Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Sunday, June 23, 2013

SITTA::VURUGU ZA ARUSHA HAZIJATISHIA JUMUIYA

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema fujo zilizotokea Arusha hazijatishia miundombinu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema kama kuna nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayofanya ushawishi wa kuhamisha makao makuu katika nchi zao, ni upuuzi.
Sitta aliyasema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na NIPASHE .
Kauli hiyo ya Sitta inafuatia taarifa za uvumi kuwa baada ya mjini wa Arusha kukumbwa na vurugu za mara kwa mara na
Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa mjini humo, baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo wameanza kujiandaa kuhamishia makao hayo nchini mwao.
“Sina taarifa ya nchi jirani kugombania na kushawishi makao makuu yahame Arusha. Hilo litakuwa ni upuuzi…huko kuna fujo kubwa zaidi kuliko zilizotokea Arusha,”alisema.

Alitoa mfano wa vurugu zilizojitokeza nchini Kenya katika mji wa Nairobi baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2008/9, nchini Uganda mwaka 2011 zilizohusisha Al-Shabab na Rwanda ambapo kuna tishio la waasi mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alisema isitoshe fujo za Arusha hazijatishia miundombinu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumzia kuhusiana na athari, Sitta alisema mbali na vifo na majeruhi ni za kiuchumi kwa sababu watalii waliokuwa wafike katika jiji hilo kuona vivutio watafuta safari zao.

Alisema kufutwa kwa safari hizo kunapunguza watalii na hivyo mapato yanayotokana na fedha za kigeni yatapungua.

Jiji la Arusha lilikumbwa na mlipuko wa bomu mwezi Mei, mwaka huu katika Kanisa Katoliki Parokia Olasiti ambapo watu watatu walipoteza maisha.

Juni 15, mwaka huu, kulitokea tena mlipuko wa bomu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika eneo la Soweto, kata ya Kaloleni jijini Arusha, wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani ambapo watu wane walipoteza maisha.

Baada ya tukio hilo, zilifuatia tena vurugu wakati wa a kuaga miili ya watu hao waliofariki dunia baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu.

ULINZI MPAKANI NAMANGA WAIMARISHWA
WAKATI huo huo, matukio mfululizo ya ulipuaji mabomu jijini Arusha yaliyotokea katika kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti na Uwanja wa Soweto kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yamesababisha ulinzi uimarishwe katika mpaka wa Namanga, ulio karibu na nchi ya Kenya.

Afisa Mkuu Mfawidhi wa Uhamiaji, Kituo cha Namnaga, Naibu Kamishna, Albert Kishe, alisema jana wakati
akizungumza na wanahabari.

Alisema ulinzi kwa sasa ni mkubwa na umeimarishwa sana tofauti na miezi ya nyuma na ukaguzi wa wanaoingia na kutoka kupitia mpaka huo umeimarishwa pia.


Kishe alisema hali iliyojitokeza imewalazimu kuongeza ulinzi, na imewasaidia kufahamu idadi ya wageni wanaoingia nchini, kupitia mpaka huo kwa kila siku, ambao ni kati ya 200 na 300.
Mbali na kuimarisha ulinzi mpakani hapo, pia wameamua kuweka nguvu kubwa kudhibiti njia za panya, ambazo kwa kiasi kikubwa hutumiwa na wajanja kupitisha wahamiaji haramu, kutoka nchi za Somalia na Ethiopia.

‘’Kutokana na hili suala la kuimarisha ulinzi, tunashirikiana na Polisi wa Longido na tumeanza Operesheni maalum kwenye njia zote za panya, ambazo hupendwa sana kutumiwa na wahamiaji haramu na tumeanza kuona mafanikio makubwa," alisema.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wameweza kukamata magari mawili aina ya fuso, kwa nyakati tofauti yakiwa na wahamiaji haramu 250, kutoka nchini Ethiopia.

"Lakini magari haya ya mizigo yalitumiwa zamani kwa manamba, ila hadi leo tunashangaa kuona watu wanakubali kugeuzwa manamba na kupakizwa katika lori au fuso ambalo moja wapo tulikuta wamepangwa raia wa Ethiopia 95, wote wakiwa wamesimama wima, na kukosa hata eneo la
kupiga hatua," alisema.

Alisema tayari wahamiaji hao walichukuliwa hatua za kisheria kwa kufikishwa mahakamani, huku baadhi yao wakihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na magari yao kutaifishwa na waliohusika kuwasafirisha walitozwa faini ya shilingi milioni tano.

Kishe alitoa rai kwa watu wanaokwenda nje ya nchi kupitia mpaka wa Namanga kuhakikisha wanafika mpakani wakiwa tayari wana hati za kusafiria na wasidhani kuwa hati hizo, zinapatikana mpakani hapo.

Alisema hati za kusafiria zipo za muda mfupi ama za muda mrefu na hutolewa Arusha mjini, hivyo wananchi wasikubali kuingizwa kwenye mitego na baadhi ya
matapeli, ambao hudanganya watu kuwa wanaweza kupata hati mpakani hapo.

Naye Mkuu wa Utumishi uhamiaji Namanga, Semu Mwailima, amewataka wananchi wanaoelekea Wilaya ya Longido, kuhakikisha wanatembea na kitambulisho, ili kuepuka matatizo.

Mwailima alisema wameanzisha utaratibu kwa kushirikiana na Polisi Longido kwa kukagua magari yote ya abiria na binafsi, yanayoingia Longido, huku wakikagua kila raia, kwa kuangalia kitambulisho chake ili
kumtambua.


SOURCE: NIPASHE
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...