Gazeti la Daily Mirror leo
limebeba habari kuwa baba wa nyota wa timu ya soka ya Chelsea ya
Uingereza John Terry amefikishwa mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa
`shambulio lililotokana na ubaguzi` na pia ameshtakiwa kwa kutishia
kumshambulia mtu mwingine kutokana na hisia za kibaguzi.Makosa yote hayo
aliyafanya kwenye tukio moja,ugomvi uliotokea katika mtaa mmoja jijini
London.
Mzee Terry mwenye umri wa miaka
59,alitiwa mbaroni Machi 22 mwaka huu baada ya kutokea ugomvi aktika
mtaa mmoja uitwao Frenchurch ndani ya jiji la London,nchini Uingereza.
Alisomewa mashtaka yake leo asubuhi katika kituo cha Polisi cha
Bishopsgate wakati akiripoti kwenye dhamana aliyopewa.Watu wengine
wawili,Tudor Musteata,47, na Stephen Niland wanahusishwa katika kesi
hiyo na watafikishwa mahakamani kujibu kesi tarehe 23 mwezi huu katika
mahakama ya jiji la London. Polisi wamethibitisha kuwepo kwa kesi hiyo
lakini hawakutoa maelezo zaidi.
Kesi hiyo ya Terry mkubwa imekuja ikiwa ni mwaka tu tangu mtoto
wamzee Terry John afutiwe mashtaka mahakamani kutokana na kesi
iliyomkabili ya kumtolea lugha ya kibaguzi mchezaji wa Queen`s Park
Rangers Anton Ferdinand mdogo wa Rio Ferdinand wa Manchester United
John Terry alikanusha kumtolea lugha hiyo Anton Ferdinand wakati wa mechi kati ya Chelsea na QPR mwaka juzi
Lakini Chama cha Soka cha Soka cha Uingereza kilipingana na maamuzi
ya mahakama ya kumtoa hatiani John Terry na kudai kuwa utetezi wa Terry
ulikuwa ni wa `kutunga na usioendana na tukio`,wakamfungia mechi
nne.Terry hakukata rufaa FA na aliomba radhi kwa kosa lake la kutumia
lugha isiyofaa.
Lakini alishutumiwa kwa kutomtaka radhi Anton Ferdinand mwenyewe na
Chelsea nao walilaumiwa kwa kuendelea kumuachia Terry unahodha wa timu.
Katika miaka ya nyuma ,2002,John Terry akiwa na wachezaji wengine
wawili,alifunguliwa mashataka ya kuvunja amani baada ya kuibua zogo
dhidi ya baunsa kwenye klabu ya starehe usiku.Aliondolewa mashtaka
baadae.