Na Joachim Mushi, Kishapu
WASWAHILI
wanasema ‘maji ni uhai’ na maisha bila maji ni kadhia. Kimsingi
mwanadamu anahitaji maji safi na salama katika kuendesha maisha yake ya
kila siku. Na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama eneo fulani
huchangia kiwango fulani cha ugumu wa maisha kwenye familia.
Hali
hii ndiyo inayowakumba wakazi wa baadhi ya vijiji vya Kata ya Kishapu,
Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga. Tabu ya maji katika vijiji kama
Lubaga, Isoso, Mwanuru pamoja na Kishapu yenyewe ni msamiati wa kawaida.
Vijiji hivi hupata hauweni katika msimu wa masika pekee ambapo maji
hutiririka hata kwenye mito ya msimu (masika).
Lakini
mbali na familia kutaabika kusaka maji umbali mrefu kwa ajili ya
matumizi ya kila siku, lipo kundi ambalo huathirika zaidi na kero za
maji kwa kuwa kundi hilo ndilo linalotegemewa kutafuta maji katika
familia kwa matumizi anua. Kundi hilo ni wanawake na watoto wakiwemo
wanafunzi.
Makundi
haya ndiyo yenye majukumu ya kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani
(kwenye familia) wakati wote kulingana na mfumo wa kifamilia na tamaduni
za wakazi wa maeneo haya. Kadri ya msimu wa ukame katika vijiji hivyo
unavyozidi kushamiri ndivyo umbali wa kuyafuata maji kwa matumizi
uendelea kuongezeka.
Kwa
hali hii akina mama na wanafunzi hutembea kati ya kilimita tano hadi 10
kufuatilia maji kwa matumizi ya familia, kulingana na umbali wa kijiji
chao kwenda kwenye chanzo kikuu (ambacho hata hivyo si cha uhakika) cha
maji yaani Mto Tungu. Chanzo hiki cha maji nacho hukauka kipindi cha
kiangazi na hali kuwa ngumu zaidi.
Enock
Manyenye Shimba ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lubaga, anasema huduma
ya maji wanayotegemea licha ya kupatikana umbali mrefu haitosherezi kwa
matumizi. Anasema Kijiji hicho hutegemea maji ya Mto Tungu ambao upo
umbali wa kati ya kilimeta tano hadi kumi. “Kijiji chetu ni Kikubwa wapo
baadhi ya wanakijiji hulazimika kutembea hadi kilimeta 10 kutafuta
huduma hii…licha ya kuwa haitoshelezi kwa matumizi,” anasema Shimba.
Anaongeza
kuwa kadri ya msimu wa kiangazi unapochanganya maji katika Mto Tungu
nayo huadimika hivyo wananchi kutegemea kuchimba visima vya muda ndani
ya mto huo ili kupata masalia ya maji ardhini chini ya mto huo. “Hali
hii huwa sio kazi nyepesi maana wananchi huchimba na kufukia visima hivi
kila maji yanapoisha kwenye eneo la kisima…kwa sababu visima hivi huwa
vifupi unakuta kikichimbwa kisima kinaweza kutumia muda mfupi na maji
kukauka eneo hilo kisha tunachimba eneo lingine,” anasema Shimba.
Shimba
anasema kundi la wanawake na wanafunzi ndio watafutaji maji wakubwa
katika familia nyingi za Kijiji cha Lubaga na maeneo ya jirani na kijiji
hicho. Anaendelea kusema kuwa hata visima ambavyo hutumika hutoa maji
kidogo kidogo jambo ambalo husababisha uwepo wa foleni kwa wanavijiji
maeneo ya visimani.
Kiongozi
huyo wa kijiji cha Lubaga anasema mwaka 2010 wakati wa kampeni za
Uchaguzi Mkuu kijiji chao kilipewa ahadi ya kuchimbiwa visima virefu vya
maji na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Seleiman Nchambi ahadi ambayo
anasema hadi leo wanaifuatilia lakini bado haijatekelezwa. “Ahadi hii
nimeikuta hata katika nyaraka za ofisi ya kijiji lakini bado
haijatekelezwa,” anasema Shimba akizungumza na mwandishi wa makala haya
kijijini hapo.
Hata
hivyo kwa akinamama ambao umri umeenda zaidi kilio cha maji huwa
maradufu. Ester Bundera (60) ni mkazi wa Kijiji cha Isoso, anasema
katika kijiji hicho shida ya maji ni kubwa hasa miezi ya kiangazi.
Anasema wao hulazimika kuyafuata maji hadi mji mdogo wa Mhunze ulipo Mto
Tungu umbali ambao ni takribani kilometa 10 kwenda tu.
“Hapa
kijijini kwetu upo mto mdogo unaojulikana kama Nkonze ambao hutoa maji
msimu wa masika tu tena kwa shida…maji haya huyapata kwa kuchimba visima
vidogo vidogo mtoni kutokana na kutoka kidogo kidogo huwa ni ya
kugombea, lakini kuanzia mwezi wa saba mto huu visima vyake hukauka
hivyo kulazimika kwenda Mto Tungu,” anasema.
Bi.
Anastazia Christopher ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Karume kilichopo
Kijijini Isoso, akielezea shida ya maji ambayo wanakijiji hicho huyapata
katika Mto Nkonze anasema familia zisizo weza kuvumilia foleni na
vurugu za kuchota maji yanayotoka taratibu visimani hulazimika kwenda
mtoni usiku muda ambao wakazi wengi huwa wamepungua jambo ambalo ni
hatari kiusalama.
“Wanawake
ndio wachotaji wa maji wakubwa pamoja na watoto wao hulazimika kwenda
vizimani majira ya saa mbili na saa tatu usiku muda ambao panakuwa
pametulia na kuanza kuchota maji…unajua huku kwetu wanyama kama fisi
ndio ambao hututishia hivyo unaweza kuomba vijana wakusindikize kisimaji
majira kama hayo,” anasema Bi. Christopher.
Aidha
anasema matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama kijijini hapo
sasa yanazidi kuyeyuka, kwani ulikuwepo mradi unaodaiwa kufadhiliwa na
UNDP ambao ulisambaza mabomba hadi kijijini hapo, lakini umekwama kwa
zaidi ya miaka 10 tangu uanze bila kufanya kazi. Kwa sasa mabomba
yaliokuwa yametandazwa yanang’olewa na Serikali na kupelekwa maeneo
mengine kitendo ambacho anasema kinazidi kuwakatisha tamaa. Anasema
kijiji hicho pia ni miongoni mwa vijiji vilivyoahidiwa kuletewa maji na
Mbunge Nchambi ahadi ambayo bado ijatekelezwa.
Hata
hivyo kilio cha maji hutofautiana kutoka kijiji kimoja hadi kingine
kutokana na umbali wa kijiji husika na chanzo cha maji wanachokitegemea.
Kwa msingi huo hali ya huduma ya maji ni mbaya zaidi katika Kijiji cha
Kishapu, ambacho wananchi hutegemea maji ya mabwawa ya mvua ambayo si
safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Kipindi cha kiangazi ukame
unapokausha mabwawa wanakijiji hulazimika kusafiri hadi eneo la Mto
Tungu kupata huduma ya maji. Umbali kutoka katika kijiji hicho hadi
mtoni Tungu ni takribani ya zaidi ya kilometa 30 jambo ambalo ni kero
zaidi kwa wanakijiji. Na wanaoshindwa kufuata maji ya bure katika mto
Tungu hulazimika kununua kwa wachuuzi wa maji ambao huyafuata machimboni
Mwadui.
Bi.
Khadija Said ni mmoja wa wakazi wa Kishapu, anasema kero ya huduma ya
maji eneo lao ni zaidi. Wananchi wakati mwingine hulazimika kutumia maji
ya madibwi ambayo si safi na salama kutokana na hali ngumu. Vilio vya
maji katika vijiji mbalimbali vya Kata ya Kishapu havipo kwa wazazi tu.
Wanafunzi nao baada ya kurudi shuleni jioni hulazimika kuanza shughuli
ya kusaka maji kwa ajili ya matumizi.
Unapopita
maeneo ya Mto Tungu nyakati za jioni utakutana na baadhi ya wanafunzi
ambao ama wanakuwa wanachota maji au kufua sare zao za shule eneo la mto
huo. Kundi hili hujulikana kirahisi kwa kuwa huwa wamevaa nusu sare za
shule, yaani kwa wanafunzi wa kiume baadhi huwa wamevaa suruali za shule
na shati la nyumbani, huku wa kike wakiwa na sketi za shuleni na juu
vazi la nyumbani.
Biashara
ya maji kwa baadhi ya vijiji ni kubwa na inafanywa na wanaume kwa
kutumia matoroli. Wachuuzi hawa wa maji hutumia toroli lenye uwezo wa
kubeba madumu manne ambayo kila dumu linauwezo wa kuchukua lita 20.
Wachuuzi hawa huuza maji yao kwa madumu manne kwa pamoja, yaani shilingi
1,000 kwa madumu manne. Lakini licha ya kundi hili kuwa mahiri kwa
uchotaji maji ya biashara si wanaotoa msaada wa maji katika familia zao.
Jukumu hilo lipo kwa watoto na akina mama kwa matumizi ya nyumbani.
Wanyama
wanaofungwa na binadamu kama ng’ombe, mbuzi na kondoo nao ukubwa na
ukame huu. Wanyama hawa hulazimika kunywa maji kwenye chanzo kimoja na
binadamu (Mto Tungu) kutokana na shida ya maji. Kutokana na usimamizi
mbovu wa vyanzo vya maji Mto Tungu pia hutumika vibaya kwa kile baadhi
ya wananchi kuingia ndani ya mto na kufanya usafi kama kufua nguo ndani
ya mto.
Maxmilian
Lugembe ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kishapu. Katika mazungumzo na
mwandishi wa makala haya anakiri uwepo wa shida ya maji kwa kata nzima
ya Kishapu na maeneo mengine yanayoizunguka kata hiyo. Hata hivyo
anasema hali hiyo inasababishwa na jiografia ya eneo hilo. Anasema
maeneo mengi ya vijiji vya kata hiyo ni vigumu hata hupatikanaji maji ya
uchimbaji visima virefu kwa matumizi ya kawaida.
“Yapo
maeneo ambayo tumejaribu kuchimba visima virefu lakini hupati
maji…ukiangalia visima vinavyochimbwa ni vile vinavyochimbwa kwenye mto
baada ya maji yanayotiririka kukauka mtoni, hapo ndio wananchi wanapata
maji. Yapo maeneo mengine tumejaribu lakini hupati maji kabisa, eneo
hili ni tatizo,” anasema Ofisa huyo wa Serikali.
Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, George Kessy anaungana na kauli
ya mtendaji wake. “Ni kweli suala la maji ni Tatizo kwa wilaya nzima ya
Kishapu, tena ni kubwa sana…hivyo wapo sahihi wananchi wanapolalamikia
suala hilo. Hakuna chanzo cha maji cha uhakika eneo hili,” anasema Kessy
katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya.
Hata
hivyo anasema juhudi zinafanywa kuhakikisha wanapata maji ya uhakika
eneo hilo. “Lengo la halmashauri ni kuhakikisha eneo letu linapata maji
kutoka kwenye chanzo cha maji cha uhakika…na mchakato umesha anza, kuna
mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria na hili lipo kwenye
mchakato,” anasema mkurugenzi huyo.
Kwa
upande wake Mbunge Nchambi akizungumzia ahadi za maji alizotoa wakati
wa kampeni na utekelezaji wake anasema hali ni nzuri kiutekelezaji
ukilinganisha na hali ilivyokuwa ahapo awali. “Niliahidi maji jimbo zima
la Kishapu yaani jumla ya vijiji 114, wakati naingia madarakani
nimekuta hali ni mbaya ya huduma za maji…lakini hadi sasa tunapozungumza
zaidi ya vijiji 30 vinapata maji safi na salama huku jitihada zingine
zinaendelea,” anasema Nchambi.
Anabainisha
kuwa ameingia madarakani na kukuta Jimbo zima la Kishapu likipata maji
kwa chini ya asilimia nne, lakini kwa sasa vijiji vingi vimeongezeka.
Utekelezaji wa ahadi zake juu ya huduma za maji unaenda awamu kwa awamu
hivyo kila kijiji kitapata maji safi na salama. “Ahadi yangu mimi ni
miaka mitano, ilani ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) ni ya miaka mitano,
ninaenda kwa awamu yaani vijijini 10 kwa kila mwaka kwa wilaya,” alisema
mbunge huyo.
Anasema
upo mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao bomba lake linatokea Mkoa wa
Shinyanga, mradi ambao utavinufaisha kihuduma za maji vijiji vingine
vingi kutoka Jimbo la Kishapu. Anawashauri wananchi kuwa wavumilivu
kwani juhudi zinaendelea kufanywa kuhakikisha maji yanasambazwa katika
vijiji vyote vihitaji.
Akitoa
ufafanuzi juu ya zoezi la ufukuaji mabomba yaliosambazwa kwa baadhi ya
vijiji anasema, kwanza mabomba hayo si salama kutokana na kukaa muda
mrefu ardhini bila kutumika. maji yanayotoka eneo la Kishapu yalifungwa
mabomba mapya, mabomba yanayofukuliwa kwa sasa yamekaa muda mrefu
ardhini bila kutumika hivyo si salama. Anasema utakapofika mradi wa Ziwa
Victoria yatafungwa mabomba mapya na kusambaza maji vijiji husika.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com