Dereva wa matatu
akijaribu kupata intaneti isiyotumia waya kaitka simu yake ya mkononi. [Na Rajab
Ramah/Sabahi]
Na Rajab Ramah,
Nairobi
Magari ya usafiri wa umma mjini Nairobi --
yanayojulikana kwa mziki wake wa sauti kubwa, kupiga honi na uendeshaji mbaya --
yanabadilisha mwenendo.
Waendeshaji wa mabasi madogo na magari madogo
ya kuchukua abiria, kienyeji yanayojulikana kama matatu, yanaifanya safari ya
abiria kuwa ya kufurahia na wa rahisi zaidi baada ya kuanzisha huduma za
intaneti bure bila ya kutumia waya ndani ya mabasi.
"Tumekuwa tukijulikana kwa mambo yote mabaya,"
alisema Daniel Masava, dereva anayefanya kazi njia No. 125 kutoka katikati ya
jiji la Nairobi kuelekea kitongoji cha Ongata Rongai.
"Tunaitwa madereva jeuri ambao tunapuuza sheria
za barabarani na kutojali," aliiambia Sabahi. "Lakini tangu kuingizwa kwa Wi-Fi
katika magari yetu, sasa tunaonekana kama kibanda cha intaneti kinachotembea
tukiwa na mchango kwa uchumi."
Huduma ya Vuma
Online inatangazwa nyuma ya matatu mjini Nairobi. Huduma hiyo ni ya bure kwa
mabasi ya abiria na shilingi 1,500 kwa mwezi kwa waendeshaji mabasi. [Na Rajab
Ramah/Sabahi]
Hapo tarehe 14 Juni, kampuni ya utoaji wa
mawasiliano ya simu Safaricom Limited ilitoa huduma za intaneti bila ya kutumia
waya, inayoitwa "Vuma Online", kwa kushirikiana na waendesha matatu mjini
Nairobi.
Huduma hii itawapa abiria intaneti ya bure bila
kutumia waya kwa matatu 200. Magari madogo yanayotumiwa kwa usafiri wa umma kwa
kawaida huchukua abiria 14 wakati mabasi madogo yanaweza kuchukua hadi abiria
32.
Huduma hii iliibuka kama mpango wa majaribio
ambayo ilijaribu matumizi ya intaneti bila ya kutumia waya na mwitiko wa
watumiaji kwa magari 20 ya usafiri wa umma. Sasa, waendeshaji wa mabasi madogo
na magari madogo ya abiria wanaweza kujiandikisha kwa huduma hii na kulipa
shilingi 1,500 (dola 17) kwa mwezi, ikiwa ni pamoja na kifaa kisiyotumia waya ya
kuleta intaneti.
"Wakati wa programu ya majaribio, tuligundua
kwamba wateja wetu wanaotumia zaidi matatu kama njia yao ya usafiri ya kila siku
wanayoipenda, walitaka wawe mtandaoni, hata pale wanapokuwa wanasafiri," alisema
Afisa Mtendaji Mkuu wa Safaricom Bob Collymore.
"Kwa hivyo, kwa sisi kusisitiza hadithi ya
intaneti na kuifanya kuwa ni njia ya maisha, ilitubidi tuwapelekee intaneti hiyo
kwa kuwapatia Wi-Fi bure katika njia yao za usafiri."
Mpango huu ni wa kwanza wa aina yake barani
Afrika na una dhamiri ya kuunganisha mgawanyiko wa kidigitali nchini Kenya,
Collymore alisema. Vuma Online inawaruhusu watu wasioweza kumudu huduma za
intaneti majumbani kwao kuweza kutumia intaneti kupitia simu zao za mkononi
wakati wanasafiri, alisema.
Safaricom pia itategemea uunganishaji wa
intaneti isiyotumia waya ndani ya mabasi ili kutoa habari za barabarani na
kufuatilia iwapo mabasi ya umma na magari madogo yanakwenda kwa mujibu wa
ratiba, Collymore.
Utoaji wa huduma za intaneti kwa vyombo vya
usafiri wa umma unaongeza thamani kwa sekta hii, Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Matatu Simon Kimutai alisema, akikana wasiwasi kwamba hii itapelekea
kupanda kwa ada.
"Nairobi ni mji wenye matatizo ya msongamano wa
magari. Watu [wanaweza] kutumia masaa matatu barabarani, na hii imekuwa
ikiwaudhi wasafiri," aliiambia Sabahi. "Lakini sasa hii imebadilika. Wanaweza
kuzungumza wakiwa kwenye Facebook, kutuma ujumbe na kutumia intaneti jambo
linalowafanya safari yao iwe imejaa furaha."
"Kwa sisi, ni wakati wa kusisimua kwa magari ya
umma," Kimutai. "Tuna mageuzi mengi yanayoendelea nchini, lakini mbali na
uvumbuzi huu mara hii kuwa unafaa sana kwa abiria, unatufanya tuwe sehemu ya
safari ya kuigeuza nchi kuwa ya dijitali."
Wasafiri watathmini huduma hiyo mpya
Kwa Caroline Omondi, mwenye umri wa miaka 26,
intaneti bila ya waya ndani ya matatu inamweka mbele kwa siku yake ya kazi na
inamruhusu kupata masaa ya ziada ya kulala asubuhi.
Omondi alisema alikuwa anaamka saa tatu mapema
zaidi ili kusafiri kutoka Kayole hadi kazini kwake mjini Nairobi kama opereta wa
safari na utalii ili aweze kujibu barua pepe za kampuni kabla ya kufika saa ya
harakati nyingi.
"Sasa ninaondoka nyumbani saa 2 asubuhi, na
wakati ninapokuwa ofisini kiasi cha saa 3:30 asubuhi, ninatumia intaneti
inayotolewa na matatu ili kujibu mahitaji yangu yote," alisema. "Kwa sasa sina
wasiwasi tena wa kuamka nimechelewa."
Omar Said, mwanafunzi wa sheria mwenye umri wa
miaka 23 katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anatumia huduma za intaneti bila ya
kutumia waya ndani ya basi kwa kupakua programu za matumizi kwa ajili ya simu na
kompyuta yake, miongoni mwa shughuli nyengine ambazo zinamfanya awe na harakati
wakati wa safari yake baina ya nyumbani na shule.
"Ninatumia angalau saa nne kwa siku katika gari
la umma," aliiambia Sabahi. "Katika muda huu, ninafanya utafiti wangu na kupakua
nyaraka mtandaoni ambazo ninazitumia kujenga mradi wangu ambao unatakikana mwezi
ujao."
Hata hivyo, Viola Maingi, 22, alikuwa mmoja wa
wasafiri walioeleza wasiwasi wao kwa huduma hii mpya, alisema ilisababisha
kuongezeka kwa wizi wa simu.
"Wiki iliyopita, simu yangu iliporwa na mtu
aliyejidai kuwa mtembea kwa miguu katika Barabara ya Jogoo. Simu yangu ilikuwa
kiganjani na madirisha ya gari yalikuwa wazi," aliiambia Sabahi. "Woga huu ni wa
kweli na ni jukumu ya wasimamizi wa matatu kuhakikisha usalama wetu ili huduma
hii iweze kuwa yenye mafanikio."