Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Thursday, July 4, 2013

FBI WATUA MKOANI ARUSHA KUCHUNGUZA BOMU LA SOWETO

 

Askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), tayari wapo Arusha kushirikiana na polisi ili kuchunguza tukio la mlipuko wa bomu la kutupa kwa mkono kwenye mkutano wa kampeni za Chadema.

Katika tukio hilo lililotokea Juni 15, mwaka huu Viwanja vya Soweto, eneo la Kaloleni, Arusha, watu wanne walipoteza maisha huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, alithibitisha ushiriki wa FBI katika upelelezi huo.

Licha ya FBI, polisi wanashirikiana na wenzao kutoka nchi jirani ya Kenya, ambao wana uzoefu na matukio ya milipuko ya mabomu yanayotokea nchini mwao mara kwa mara, hasa baada ya nchi hiyo kupeleka wanajeshi nchini Somalia kukabiliana na Kundi la Al-Shabaab.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kina mlipuko wa bomu Soweto, tayari wenzetu wa FBI na polisi wa Kenya wamefika kushirikiana nasi, nachukua fursa hii kuwaomba wenye ushahidi utakaosaidia upelelezi kujitokeza,” alisema Sabas.

Serikali imetangaza zawadi ya Sh100 milioni kwa yeyote atakayetoa taarifa itakayosaidia kumpata aliyehusika, au wanaohusika na mlipuko huo.

Sabas alisema watu watatu waliokuwa wakishikilia na polisi kwa mahojiano kuhusu bomu hilo, tayari wameachiwa kwa dhamana.

Hii ni mara ya pili maofisa wa FBI na polisi kutoka Kenya kushiriki uchunguzi wa mlipuko wa bomu Arusha.

Mara ya kwanza walishiriki kuchunguza mlipuko uliotokea kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti iliyotokea Mei 5, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bomu lililolipuka Soweto ni la kijeshi na limetengenezwa nchini China.

Uchaguzi wa madiwani kata nne za Elerai, Kimandolu, Themi na Kaloleni, uliahirishwa hadi Juni 30, mwaka huu kabla ya kusogezwa mbele tena hadi Julai 14, kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, kuwa sababu za usalama.

Wakati huohuo, Serikali imetangaza kugundua mtandao wa milipuko ya mabomu yaliyotokea Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti na Viwanja vya Soweto, Arusha.Pia, iliahidi kuwachukulia hatua stahiki wahusika wote bila kujali cheo, umaarufu wala nafasi yake kisiasa.

Tamko hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, alipozungumza kwenye kikao cha Baraza la Ushauri Mkoa (RCC).

Mulongo alisema uchunguzi umegundua kuwa mipango ya milipuko ya mabomu yote mawili ya Olasiti na Soweto, ilifanyika Arusha.

Hata hivyo, Mulongo hakutoa ufafanuzi na kwamba, Serikali imefanikiwa kujua mtandao unaohusika na milipuko hiyo baada ya kupata maelezo kutoka kwa raia wema waliojitokeza kutoa taarifa baada ya matukio hayo.

Mwananchi:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...