Kundi
la Muslim Brotherhood limeapa kuendelea na maandamano ya amani kupinga
kuondolewa madarakani kwa Rais Mohammed Morsi na jeshi la nchi. Wafuasi
wa Mosri wamekua wakiandamana mjini Cairo karibu na kambi kuu ya jeshi
anakoaminika amezuiliwa
Taarifa
ya Brotherhood inajiri wakati kumetolewa kibali kuwakamata viongozi
wake wakuu. Hapo Jumatatu wiki hii wafuasi wa kundi hilo zaidi ya 50
waliuawa katika makabiliano na jeshi.
Huku
haya yakiarifiwa Marekani imetangaza kwamba itatoa ndege za kivita aina
ya F-16 kwa jeshi la Misri katika majuma yajayo. Utawala wa Rais Barack
Obama inaendelea kutafakari matukio yaliyotokea Misri wiki jana.
Ufadhili
wa jeshi ungesitishwa mara moja endapo mwingilio huo wa jeshi
ungelionekana kuwa mapinduzi. Hapo Jumatano maafisa wa Misri walitoa
kibali cha kukamatwa viongozi wa Muslim Brotherhood akiwemo kiongozi
mkuu Mohammed Badie.
Viongozi
hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia ambapo wafuasi wao waliuawa pamoja
na maafisa watatu wa usalama. Tayari ratiba ya uchaguzi mpya
imetangazwa na Rais mpya anatarajiwa kuchaguliwa mwakani sawa na bunge.
Katiba
itafanyiwa marekebisho na kupigiwa kura ya maoni kabla ya mwisho wa
mwaka huu.Kundi la Brotherhood limepinga mpango mpya na kuapa
halitashiriki mchakato wowote bila Mohammed Morsi kurejeshwa madarakani.
BBC SWAHILI