Baadhi ya miundombinu ya umeme iliyopo kwa sasa nchini. |
Serikali
imeweka wazi miradi ya umeme ya kipaumbele, itakayotoa matokeo ya haraka
ifikapo 2015/2016, na kunufaisha wananchi katika mikoa 13 nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo
jana mbele ya wadau waliokusanyika katika mkutano wa siku moja wa
kukusanya maoni kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema wizara hiyo imedhamiria kuhakikisha miradi
hiyo kwa kipindi hicho, inaleta matokeo muafaka yatakayoonekana wazi kwa Watanzania wote.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na bomba la gesi kutoka Mnazibay
hadi Dar es Salaam, lenye urefu wa Kilometa 534, ambalo litagharimu dola
za Marekani bilioni 1.2.
ÒNasisitiza acheni malumbano ya kipuuzi na malalamiko yasiyo na tiba,
bomba hili lazima likamilike ndani ya miezi 18,Ó alisema Muhongo.
Alisema wote wanaopinga kutandikwa kwa bomba hilo, hawaitakii mema
Tanzania na wananchi wake na kwamba hoja zao zimejaa ubaguzi.
ÒNaomba tusipoteze muda kujadili bomba hili, wapo watu wana sababu
zao, hii gesi itanufaisha Watanzania wote wakiwemo wa Mtwara, tusikubali
ujinga wa mtu mmoja uwe wa taifa zima,Ó alisisitiza.
Alitaja miradi mingine kuwa ni mitambo saba mipya ya Kinyerezi,
itakayozalisha megawati za umeme 1,310, itakayozalisha megawati 990, na
mradi wa upepo wa Singida wa megawati 50 na Kiwira wa megawati 200.
Miradi mingine ni ya ujenzi wa njia za usambazaji umeme, ambazo ni
Iringa-Shinyanga yenye kilometa 657 utakaosambaza umeme wa KV 400 na Dar
es Salaam-Chalinze-Tanga-Same-Arusha, wenye kilometa 682 utakaosambaza
umeme wa KV 400.CREDIT ZIRRO
Pia upo mradi wa Singida-Arusha wa kilometa 414 utakaosambaza umeme
wa KV 400, Somanga-Fungu-Somanga-Kinyerezi wa kilometa 300,
utakaosambaza umeme wa KV 220.
Mradi mwingine ni wa Nyakanazi-Kigoma-Mpanda-Sumbawanga-Mbeya, wenye
kilometa 340 utakaosambaza umeme wa KV 400 na Dar es
Salaam-Morogoro-Dodoma wenye urefu wa kilometa 530, utakaosambaza umeme
wa KV 400.
Ili kuhakikisha kila mradi, utekelezaji unasimamiwa vilivyo,
wakurugenzi wanne walioko chini ya Wizara ya Nishati na Madini,
watakaowajibika kutekeleza miradi hiyo, wameapa mbele ya wananchi kuwa
watafanikisha matokeo ya miradi hiyo, vinginevyo wako tayari kutimuliwa
kazi.
Wakurugenzi hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme
(Tanesco), Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli (TPDC), Yona Killagane.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini
(REA), Lutengano Mwakahesya pamoja na Kamishna wa Nishati na Petroli,
Hosea Mbise ambaye ndiye msimamizi mkuu wa miradi hiyo.
Wakurugenzi hao walitoa kiapo hicho mbele ya wadau waliokusanyika
katika mkutano wa siku moja ulioandaliwa na wizara hiyo, kwa ajili ya
kukusanya maoni juu ya utekelezaji wa miradi hiyo yenye matokeo makubwa
nchini ifikapo mwaka 2015/2016.
Akizungumza mara baada ya kuapa mbele ya wadau hao, Mbise, alisema
wizara hiyo imedhamiria kuhakikisha kuwa miradi hiyo kwa muda huo,
inaleta matokeo muafaka yatakayoonekana wazi kwa Watanzania wote.
ÒNi kweli kumekuwepo na miradi mingi ya wizara hii kwa muda mrefu,
lakini sasa nawaahidi kuwa tunakuja na njia mpya ya kuzingatia miradi
michache, lakini matokeo yake pamoja na kuonekana haraka, yatanufaisha
Watanzania wengi.
ÒNinawaahidi katika utekelezaji wa miradi hii, tutaachana kabisa na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea,Ó alisisitiza.
Kwa upande wake Mramba, alisema miradi hiyo, sehemu kubwa
itatekelezwa na shirika lake. ÒNawaahidi Tanesco haitowaangusha,
ninaamini uwezo wa kuleta matokeo haya makubwa ninao, nikishindwa niko
radhi mnichukulie hatua.Ó
ÊKillagane naye alisema ili kufanikisha miradi yote hiyo, jambo la
msingi ni kuhakikisha gesi inapatikana kwa haraka, ambapo kwa mujibu wa
maelekezo ya TPDC, ni lazima bomba la gesi kutoka Mnazibay mkoani Mtwara
hadi Dar es Salaam, liwe limetandikwa na kukamilika ifikapo Juni
mwakani.
ÒHili nitasimamia kwa dhati kuhakikisha gesi hii inafika jijini hapa
mwakani kama ilivyopangwa, TPDC tumejipanga ili kuhakikisha hii kazi
haikwami,Ó alisisitiza.
Mwakahesya ambaye ni Mkurugenzi wa REA, alisema jukumu lake katika
utekelezaji wa miradi hiyo, ni kushirikiana na sekta binafsi na ya umma,
ili umeme ufike vijijini. ÒSi maneno bali ni vitendo, niwajibisheni
kama sitafanikisha haya.Ó
Muhongo alisema anaamini watendaji hao hawawezi kumdanganya yeye wala
Watanzania, kwa kuwa anao uzoefu wa kutosha kubaini iwapo anadanganywa.
ÒNaomba mkiona mtu anafanya kazi chini ya wizara yangu hii kinyume na
taratibu, mleteni kwangu na nina ahidi mbele ya wananchi hawa kuwa
sababu zitakazomuondoa mtumishi wa wizara hii kazini, ni pamoja na
rushwa, wizi, utendaji mbovu na ubababishaji, hapa hakutakuwa na
mjadala, nyie mtaona tu watu wakipukutika,Ó alisisitiza.
Kuhusu umeme vijijini, Muhongo alisema kupitia mpango wao
walioainisha wa umeme vijijini, watahakikisha kila mwaka kwenye kila
mkoa, vijiji kadhaa vitakavyobainishwa kulingana na idadi ya watu wake,
vitapatiwa umeme na tayari Sh bilioni 330 zimetengwa kwa ajili ya kazi
hiyo.
Alisema miradi hiyo ikikamilika, Tanzania itakuwa inazalisha megawati
za umeme 2,780 na lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, megawati za
umeme 3,000 zinazalishwa na asilimia 56 ya Watanzania wana umeme. Kwa
sasa megawati za umeme zinazozalishwa ni 1,430.24 wakati mahitaji ni
megawati 850.
Ili kufanikisha malengo hayo, Muhongo alisema tayari hatua za kubomoa
Tanesco zimeshaanza kuchukuliwa, kwa sasa mchakato wa kumtafuta
mshauri kwa ajili ya kufanyia kazi ripoti ya menejimenti ya shirika
hilo, juu ya namna liwe, umeanza kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (ADB).
Mapendekezo ya awali yanaonesha shirika hilo litabomolewa na
kugawanywa, ambapo sehemu za uzalishaji, usambazaji na usafirishaji
umeme zitajitegemea, kwa kuwa na kampuni zaidi ya tatu, ambazo
hazitotegemea ruzuku ya Serikali.
Kwa upande wa TPDC, Muhongo alisema Serikali pia italifumua shirika
hilo kutoka kwenye muundo wake wa sasa, na kuwa shirika kubwa
litakalofanya utafiti na uvunaji wa gesi na mafuta, kama kampuni kubwa
za kigeni zinavyofanya ili kuondoa malalamiko ya nishati hiyo kuibiwa na
wageni.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakim Maswi, alisema tayari alishafuatwa na watu kadhaa ambao walitaka
kumpa rushwa, ili miradi yao mibovu itekelezwe na Serikali.
ÒKuna mtu alikuja akaniambia nikiweka saini kwenye mradi wake,
atanipa dola za Marekani 200,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 350,
nikamkatalia na kumtaka aondoke haraka na mradi wake uchwara,Ó alisema.
Kuhusu kusafisha Tanesco, alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana na
Juni mwaka huu, Shirika la Umeme (Tanesco), tayari limefukuza kazi
watumishi 49 wanaotuhumiwa kuhusika na rushwa na kulihujumu shirika
hilo.