Obama: Tunataka Uwazi wa Mikataba. Omba radhi Kwa mauaji ya Lumumba
Hatimaye Barack Obama, Rais wa Marekani anatembelea tena bara la
Afrika. Hii itakuwa ni mara ya pili Obama kutembelea Bara hili alikotoka
baba yake baada ya ziara yake ya kwanza mwaka 2009. Mwaka huo
alitembelea Ghana na Misri ilhali mwaka huu anatembelea Senegali, Afrika
Kusini na Tanzania. Ziara hiyo itakayoanza tarehe 26 mwezi Juni,
itamfikisha Tanzania tarehe 1 Julai na kuondoka siku ya pili yake.
Uchaguzi wa Obama kuwa Rais wa
Marekani ulipokolewa kwa shangwe Afrika nzima. Wakati Waziri wa mambo ya
nje wa Nigeria alilia kwa furaha, nchi ya Kenya ilitangaza siku ya
mapumziko na Rais wa zamani wa Afrika Kusini ndugu Nelson ‘Madiba’
Mandela alisema ‘ushindi wa Obama unawafanya Waafrika wathubutu kuota
ndoto (Jarida la The Economist). Hapa Tanzania kulikuwa kuna shamra
shamra za kila namna na magazeti yaliweka vichwa vya habari kana kwamba
ni Rais wa Tanzania aliyechaguliwa.
Waafrika walikuwa na matumaini makubwa sana na bwana Obama. Yamefikiwa?
Ni vema ifahamike kuwa Barack Obama ni Rais wa Marekani na siku
zote atalinda maslahi ya Marekani tu. Kuwa na matumaini makubwa kwamba
labda yeye angeliweza kuiweka Afrika mbele sana ilikuwa ni kujifurahisha
tu nafsi. Maslahi ya Marekani ni ya kipaumbele kuliko kitu kingine
chochote kwa Rais Obama. Kwa wengi Obama amekuwa kama amewavunja moyo.
Tanzania inapokea kiongozi wa Taifa kubwa duniani wa pili sasa
ndani ya kipindi cha miezi 3 tu. Kwanza alikuja Rais wa China na sasa
wiki hii anakuja Rais wa Marekani. Maneno ya mtaani na kwenye mabaraza
ya majadiliano ni kwamba viongozi hawa wanakuja kugombea maliasili
tulizo nazo kama gesi asilia na madini. Nadhani haya ni maneno ya kusema
katika kupiga soga maana kunyonywa kwa rasilimali hakuhitaji Rais wa
Marekani aje Tanzania. Makampuni yote makubwa yanayochimba dhahabu hapa
nchini ni makampuni ya nje na marais wao hawakuja ili waweze kupata
mikataba minono ya kuvuna utajiri wetu. Katika kitalu namba 2 cha
utafutaji wa mafuta na gesi huko Bahari Kuu kampuni ya kimarekani ya
ExxonMobil ina ubia na kampuni ya Norway ya StatOil. Kampuni hiyo
haikusubiri Rais wa Marekani aje ili wapate mikataba.
Kuna makampuni mengi sana ya kichina yanajenga barabara zetu hapa
nchini yakiwa na mikataba minono sana. Kule Mchuchuma na Liganga kuna
kampuni ya kichina inajiandaa na uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe.
Makampuni yote haya hayakusubiri Rais wao aje.
Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ujio wa Marais mbalimbali nchini
ni ujio wa kujijenga kidiplomasia na wakati mwingine kama sehemu ya
kutuma ujumbe Fulani kwa dunia. Nchi inayotembelewa pia inaweza kuona
kuwa diplomasia yake inaheshimiwa na mataifa yanayoitembelea.
Hata hivyo hii haiondoi ukweli kwamba Obama anakuja kwa ajili ya
maslahi ya nchi yake kama ilivyo kwa wachina walivyokuja. Tumesikia Rais
Obama ataambatana na mamia ya wafanyabishara kutoka Marekani kwa ajili
ya kupata fursa za kuwekeza nchini. Pia tutasikia matangazo kuhusu
msaada wa pili wa Millenium Challenge ambapo Wamarekani wanaendelea
kumwaga pesa nchini kusaidia miundombinu lakini pia kushawishi kuungwa
mkono na nchi zetu kwenye maamuzi Fulani Fulani jumuiya za kimataifa.
Tumesikia Obama atakwenda kutembelea mitambo ya kampuni ya
Symbion. Hii ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele kuwa
ni mitumba na hivyo TANESCO wasiinunue. Hawakununua na badala yake
kampuni hiyo ya kimarekani ikainunua, wakaingia mkataba na TANESCO
kuwauzia umeme unaozalishwa na mitambo hiyo hiyo chakavu. Wakati
tunasuburi kulipa takribani tshs 105 bilioni kwa Dowans baada ya
kutubwaga kwenye kesi, tunasubiri kuona wanasiasa watakaokwenda
kumsindikiza Obama kwenye matembezi hayo ya kutembelea mitambo chakavu.
Kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE
imetangaza kuingia ubia na kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini.
Takribani 400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya
Taifa. Pia sehemu kubwa ya umeme utakaozalishwa Mtwara tayari umepata
soko kwenye kiwanda cha kuzalisha udongo ulaya (simenti) cha bwana
Dangote kule Mtwara. Mtendaji Mkuu wa GE bwana Jeff Immelt ametangaza
kuwa kampuni yake itauza mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
mingi zaidi Afrika Mashariki kuliko Marekani katika kipindi cha miaka
mitatu ijayo. Ni biashara tu!
Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwa ziara ya Rais Obama.
Kwa nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri
kipaumbele hiki watu wengi watakiiunga mkono. Hata hivyo Obama ni lazima
asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata
miakataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo na kulipa kodi
inavyostahili. Makampuni ya mafuta kutoka Marekani hayana historia nzuri
duniani na hivyo ni lazima tulisisitize mapema kabisa. Uwazi wa
mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika
vita dhidi ya Ufisadi na ubadhirifu.
Rais Obama atambue kuwa iwapo Tanzania ingekuwa inakusanya nusu
ya kodi zinazokwepwa na makampuni makubwa yanayotumia mbinu kali, basi
tungehitaji misaada ya Marekani na hapa nchini angekuja kama mbia wa
kweli na sawa katika dunia. Hivyo ni vema aungane na Waziri Mkuu wa
Uingereza kuhakikisha kuwa makampuni makubwa hayatumii ‘tax havens’
kukwepa kodi katika nchi kama Tanzania. Uwazi wa mapato yao na
kilicholipwa kwa Serikali ni vema usisitizwe sana na Obama mwenyewe ili
makampuni yao yasikie na yaache kupora utajiri wa Afrika kiujanja
ujanja.
Mwisho ni vema kama Rais Obama ataomba radhi kwa ushiriki wa
Marekani kwenye mauaji wa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo Patrice
Lumumba. Hivi Tanzania inahangaika zaidi ya uwezo wake kupeleka majeshi
huko mashariki ya Kongo kulinda amani. Waafrika wengi tunaamini kuwa
mauaji ya Lumumba ilikuwa ni kama laana kwa Taifa lile na hivyo limekuwa
ni taifa la vurugu na vita licha ya utajiri mkubwa ulioko nchini humo.
Nyaraka za CIA zinaonyesha dhahiri kuwa Rais wa Marekani wa wakati huo
Lyndon Johnson aliagiza kuuwawa kwa mwanamapinduzi Patrice Lumumba.
Kuwaomba radhi Waafrika na hasa Wakongo kuhusu mauaji ya Lumumba ni
jambo litakaloweza kusaidia sana kurejesha amani Kongo.
Karibu Afrika, Karibu Tanzania ndugu Barack Hussein Obama.
Zitto Z Kabwe
Makala haya yanatarajiwa kutoka kwenye gazeti la MWANANCHI, mfululizo wa makala kuhusu ziara ya Obama.




