Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi jana alikuwa na wakati
mgumu katika Kongamano la Amani lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), baada ya Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willbroad Slaa kumtaka ajiuzulu kutokana na kushindwa
kudhibiti uhalifu nchini.Mbali
ya Dk Nchimbi, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi katika kongamano hilo,
Brigedia Jenerali, Elias Athanas naye alibanwa akitakiwa kueleza tuhuma
za askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuhusishwa na vitendo
vya ubakaji na utesaji wa raia mjini Mtwara.Akizungumza
katika kongamano hilo, Dk Slaa alisema hakuna haja ya kutafuta mchawi
wa amani ya nchi bali, Serikali inapaswa kulaumiwa kutokana na watendaji
wake kushindwa kuwajibika ipasavyo.Alitoa
mfano wa kitendo cha Bandari ya Dar es Salaam kutumiwa kupitisha pembe
za ndovu wakati maofisa polisi wakiwemo ni kitendo cha aibu ambacho
kinatosha kumfanya Waziri Nchimbi ajiuzulu.Akijibu
madai hayo wakati akihitimisha kongamano hilo, Waziri Nchimbi alikiri
kuwa baadhi ya polisi wamekuwa na tabia ya kujihusisha na rushwa na
katika kupambana na hali hiyo, Serikali imeshawatimu kazi askari 101
katika kipindi cha mwaka 2012.Hata
hivyo, Dk Nchimbi alisema suluhisho la matatizo yaliyopo ndani ya Jeshi
la Polisi siyo kuwatimua kazi askari pekee na ndiyo maana Serikali
imeanza mkakati wa kutoa mafunzo ya maadili ili kuwawezesha kufanya kazi
zao kwa weledi.Alisema
ataendelea kupokea changamoto kutoka kwa wadau wote wa amani na
kupongeza waliobuni kongamano hilo, huku akiahidi kutoa ushirikiano
kufanikisha jambo lolote linalohusiana na mjadala wa amani ya nchi.
Kuhusu
ubakaji na utesaji wa wanajeshi, Dk Slaa alisema inasikitisha kuona
jeshi ambalo linapaswa kulinda amani linatesa na kuwabaka raia.
Kauli
hiyo iliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ambaye
alisema anao ushahidi wa wanachama wa chama chake waliojeruhiwa na
kupakwa pilipili akisema kwamba jeshi hilo limekuwa na baadhi ya askari
wakatili tofauti na misingi ya kuanzishwa kwake.
Akijibu
tuhuma hizo, Brigedia Jenerali Athanas alikanusha madai hayo akisema
siyo kweli kwamba JWTZ linaendesha unyama na kwamba lipo Mtwara kwa
ajili ya kulinda amani na kusema tuhuma hizo ni za mitaani.
Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), alidai kuwa tangu nchi ilipopata uhuru
haijawahi kuwa na amani ya kweli akitoa mfano wa wananchi kuhamishwa kwa
nguvu katika maeneo yao.
Alisema
katika siku za karibuni, tofauti na zamani polisi ilipokuwa ikifanya
kazi ya kudhibiti uhalifu, sasa inaonekana kama kazi yake ni kudhibiti
upinzani na limekuwa likituhumiwa mara kwa mara kwa kufanya vitendo vya
uvunjifu wa amani na kusababisha mauaji.
NA MWANANCHI