuri muda wa wiki mbili waliopewa na rais,
vinginevyo watajutia vitendo vyao kwa sababu katika mkutano huu,
tutajadili namna ambavyo tutawashughulikia wale ambao hawatatekeleza
amri hiyo ya rais,” alisema.
Alisema mkutano huo ni miongoni mwa mikutano waliyoanzisha chini ya
Jukwaa la Haki Jinai wenye lengo la kuwakutanisha wadau pamoja kujadili
changamoto katika utoaji wa haki jinai.
Alisema changamoto mojawapo inayowakabili, ni kupunguza msongamano wa
mahabusu na wafungwa magerezani na kwamba idadi yao imepungua kutoka
wafungwa 45,000 mwaka 2003 hadi wafungwa 33,033 kufikia Julai mwaka huu.
Pamoja na hayo, alisema uwezo wa magereza yote nchini ni kuhifadhi wafungwa 29,552.