Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
|
Polisi
imekiri kuwa wasichana wawili raia wa Tanzania waliokamatwa nchini
Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya Sh. bilioni
6.8, walipitia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Wasichana hao walisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la South African Airways linalomilikiwa na serikali ya Afrika Kusini.
Kamanda
wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey
Nzoa, alisema hayo jana wakati akizungumza katika mahojiano na NIPASHE
iliyotaka kujua kama wasichana hao walipitia uwanja gani na kama
walikaguliwa na maofisa wa uwanja huo.
“Kila
mtu anapopita uwanja wa ndege anakaguliwa na kama ana kitu ambacho ni
kibaya ndipo anakamatwa, hawa wasichana walikaguliwa maana huwezi kupita
uwanja wa ndege bila kukaguliwa,” alisema Kamanda Nzoa.
Kamanda
Nzoa alisema si jukumu la Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi kwenye
viwanja vya ndege, lakini ni jambo la kawaida mtu kukamatwa nchi
nyingine na dawa za kulevya wakati katika nchi aliyoanzia safari
hajakamatwa kwani inategemea utalaamu wa watu wenyewe wanaokagua.
Alisema
kinachotakiwa watu wa uwanja wa ndege ni lazima wawe na mtu au wakaguzi
ambaye ni mtaalamu sana wa kutambua dawa za kulevya kwa kuwa ziko za
aina nyingi na mbinu nyingi zinatumika kuzisafirisha.
Aidha, alisema dawa za kulevya ni nyingi na siyo cocaine tu ambayo imezoeleka mara kwa mara.
“Utakumbuka
Juni 23 mwaka 2010 nilikamata mabalozi wawili, hawa watu walitoka
Brazil wakaenda Afrika Kusini, lakini tukawakamatia hapa Tanzania,”
alisema Nzoa.
Aliongeza kuwa hivi sasa wasichana hao wamekwisha kufunguliwa mashtaka nchini Afrika Kusini.
Kamanda Nzoa alisema uchunguzi unaendelea kumbaini mmiliki wa dawa hizo na kuna dalili za kuwabaini wahusika hao.
Dawa
hizo zilisafirishwa kama mizigo mingine inayokaa sehemu za mizigo
ndani ya ndege kwani uzoefu unaonyesha kwamba kwa namna yoyote ile
abiria hawezi kuruhusiwa kwenda kukaa na mzigo wake ndani ya ndege
unaofikia kilo 150.
Uzoefu
unaonyesha kwamba kwa kawaida ndege kulingana na ukubwa wake zimekuwa
zikiruhusu abiria kupanda na kukaa na mizigo yao ya mkononi isiyo na
uzito mkubwa.
Baadhi
ya ndege zinaruhusu abiria kupanda ndani ya ndege wakiwa na mizigo yao
ya mkononi isiyozidi uzito wa kilo kumi wakati mzigo unaokaa kwenye
mizigo chini baadhi ya mashirika ya ndege huruhusu uzito wa kuanzia kilo
20 hadi 40.
Katika
hali ya kawaida, hata kama wasichana hao wangeamua kugawana dawa hizo
kwa usawa, kila mmoja angebeba kilo 75, kiasi ambacho hata hivyo abiria
haruhusiwi kupanda nacho kama mzigo wa mkononi, wala mzigo ambao
haulipiwi.
Kwa
hali hiyo, mizigo hiyo ililipiwa gharama za ziada za usafirishaji kwa
kuwa hakuna shirika la ndege lenye unafuu wa mizigo ya bure kwa abiria
wake kwa uzito wa kilo 75.
Jitihada
zinaendelea kumtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Nchini (TAA), kujua ilikuwa je watumishi waliokuwa zamu siku ambayo
mzigo huo ulisafirishwa kuelekea nchini Afrika Kusini hawakutambua dawa
hizo.
Juzi
Kamanda Nzoa aliwataja wanawake hao waliokamatwa Afrika Kusini wakiwa
na dawa hizo kuwa ni Agnes Jerald (25) na Melisa Edward 24.
Jumapili
iliyopita NIPASHE ilipata taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya aina
ya Crystal Methamphetamine zenye thamani hiyo nchini Afrika Kusini
wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Taarifa
hizo zilionyesha kuwa wanawake wawili walikamatwa katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo uliopo eneo la Kempton Park Ijumaa
wiki iliyopita wakitokea Tanzania.
Wasichana
hao walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini wakiwa
na masanduku sita ambayo yalipokaguliwa yalikutwa na kilo 150 za dawa
hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ zikiwa na thamani ya bei ya
mtaani ya Sh. bilioni 6.8 sawa na Randi milioni 42.
Baada ya kukamatwa na dawa hizo wasichana hao walikabidhiwa polisi.
CHANZO: NIPASHE