
Rais Barack Obama amepongeza hatua zilizopigwa na Afrika katika kujenga demokrasia, imeelezwa kutoka Dakar, Senegal.
Obama
alisema jana baada ya kukutana na Rais Macky Sall wa Senegal alikowasili
juzi usiku ukiwa ni mwanzo wa ziara yake ya nchi tatu za Afrika,
Tanzania ikiwamo.
Alisema Senegal ni moja ya wabia wakubwa wa Marekani katika bara la
Afrika na inaonekana kuwa mfano wa utawala bora. Nchi zote anazotembelea
– Senegal, Afrika Kusini na Tanzania- zina demokrasia ya kweli.
Katika ziara yake hiyo nchi za Kenya ambako baba yake alizaliwa na
Nigeria ambayo inaongoza Afrika kwa uzalishaji mafuta jamii ya petroli
lakini imekumbwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu,
hatazitembelea.
Maofisa wa Serikali walisema kutuhumiwa kwa Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) jijini The
Hague, kutokana na ghasia za uchaguzi, ndiko kumesababisha ugumu wa
Obama kupita nchi hiyo.
Ziara yake nchini Afrika Kusini, inatarajiwa kugubikwa na hali mbaya kiafya aliyonayo Rais wa zamani Nelson Mandela.
Hata hivyo, Ikulu ya Marekani, imesema itafuata kitakachoamuliwa na
familia ya Mandela ya kama ana uwezo wa kumpokea Obama akiwa
hospitalini.
Obama na Mandela walikutana mwaka 2005, wakati Rais huyo wa zamani wa
Afrika Kusini alipokwenda Washington, DC, kipindi Obama akiwa ndiyo
kwanza amechaguliwa useneta, ambapo wawili hao tangu wakati huo walikuwa
wakiwasiliana kwa simu.
Lakini matarajio ya muda mrefu ya viongozi hao wawili wa kwanza weusi
wa Afrika Kusini na Marekani kukutana, sasa yanaonekana kushindikana.
Obama alisema Afrika imepiga hatua kubwa katika kufanikisha
demokrasia, akizitaja Senegal, Ghana, Sierra Leone, Ivory Coast na
Niger.
“Senegal ni moja ya mataifa yenye demokrasia katika Afrika na moja ya
wabia wakubwa tulionao katika eneo hili la Afrika. Inaelekea pazuri na
mabadiliko ya kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kama ilivyo,
Waafrika wengi hivi sasa wameamka kudai serikali zao ziwajibike na
kusaidia watu, naamini Senegal inaweza kuwa mfano katika hilo,” alisema
Obama.
“Haitoshi kuwa na uchaguzi, haitoshi kuwa na viongozi waliochaguliwa
kidemokrasia. Mnahitaji kuwa na mahakama huru. Mnatakiwa kuwa na imani
kwa utawala wa sheria. Mnahitaji kuwa na jitihada za kupambana na
rushwa,” Mshauri wa Obama wa Sera ya Mambo ya Nje, Ben Rhodes
alikaririwa akisema.
“Mnahitaji kuwa na juhudi za kupambana na rushwa kwa sababu, kusema
kweli, si nzuri tu kwa demokrasia na heshima kwa haki za binadamu,
lakini ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Afrika.”
Rais huyo wa Marekani anasafiri katika kivuli cha watangulizi wake,
Bill Clinton na George W. Bush, ambao wanakumbukwa kwa mipango yao ya
maendeleo ya uchumi na mapambano dhidi ya Ukimwi.
Baada ya kuzuru Goree jana akifuatana na mumewe, Michelle pia atazuru
shule ya kati ya wasichana ya Martin Luther King akifuatana na mke wa
Rais Sall.
Jumapili atatembelea kisiwa cha Robben ambako Mandela alifungwa kwa
miaka 18 kati ya 27 aliyokaa gerezani. Hata hivyo, bado hakuna uhakika
kama ziara hiyo itafanyika kutokana na hali ya Mandela kuendelea kuwa
mbaya.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, amesema ziara ya
Rais Obama haitaathiri shughuli za kiuchumi wala kuzuia watu kuingia na
kutoka jijini.
Amebainisha kuwa Obama atakapowasili nchini atatembelea na kuzindua
barabara ya Ocean ambayo Manispaa ya Ilala imepanga kuibadili jina na
kuipa jina la Barack Obama Avenue ikiwa ni heshima kwake.
Pia gazeti hili limeshuhudia maandalizi ya mapokezi ya kiongozi huyo,
ambapo barabara kadhaa zinazoaminika kuwa atazitumia katika ratiba yake
zinafanyiwa ukarabati kwa kuwekwa lami na taa.
Akizungumza na mwandishi Dar es Salaam jana Sadiki, alitaka wakazi wa
Dar es Salaam, waitumie vyema fursa ya ujio wa kiongozi huyo nchini na
kuachana na maneno ya mitaani kwamba shughuli zote za kiuchumi
zitasimama.
Kuhusu baadhi ya wafanyabiashara wadogo kuondolewa katika maeneo yao,
Sadiki alisema suala hilo halihusiani na ziara hiyo na kwamba ni
mpango wa Jiji wa muda mrefu kulirejesha katika usafi.
Aidha baadhi ya vyombo vya ulinzi kutoka Marekani vimeanza kuonekana
jijini, ambapo manowari ya Marekani ilionekana ikiwa imeegeshwa pembeni
mwa kisiwa cha Mbudya.



