Msemaji na waziri Kivuli, Sheria, Katiba na Utawala kambi ya Upinzani Bungeni Mh Tundu Antiphas Mughwai Lissu.Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(CHADEMA) jana ‘alimtunishia msuli’ Spika wa Bunge, Anne Makinda wakati
wa kujadili Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa
Mwaka 2013.
Hali hiyo, ilijitokeza wakati Lissu
alipokuwa akitoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kuhusu muswada
huo, kutokana na wadhifa wake kama msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya
Sheria na Katiba.
Lissu, alikuwa akitoa maoni hayo baada ya
muswada huo kuwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema, ambao unapendekeza marekebisho ya sheria tatu.Sheria
hizo, ni Sheria ya Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura 292,
Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171 na Sheria ya Utumishi
wa Umma, Sura ya 298.
Malumbano
kati ya Lissu na Spika Makinda, yalianza wakati Mbunge huyo alipokuwa
akisoma maoni ya Upinzani, aliilaumu CCM kwa kutumia vibaya vifungu 115
(1) (a) vya Sheria ya Uchaguzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa na
kifungu 111 (1) (a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Alisema CCM
imekuwa na utamaduni mbaya wa kuwarubuni wanachama wake kufungua kesi
za uchaguzi dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani.
“Kwa kutumia vifungu hivyo vya
sheria, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejenga utamaduni mbaya wa kurubuni
wapiga kura ambao ni wanachama wa CCM kufungua mashauri ya uchaguzi
mahakamani dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani waliochaguliwa katika
uchaguzi. “Katika kesi hizo, CCM na au wagombea wake walioshindwa
wamekuwa wakilipia gharama zote za kuendesha kesi hizo, ikiwa ni pamoja
na kuwalipa mawakili na gharama za usafiri, chakula na makazi ya
wanaofungua kesi hizo na mashahidi wao,” alisema.
Wakati akiendelea kutamka maneno hayo, Spika Makinda alimkatisha akimweleza kuwa kinachojadiliwa ni sheria na siyo CCM.
“…Mheshimiwa Tundu Lissu hapa
tunazungumzia sheria siyo CCM… utaandika sheria kwa kuandika CCM kweli?”
alisema na kumtaka Lissu kufuata utaratibu.
Hata hivyo, Lissu alisema anachofanya ni kuzungumzia sheria na upungufu ambao umekwisha kujidhihirisha.
“Mheshimiwa Spika, mimi nazungumzia sheria hii na upungufu ambao umekwisha kujitokeza…,” alisema.
Hata hivyo, Spika alimkatisha na
kumuamuru akae. Makinda aliendelea kumweleza Lissu kwamba, kilichokuwa
kinafanywa ni kutunga sheria na kwamba masuala ya siasa yafanyiwe kwenye
majukwaa.
“Najua Tundu Lissu, anazifahamu
kanuni na taratibu…lakini akiamua kuzikunja anazikunja,” alisema Makinda
na kumtaka Lissu aendelee kusoma hotuba yake ingawa hakusema ayafute
maneno hayo.
Pengine kwa kuona hakutakiwa kuyafuta
maneno hayo, Lissu aliendelea kusoma hotuba yake ambayo kwa kiasi
kikubwa iliishutumu CCM kwa kutumia vibaya sheria hizo.
Alisema baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010, CCM iliwafungulia kesi wabunge 14 wa Chadema na kati ya hao
wabunge 11 walifunguliwa na wapiga kura wanachama wa CCM.
Alisema CCM pia iliwafungulia kesi wabunge watatu wa NCCR-Mageuzi, huku kesi zote hizo zikifunguliwa na wanachama wa CCM.
Alisema kesi zote, zilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu.
Aliwalaumu wakuu wa CCM, Katibu Mkuu
wa zamani, Yusufu Makamba na Katibu Mkuu wa sasa, Abdulrahman Kinana,
akidai wote kwa nyakati tofauti waliandika barua za kuelekeza
kufunguliwa kesi hizo.
Lissu aliilaumu Serikali kwa
kutowasilisha bungeni marekebisho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kupiga
marufuku mpiga kura kufungua kesi dhidi ya mbunge aliyeshinda uchaguzi,
kwa kuzingatia kutupiliwa mbali na Mahakama ya Rufani kesi ya uchaguzi
iliyofunguliwa na wanachama wawili wa CCM kupinga ushindi wa Godbless
Lema kama Mbunge wa Arusha Mjini.
“Kawa maneno mengine, kwa mujibu wa
uamuzi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Desemba 20, 2012, katika Shauri
Namba 47 la 2012 kati ya Godbless Jonathan Lema dhidi ya Mussa Hamisi
Mkanga & wenzake wawili, wapiga kura anmbao haki zao kama wapiga
kura hazikuathiriwa na matokeo ya uchaguzi husika, hawana haki ya
kulalamikia matokeo ya uchaguzi huo.
“Hivyo Serikali hii ya CCM, ingeleta
kama muswada huu mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 111 (1q) (a) x
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu 115 (1) (a) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuviwianisha vifungu hivyo
na uamuzi huu wa Mahakama ya Rufani,” alisema.
CHANZO MTANZANIA