Biashara ya
dawa za kulevya nchini inazidi kuchukua sura mpya ambapo sasa wanawake
wanaouza vyakula, maarufu mama ntilie, hutumika kusambaza dawa hizo kwa
wateja. Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali
jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa biashara hiyo inafanyika katika
maeneo ya Tandika, Manzese, Vingunguti, Temeke, Tandale, Mtongani na
Keko.
Wanawake
hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuuza chakula kama kinga yao, huku
biashara yao kubwa ikiwa ni kuuza dawa za kulevya aina ya heroin, bangi
na aina nyingine.
Mbinu hii
mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya kwa kutumia wanawake wanaouza
vyakula imeelezwa kuwa inawasaidia wahusika wakuu, kuendesha biashara
yao kwa ufanisi zaidi.
Uchunguzi
umeonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa hizo wameamua kuwatumia
mamalishe kutokana na kuwa waaminifu na kuhudumia wateja wengi, hivyo ni
vigumu watu kuwashtukia wakiwamo askari polisi.
Imebainika
kuwa dawa hizo huuzwa kulingana na maeneo, wakati maeneo ya watu
wasiokuwa wa uwezo hupimwa kwa kutumia kipimo kidogo zaidi kwa bei ya
chini ambayo watumiaji husika huweza kuimudu.
Aidha dawa
hizo hufungwa katika mitindo miwili tofauti, ukiwa katika unga wa
vidonge na wa kawaida ingawa bei zake hazitofautiani sana.
Uchunguzi unaonyesha kuwa vidoge huuzwa vikiwa vizima au vipande, huku unga wa kawaida ukiuzwa kwa kipimo maalumu.
Kwa kawaida
‘unga’ huo huuzwa kwa Sh1,000 kwa pointi huku kete moja ikiuzwa kwa
Sh2,000, wakati vidonge, kizima huuzwa kwa Sh2,000, huku kipande huuzwa
kwa Sh1,000 zikitofautiana kulingana na maeneo.
Gazeti hili lilifanikiwa kuongea na baadhi ya wanawake wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo.
Dada mmoja
aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha (28) ambaye siyo jina lake
halisi ni muuzaji mkubwa wa dawa hizo. Awali alikuwa akifanya shughuli
zake hizo za uuzaji katika maeneo ya Yombo Kilakala, ingawaje hivi sasa
amehamia Temeke.
“Unajua siku
zote dhumuni la kufanya biashara ni kupata faida, hivyo naweza kusema
niliingia kwenye biashara hii kwa sababu tu ina faida zaidi kuliko
biashara nyingine,” anasema.
Awali
alikuwa akiuza vyakula huku akifanya biashara hiyo ya kuuza dawa,
baadaye akaacha kuuza vyakula akabaki na biashara ya dawa za kulevya.
Akielezea
namna anavyofanya biashara yake hiyo, Asha anasema kwa kawaida huwa
ananunua mkanda ambao unakuwa umefungwa vidoge vidogovidogo kumi hadi
ishirini. Mara nyingi huuza kulingana na mahitaji ya mteja.
“Halafu baada ya kununua hivyo huwa nauza kidogokidogo vidonge hivyo.
Kwa kawaida
kidoge kimoja huwa nauza kati ya sh1,000 hadi Sh2,000. Bei yake
hutegemea na mahali unapouzia. Kama unauzia watu waliochoka sana inabidi
upaki kidogokidogo ili kuweza kuliteka soko lao,” anasema.
“Nimefanya
biashara hii kwa muda wa miaka mitatu, lakini ukweli ni kwamba hadi sasa
nimefanikiwa kwa kiasi fulani. Nimeweza kujenga nyumba ya kwangu
mwenyewe, pia kuhudumia familia yangu. Licha ya kuwa na madhara kwa
watu, lakini ukweli ni kuwa biashara ya unga inalipa,” anasisitiza.
Abubakari
Ismail (33) aliyewahi kutumia dawa za kulevya, ambaye kwa sasa ni
kiongozi wa kupambana na dawa hizo kinachofahamika kama Use Ant -Drugs,
kilichopo Yombo, wilayani Temeke, anasema kuwa tatizo la wanawake
kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya linachangia kwa kiasi kikubwa
kuzorotesha mapambano dhidi ya dawa hizo hususan kwa vijana.
‘Joseph
(17)’, siyo jina lake halisi ni kijana aliyekuwa katika matibabu
kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Hivi sasa kijana huyu
amelazimika kuhama nyumbani kwao kutokana na kumkimbia mama yake mzazi
ambaye anajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Makangarawe Youth Information Center cha jijini Dar es
Salaam, kinachojishughulisha na miradi kadhaa ya vijana ikiwamo
mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana, Ismail Mnikite, amesema
kitendo cha wanawake kushiriki katika uuzaji wa dawa za kulevya ni
tatizo jipya linalochangia kukwamisha juhudi za mapambano hayo.
Chanzo - Mwananchi