Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Wilfred Lwakatare, amesema mfumo wa kuwatafuta wahalifu ndani ya Jeshi
la Polisi ni dhaifu kwani pamoja na kutuhumiwa kwa ugaidi matukio hayo
yameendelea kuitikisa nchi katika maeneo mbalimbali.
Akiwahutubia
wananchi wa mjini Bukoba juzi katika Uwanja wa Mashujaa, Lwakatare
alidai kuwa aliwaeleza maofisa wa polisi kuwa amegundua udhaifu wa
kuhoji ili kubaini watuhumiwa na kutaka salamu hizo zimfikie Mkuu wa
Jeshi hilo Saidi Mwema.
Kwa mujibu wa Lwakatare jeshi hilo bado lina safari ndefu ya kuwapata watuhumiwa sahihi wa makosa ya ugaidi.
Alisema udhaifu uliopo ndiyo unaosababisha matukio hayo yaendelee kutokea na watu kupoteza maisha.
Alisema
siku 92 alizoishi gerezani zimemfundisha mambo mengi na kuwa atatumia
siku zote atakazokuwa huru kutoa ushuhuda wa mambo mbalimbali
aliyoshuhudia.
Pia
Lwakatare alimsifu kiongozi wa Jumuiya za Kiisalamu, Shekhe Issa Ponda
kuwa ni kiongozi shupavu aliyemfundisha kuwa jasiri na mtu wa kumwomba
Mungu baada ya kuishi naye gerezani kwa siku kadhaa.
Akizungumzia
hatima yake kisiasa, kiongozi huyo alisema hana uhakika kama atagombea
nafasi ya ubunge lakini alisema hayuko tayari kung’oka Chadema badala
yake ataendelea kupambana na maadui waliomzunguka.
Lwakatare
aliwasili mjini Bukoba kwa staili mpya baada ya wananchi waliokuwa
wamesubiri uwanja wa ndege tangu asubuhi kutangaziwa kuwa kiongozi huyo
angewasili kwa gari akitokea Mwanza.
Alipoulizwa
kama mabadiliko hayo ya ghafla ilikuwa ni kukwepa hujuma ambayo ingeweza
kutokea wakati wa mapokezi yake, Mwenyekiti wa Chadema Bukoba Mjini,
Victor Sherejei alisema kuwa Lwakatare alikosa ndege baada ya kufika
Mwanza na hivyo kutumia gari ili kuwahi mkutano.
Habari na Phinias Bashaya, Mwananchi
Chanzo - Mwananchi