- Kwa muda wa miaka mitano gharama zimepungua kutoka Sh147 kwa dakika hadi Sh62.
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
imeliambia Bunge kuwa katika kipindi cha miaka mitano, gharama za kupiga
simu zimepungua kwa kiasi kikubwa zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba ambaye alisema kuwa
gharama hizo zimepungua kwa simu za ndani na nje ya nchi.
Makamba alikuwa akijibu swali la Mhonga Said
Ruhwanya (Viti Maalumu-Chadema) ambaye alihoji kama Serikali itakuwa
tayari kutoa mchanganuo wa jinsi gharama za kupiga simu (airtime) kama
zimeshuka kama ambavyo Serikali iliahidi huko nyuma.
Mbali na hilo, mbunge huyo alihoji Serikali
imefikia hatua gani kwamba taasisi zote za Serikali zinaunganishwa na
mkongo wa Taifa ili kuondokana na gharama za mawasiliano na akataka
kujua ni lini Mikoa ya Zanzibar itaunganishwa.
Naibu Waziri alisema katika kipindi cha kuanzia
mwaka 2009, gharama za simu zimepungua kutoka Sh 147 kwa dakika na kuwa
Sh 62 kwa dakika katika kipindi cha mwaka huu punguzo linalolingana na
asilimia 57.
Alisema kuwa gharama za kupiga simu kutoka mtandao
mmoja kwenda mtandao mwingine zimepungua kutoka Sh 115 mwaka 2012 kwa
dakika hadi kuwa Sh 34.92 iliyoanza kutumika mwaka 2013.
Alisema hadi sasa taasisi 23 za Serikali pamoja na
Makao Makuu ya mikoa 24 ya Tanzania Bara zimeunganishwa kwenye mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano.
Kuhusu Mikoa ya Zanzibar alisema Serikali kupitia
makubaliano maalumu na Serikali ya watu wa China, imesaini mkataba wa
Dola 403 milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa mkongo awamu ya tatu
ambao utapelekwa huko na kumalizia maeneo yaliyobaki.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi