Kijana William ambaye anadaiwa kufanya kazi ya utapeli katika majengo
ya ibada anapokuwa misikitini hutumia jina la Hassan Idd Lumbanga ambalo
ni la bandia. Siku zote za mwizi ni arobaini basi zilitimia kwa kijana huyo baada ya siku hiyo kufika katika Msikiti wa Ijumaa Miyomboni akaungana na waumini katika swala iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Imamu wa Msikiti, Issa Boki, ghafla (kijana huyo) alijiangusha chini na kujifanya amepoteza fahamu . Naibu Imamu Boki aliliambia gazeti hili kuwa iliwalazimu kusitisha shughuli za ibada na kutafuta gari harakaharaka na wakamkimbiza kijana huyo katika hospitali ya mkoa ili akapatiwe tiba. |
“Tulimuacha hapo hospitali kwani alilazwa lakini baada ya sisi kuondoka alianza kufanya fujo akahamishiwa wodi ya wenye mtindio wa ubongo, ambako nako alifanya vurugu,” alisema Boki.
Akifafanua zaidi, kiongozi huyo alisema walishitukia kijana huyo akiwa amerudi msikitini na kuanza kuomba msaada wa nauli akidai anataka kurudi kwao Katavi.
“Alichangiwa shilingi hamsini na tano elfu na mia mbili (55,200) wakati tunajiandaa kumpatia mmoja wa waumini wetu alimtambua kuwa alimuona jijini Dar es Salaam katika msikiti mmoja na akafanya kama alivyotufanyia sisi,” alisema Boki.
Naye Katibu wa Msitiki, Juma Kibasila alisema baada ya madai hayo, walimhoji kijana huyo na akakiri kuwa yeye ni tapeli na kwamba amekuwa akiishi kwa njia hiyo na walipompekua walimkuta akiwa na funguo nyingi, hivyo kumkabidhi kwa polisi wa kituo cha kati ambako aliwekwa korokoroni akisubiri upelelezi.