STRAUSS KAHN
Aliyekuwa kiongozi wa Shirika la Fedha ulimwenguni – IMF Dominique Strauss-Kahn atakabiliwa na kesi nyingine kuhusiana na madai ya kuendesha biashara ya ukahaba katika mji wa Lille nchini Ufaransa.
Kesi hiyo mpya inazingatia madai kuwa viongozi wa kibiashara na polisi waliwapeleka makahaba katika tafrija za ngono kwenye hoteli ya Carlton mjini Lille.
Waendesha mashitaka mwezi Juni walitaka mashitaka dhidi ya Strauss-Kahn mwenye umri wa miaka 64 yafutwe, wakisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumfungulia kesi.
Lakini ofisi ya waendesha mashitaka mjini Lille imesema mahakimu wanaoendesha uchunguzi watamshtaki Strauss-Kahn na watuhumiwa wengine 12 kwa mashitaka madogo ya kushiriki katika kuwafanyisha wanawake ukahaba kama sehemu ya kundi.

Kama atapatikana na hatia, Strauss-Kahn anaweza kukabiliwa na adhabu ya hadi miaka kumi jela na faini ya hadi Euro milioni 1.5.
Hiyo ni mojawapo ya kesi ambazo zimejitokeza hadharani baada ya kujiuzulu kutoka Shirika la Fedha ulimwenguni IMF kwa madai ya kumdhalilisha kingono mhudumu  mmoja wa hoteli mjini New York.