- Hata hivyo mwenyewe Obama ameeleza wazi kuwa, hawezi kuitembelea Kenya wakati viongozi wake wa juu – Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto ni watuhumiwa wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).
Wakati huu ninapoandika makala hii, tuko kwenye
pilikapilika za kumpokea Rais wa Marekani, Barack Obama. Kwa kweli ziara
ya rais huyu imebadilisha kabisa ratiba za wakazi wa Dar es salaam.
Hata hivyo, kwa wenzetu Kenya imekuwa bahati
mbaya. Huku wakiwa wamenuna, wamebaki na maswali mengi. Kwa nini Obama
ambaye ana asili ya nchi hiyo hakupanga kufika kwao? Tanzania kuna nini
hadi marais watatu tangu wa Marekani – Bill Clinton, George Bush na
Obama wameitembelea?
Kumbuka Wakenya hawa wamekuwa wakifanya sherehe
kubwa kila mara Obama anapopata mafanikio kisiasa. Alipoukwaa urais kwa
mara ya kwanza mwaka 2008, walisherehekea. Mara ya pili mwaka 2012
walisimamisha kabisa kazi ili kusherehekea awamu ya pili ya urais wa
Obama.
Lakini sasa Obama anafanya ziara ya pili Afrika
bila kuitembelea Kenya na huenda hii ikawa ziara yake ya mwisho Afrika
hadi atakapomaliza urais wake, kwa hiyo Wakenya hawana bahati.
Hata hivyo mwenyewe Obama ameeleza wazi kuwa,
hawezi kuitembelea Kenya wakati viongozi wake wa juu – Rais Uhuru
Kenyatta na Makamu wake William Ruto ni watuhumiwa wa Mahakama ya
Kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).
Ishara ya kutowatambua viongozi hao ilionekana
tangu waliposhinda uchaguzi mkuu mwaka huu ambapo taarifa ya Serikali ya
Marekani iliishia tu kuwapongeza Wakenya kwa kufanya uchaguzi ulio huru
na wa haki, lakini haikuwataja Kenyatta na Rutto ambao ndiyo washindi.
Si Marekani tu, hata Uingereza imekataa kuwatambua
Kenyatta na Ruto kwa sababu hiyo. Mara baada ya ushindi wake, Kenyatta
alizuru Marekani kwenye mkutano wa kutafuta suluhu ya Taifa la Somalia.
Huko alikumbana na kituko baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Cameron kugoma kupiga naye picha.
Lakini swali moja linabaki, Marekani ina uhalali
gani wa kuinyooshea kidole Kenya ikiwa yenyewe imegoma kusaini mkataba
wa ICC (Rome Statute of the International Criminal Court)?
Hadi sasa kuna nchi 139 duniani zilizosaini
mkataba huo. Nchi ambazo hazijasaini ikiwemo Marekani, haziguswi na
hatia yoyote ya uhalifu wa kivita.
Marekani inajua wazi kwamba siku ikitia saini
imeingia kwenye mtego wa kushtakiwa kutokana na makosa mengi ya uhalifu
wa kivita iliyofanya.
Lakini leo Obama amesusa kwenda Kenya eti kwa
sababu Kenyatta na Rutto ni washtakiwa wa ICC! Usishangae kusikia
Marekani inayojiita kinara wa demokrasia duniani ikiwaunga mkono baadhi
ya viongozi wa kiimla na wababe wa vita duniani.
Hiyo ndiyo Marekani inayoibembeleza Tanzania.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi



