Wakati
kukionekana kuwapo kwa mvutano mkali kati ya Jeshi la Polisi nchini na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama hicho kimesema kuwa
hakitakubali kukaa kimya wakati baadhi ya watumishi wa jeshi hilo
wakitumiwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa kukandamiza raia.
Chama hicho kimesema hakina ugomvi na jeshi
hilo kwa ujumla wake, isipokuwa askari wachache kiliodai wanatumiwa
vibaya kuhujumu haki za binadamu na demokrasia nchini, kikisema hao
ndiyo wanalipaka matope jeshi hilo na kuzidi kulikosesha imani kwa
wananchi.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara Tabora
mjini, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho
hakitarudi nyuma kutetea haki na matumaini ya Watanzania.
Mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa
Chipukizi, ukiwa ni sehemu ya kukamilisha kuzindua Kanda ya Magharibi
(mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi), ikiwa ni mkakati wa chama hicho wa
kujiendesha kwa kanda.
“Ndugu zangu watu wa Tabora, wanachama na
wapenzi wetu wa Kanda ya Magharibi, katika mapambano haya ya kuing’oa
CCM na kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo na utawala ndani ya nchi yetu,
tumefika mahali utetezi wa haki na matumaini ya wananchi umegeuzwa kuwa
ni vurugu au fujo…kila leo mnasikia chama chenu ambacho kimezidi kuwa
na ushawishi miongoni mwa Watanzania wengi wenye kiu kubwa ya
mabadiliko, kinafanyiwa vituko, kimoja baada ya kingine,” alisema.
Alisema hivi sasa wafuasi na wapenzi wa chama hicho wanatekwa, wanateswa, kupigwa na hata kuuawa.
“Matukio ya namna hii yanazidi na sisi
tumesema hatuwezi kuendelea kulalamika na kulialia kwa vyombo husika.
Tutajilinda,” alisema.
“Tunatambua umuhimu wa vyombo vya ulinzi na
usalama. Taifa linawahitaji wawe waadilifu, watimize wajibu na kutenda
haki kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Chadema tunawatetea hawa
ndani na nje ya Bunge, lakini hatutakubaliana na askari wanaotumika
vibaya, kwa kupewa amri za hovyo, kama kwenye tukio la bomu Arusha,”
alisema Mbowe.
Akizungumzia suala la mjadala wa rasimu ya
Katiba Mpya, Mbowe alisema mapema mwezi Agosti, mwaka huu, chama hicho
kitaanza kuzunguka nchi nzima kwenye operesheni M4C-Katiba Mpya; na
kitaendesha mabaraza yake kwa uwazi kwenye mikutano ya hadhara.