ROMBO, Ilikuwa ni majonzi, vilio na huzuni katika kijiji cha
Mahalu, wilayani Rombo, Kilimanjaro kufuatia mazishi ya aliyetarajiwa
kufunga ndoa Jumamosi marehemu Levina Swai pamoja na mwanawe.
Marehemu Levina alizikwa na mwanaye kaburi moja
baada ya kichanga hicho kufariki siku hiyo hiyo mara baada ya mama yake
kupoteza maisha kwa kile kilichodaiwa ni kuugua Malaria, shinikizo la
damu kuwa chini na upungufu wa damu.
Marehemu Levina alifariki wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika kijiji cha Mahalu kata ya
Makiidiwilayani Rombo, alikozikwa,wifi wa marehemu, Hortensia Mrima
alisema wifi yake alifia hospitalini na alikuwa mwalimu wa Shule ya
Msingi Nndawa mkoani Lindi akiwa katika mpango wa ajira ya walimu wapya.
“Mimi ndiye nilikuwa namuuguuza hospitalini tangu
Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbuliwa na malaria na kupungukiwa na
damu na pressure (shinikizo la damu) kuwa chini,”alisema Mrima.
Ibada ya mazishi ilianza saa 8:30 mchana
ikiongozwa na Padri Emmanuel Mavengero na kuhudhuriwa na waombolezaji
kutoka Tanga na Kilimanjaro.
Mazishi hayo yalitawaliwa na simanzi huku
waombolezaji wengi akiwamo aliyetarajiwa kumuoa marehemu Levina,Gabriel
Swai muda wote alikuwa akibubujikwa na machozi na kushindwa kuzungumza.
Wifi huyo alieleza kuwa wifi yake alipopimwa
alikutwa na Malaria 13 na kupewa dawa za malaria za SP na dripu za
Quinine ambazo zilimlewesha sana na kuendelea kudhoofu.
“Siku hiyo ya Alhamisi alikata kauli akawa haongei
ikabidi daktari amwekee dripu za Glucose ili kumuongezea nguvu na
shinikizo la damu ilirudi sawasawa lakini bado alikuwa amelegea na
alikuwa haongei,”alisema.
Ilipofika Jumamosi ambayo ndiyo siku iliyokuwa
imepangwa kufunga ndoa na Gabriel Swai, ikabidi madaktari wamuwekee maji
ya uchungu ili kumuokoa mtoto baada ya mama kuwa mahututi.
“Yale maji ya uchungu yalimsaidia akaweza
kujifungua mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo 1.7 na baada ya
kujifungua alipoteza fahamu na saa 8:05 mchana akafariki dunia,”alisema.
Kwa mujibu wa Mrima, mtoto aliendelea kuishi huku
akipewa maziwa lakini alikuwa akiyatapika, hadi ilipofika saa 5:00 usiku
alifariki dunia.