Na Waandishi Wetu
HUKU
mwili wake ukitarajiwa kuwasili Bongo kesho, kifo chake Albert Mangweha
‘Ngwea’ kilichotokea katika hali ya utata Mei 28, 2013 nchini Afrika
Kusini, kimeibua mambo mapya, Ijumaa Wikienda lina mzigo wote.
MAMA MANGWEA NAYE AZIDIWA, AKIMBIZWA HOSPITALI YA MKOA
Habari
kutoka msibani Moro jana zilisema mama mzazi wa marehemu Mangwea,
Denisia Mangwea naye alizidiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro kwa matibabu zaidi.
Kwa
mujibu wa baadhi ya waombolezaji msibani hapo, mama huyo alipata
mshtuko wa moyo kufuatia kifo cha mwanaye ambapo taarifa za kifo hicho
zilimshtua tangu Jumanne mpaka alipozidiwa jana.
HABARI KUTOKA SAUZI SASA
Habari
kutoka kwenye Jiji la Johannesburg ambako Ngwea alifia, mtiririko wa
maelezo ya wenyeji wa Mangwea na Mgaza Pembe ‘M 2 The P’ nayo yanaibua
mapya ambayo awali yalikuwa hayajulikani.
MAELEZO YA SAUTI ZA WENYEJI
Wakizungumza
hewani kupitia redio moja ya jijini Dar, wenyeji wao wawili
waliojitambulisha kwa jina moja moja la Godfrey na Godluck ambao
walikuwa na Mangwea na M 2 The P, kila mmoja alisema lake huku maelezo
yao yakionesha dalili ya kutofautiana au kuzua maswali masikioni mwa
watu.
KUMBE WALITOKA KLABU SALAMA
Godluck
siku hiyo aliwaendesha wawili hao kutoka klabu kurudi nyumbani
walikofikia kwa wiki mbili nyuma ambako ni kwa Godfrey. Godluck alikuwa
akitumia gari lake.
Kwa
mujibu wa Godluck, waliondoka klabu alfajiri kurudi nyumbani kwa
Godfrey au God wakiwa salama salimini. Waligonga mlango, God akatoka
kufungua, wakaigia ndani wote.
Godluck
anaishi sehemu tofauti na nyumba hiyo, lakini kwa sababu saa 2:00
asubuhi Ngwea na M 2 The P walitakiwa kurejea Bongo na ni yeye ndiye
aliyetakiwa kuwapeleka uwanja wa ndege, hivyo aliamua kulala palepale.
Alisema wakiwa chumbani, watu wanne, yeye, Ngwea, M 2 The P na mwenyeji Godfery, Ngwea alianza kuonesha dalili za kushangaza.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Radhia Msuya (katikati) akibadilishana mawazo na baba mdogo wa marehemu David Mangweha (kulia) na mama mdogo Ella (kushoto).
“Kule
chumbani Ngwea alikuwa ananilalialalia huku amelegea, nikawa namuuliza
we vipi? Hanijibu, mara akanitapikia, nikamwamsha hakuamka, nikamwamsha
God (Godfrey) na kuuliza huyu vipi? Nikamwamsha M 2 The P, nikamuuliza
huyu vipi, mbona ananitapikia, akasema huyo ndiyo zake akilewa huwa
anakuwa hivyo, si unajua mambo yake tena,” alisema Godluck akikariri
maneno ya M 2 The P.
Aliendelea
kusema kuwa ghafla alimuona M 2 The P naye kama akaanza kuzidiwa.
“Nikamuuliza we vipi? Lakini nikajua labda ni haya mambo yao, maana
unajua mimi nilikuwa siwaelewielewi,” alisema Godluck.
Alisema
ilipofika saa mbili asubuhi, akiwa anajua wasafiri hao wameshachelewa
ndege, yeye aliamua kuondoka kurudi kwake ambako si mbali akipanga
kwenda kulala hadi mchana.
Akasema:
Lakini nikiwa nakwenda nyumbani, NILIMPIGIA SIMU MIDO, dogo mmoja
anaishi jirani, nikamwambia wale jamaa (akina Ngwea) kama wamezidiwa,
nenda kawacheki.
Alisema
akiwa amelala, aliamshwa na simu ya Mido, akaipokea na kuambiwa hali za
jamaa hao ni mbaya sana hivyo yeye akalazimika kwenda na kuwapakia
kwenye gari lake WOTE WAWILI hadi Hospitali ya St. Hellen Joseph ambako
ilithibitishwa na daktari kwamba, Ngwea aliaga dunia ila M 2 The P
hali tete.
MAELEZO YA GODFREY SASA
“Siku ya
mwisho, walitoka wakarudi asubuhi, wakanigongea mlango, nikawafungulia.
Wakaingia, Ngwea akaniambia NICHUKUE ‘KONTAKTI’ (mawasiliano) yake,
nikachukua notebook yangu na kuandika. Walikuwa wazima kabisa.
“Basi, tukawa tunaongeaongea pale kama mtu wa kawaida tu. Hakuniambia kama anaumwa popote wala hakula chochote.
“Baadaye
ndiyo wote wawili wakazidiwa, tukawachukua kuwapeleka hospitali ambako
daktari alisema Ngwea alifariki dunia lakini M 2 The P hali yake ilikuwa
mbaya akalazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).”
KUNA MADAI MAITI YA
NGWEA ILITUPWA NJE YA JIJI
Mtangazaji
alimuuliza Godfrey kuhusu madai kwamba, kabla ya Ngwea kupelekwa
hospitalini, mwili wake ulikutwa nje ya Jiji la Johannesburg ukiwa
umetupwa.
Godfrey:
Si kweli, alizidiwa palepale nyumbani ndiyo tukamchukua kumpeleka
hosptali. NGWEA NILIMPAKIZA KWENYE GARI LANGU, mwenzake alikuwa kwenye
gari la nyuma.
MASWALI MAGUMU
Katika
maelezo ya wawili hao, Godluck alisema alipokuwa anarudi kwake,
alimpigia simu dogo anaitwa Mido na kumwambia kuhusu kuzidiwa kwa akina
Ngwea aende akawacheki, kwa nini asimpigie simu Godfrey ambaye ndiye
mwenyeji wa wawili hao, ndiye aliyewafungulia mlango na ndiye
aliyemwamsha kumwambia kuhusu hali ya Ngwea?
Godluck
yeye alisema aliwapakia wawili hao kwenye gari lake hadi hospitali,
lakini Godfrey alisema alimpakia Ngwea kwenye gari lake na M 2 The P
alipakiwa kwenye gari jingine la nyuma yake (labda la Godluck).
Godfrey,
kwa mtangazaji alikiri kuishi na Ngwea kwa wiki mbili, lakini pia
akasema usiku wa kuamkia kifo chake marehemu alimpa mawasiliano, ina
maana hakuwa na kontakti za Ngwea kwa siku zote kumi na nne alizoishi
pale?
MANENO YA MAMA YAKE MZAZI
Jumamosi
iliyopita, mwandishi wetu mkoani Morogoro alifika msibani na kufanikiwa
kukutana na mama mzazi wa Ngwea, Denisia Mangwea akiwa na majonzi
mazito ambapo alisema:
“Mwanangu
Albert amekwenda, najua sitamuona tena katika maisha ya duniani,
inaniuma sana. Nilimpenda sana na yeye alinipenda sana lakini Mungu
kaamua kumchukua.”
MAZIKO
Kumekuwa
na utata wa kuwasili kwa mwili wa marehemu Ngwea, awali ilidaiwa
ungefika jana na kuzikwa Jumanne, Kihonda Morogoro, lakini baadaye
ikadaiwa mwili huo sasa utawasili kesho Jumanne.
Wakati
hayo yakiendelea, jana Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia
Msuya alikwenda nyumbani kwa baba mdogo wa marehemu Ngwea, David
Mangwea, Mbezi Beach, Dar na kusaini kitabu cha maombolezo.
MUNGU ailaze pema peponi roho ya marehemu Mangweha. Amina.
na global publisher