Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la ujasusi la Marekani Edward Snowden
leo atakutana na wanaharakati wa haki za binaadamu mjini Moscow. Mkutano
wao utafanyika katika uwanja wa ndege mjini humo alipo kwa majuma
matatu.
Itakuwa ni mara ya kwanza Snowden, wakala huyo wa zamani wa Shirika la ujasusi la Marekani CIA anafanya mkutano huo, tangu alipowasili kutoka Hong Kong.
Sambamba na hayo Snowden pia anajaribu kupata uungaji mkono zaidi dhidi ya kampeni ya Marekani ya kumuandama yeye binafsi, ikitaka arejeshwe nyumbani.
Walioalikwa katika mkutano huo wa leo ni pamoja na wawakilishi wa Shirika la kimataifa la haki za binaadamu -Amnesty International, lile la Human Rights Watch na Shirika la kupambana na rushwa la Transparency International pamoja na wanasheria kadhaa maarufu wanaofanya kazi mjini Moscow.
Katika barua pepe yenye mwaliko huo, Snowden amezishukuru nchi za Amerika Kusini kwa kuwa tayari kuzingatia kumpa hifadhi ya kisiasa na wakati huo huo akailaani kampeni ya Marekani kujaribu kuzuwia asipewe hifadhi .
Nchi za Amerika Kusini zamkaribisha Snowden
Msemaji wa uwanja wa ndege wa Sheremetyevo mahala pa mkutano huo ulioitishwa leo, Anna Zakharenkova alithibitisha kwamba Snowden atakuwa na mkutano huo katika eneo la uwanja huo wa ndege,akiongeza kwamba wao watatoa nafasi hiyo, lakini alikataa kueleza zaidi.
Tangu awasili kutoka Hong Kong Juni 26 , Snowden hakuonekana hadharani na kwa mujibu wa maafisa amekuwa wakati wote kwenye eneo la abiria wapita njia, huku Rais Vladimir Putin wa Urusi akiwa amesisitiza kwamba nchi yake haitomkabidhi Snowden kwa maafisa wa Marekani.
Aidha Putin alisema Urusi ina hamu ya kuona suala hilo la mtu ambaye amezidisha utata katika uhusiano wa Urusi na Marekani ambao tayari ni tete, linapatiawa ufumbuzi.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/afp
Mhariri: Daniel Gakuba