Mbunge wa Jimbo la Ubungo -Chadema John Mnyika
---
Katika
kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha amesema
kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya simu
ni ya wabunge.
Kauli
inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa Wizara
yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii katika
siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na
sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu udhaifu wa Rais
(na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala yanayohusu maandalizi
ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo na
ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa wananchi. Kwa kauli
hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea kujihidhirisha.
Kauli
hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya
wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa
wabunge.
Ni
muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali
ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo.
Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga
pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho
lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu
hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria
kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na
marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.
Hata
kama ikiwa ni ukweli kwamba wazo hilo ni la baadhi ya Wabunge (ambao ni
muhimu wakatajwa kwa majina), Serikali inayokwepa kutetea maamuzi ambayo
Serikali yenyewe imeyaunga mkono inadhihirisha kwamba imechoka na
imepoteza uhalali kwa kimaadili kwa kushindwa kukubalika mbele ya
wananchi wake yenyewe (illegitimate government) .
Mamlaka
na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuishauri na
kuisimamia Serikali. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Bunge ni chombo cha
uwakilishi wa wananchi na chenye mamlaka pia ya kutunga sheria na
kupitisha bajeti ya nchi. Hata hivyo, ibara ya 99 ya Katiba imeweka
mipaka kwa mamlaka hayo ya Bunge inapokuja suala la kutunga sheria ya
fedha kama hii iliyoongeza mzigo wa kodi kwa wananchi. Mamlaka hayo
yamewekwa kwa kiwango kikubwa mikononi mwa Rais kupitia Waziri wake
mwenye dhamana.
Ninachofahamu
mimi ni kwamba kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya
ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma bajeti ya
Serikali. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri lakini wakati
wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba imefutwa.
Waziri
wa Fedha aeleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka
likaingia katika kitabu cha hotuba yake na nini maamuzi ya Baraza la
Mawaziri kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma
hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).
Kifungu
hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya
Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha
mwenyewe. Hivyo, ajitokeze na kueleza katika hatua hiyo, ni wabunge
gani waliotaka kodi hiyo iingizwe katika muswada huo na sababu za Wizara
ya Fedha kukubaliana nao.
Uzembe
wa Bunge usitumike kama kisingizio cha kuficha udhaifu wa Serikali
katika suala hili na mengine. Ni wazi, kuna uzembe pia kwa upande wa
Bunge kwa kuacha mapendekezo ya wabunge wachache yageuzwe kinyemela kuwa
ni msimamo wa wabunge wote bila ya kuwa na azimio la Bunge kuhusu
mapendekezo hayo.
Katika
mchango wangu bungeni kuhusu muswada huo, nilifanya rejea ya inayoitwa
Kamati Ndogo ya Spika ya kupanua wigo wa mapato iliyoundwa kabla ya
kuundwa kwa Kamati ya Bajeti; zote mbili zikiongozwa na Mh. Andrew
Chenge (Mb).
Kamati
hii ambayo haijawahi kuwasilisha ripoti yake Bungeni bali kwa Spika
mwenyewe na hatimaye sasa ripoti kuwekwa kwenye maktaba ya Bunge, bila
ya ripoti hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni kama taarifa ya kamati
au walau kuwekwa mezani kama hati rasmi ya Bunge; sasa inatumika
kusukuma mzigo wa lawama kwa Bunge na wabunge.
Baada
ya kamati hii, majadiliano kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti
yaliyofanyika kwa nyakati mbalimbali yanatumika kuhalalisha maamuzi ya
Serikali yenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi katika
hali yenye kudhihirisha uzembe wa Bunge wa kuachia mamlaka na madaraka
yake kutumiwa visivyo.
Katika
muktadha huu, kulaumiana kati ya Serikali na Wabunge au kulalamika kwa
wananchi pekee hakutoshelezi kuwezesha uwajibikaji au mabadiliko
yanayokusudiwa. Lawama ziendelee kwa kuwa zinasaidia kuendeleza mjadala
na kufanya ukweli uoendelee kutolewa na pande zote. Malalamiko ya
wananchi yaendelee kwa kuwa inawezesha Serikali na wabunge kutambua
athari za maamuzi hayo kwa wananchi.
Tunapaswa
kwenda mbele zaidi kwa wewe, mimi na mwingine kuchukua hatua? Wewe
unapendekeza hatua gani zichukuliwe? Nitatoa msimamo wangu kuhusu hatua
zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kupata maoni yenu kwa kuniandikia
kupitiambungeubungo@gmail.com. Maslahi ya umma kwanza.
JOHN MNYIKA (MB)
11/07/2013