Kilimanjaro
Premium Lager – wadhamini wakuu wa timu ya Yanga imetoa kiasi cha
shilingi milioni 25 kama zawadi kwa timu hiyo kwa kushinda Ligi Kuu ya
Vodacom 2012/2013.
Akikabidhi
hundi ya Sh milioni 25 kwa Yanga SC, Meneja wa bia ya Kilimanjaro
Premium Lager, George Kavishe alisema Kilimanjaro Premium Lager
imefurahishwa sana na ushindi wa timu ya Yanga na kusema imejizatiti
kikamilifu kuisaidia timu ambayo imeibuka bingwa katika ligi yenye
ushindani mkubwa kutokana na kuibuka kwa timu mpya zenye nguvu.
“Yanga
imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa ligi kuu, na sio
ajabu wao kuibuka washindi wa Ligi hii. Napenda kuwapongeza wachezaji
wa Yanga, kocha na Uongozi mzima wa Yanga kwa matokeo mazuri ya
kushinda Ligi kuu kwa mara ya 24 sasa.”
Kavishe
aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 ya udhamini wa
Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga na imetolewa kwa lengo la
kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi zaidi na kusaidia klabu katika
maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ambayo tayari Yanga
ina sifa za kushiriki kutokana na ubingwa waliojipatia.
Akipokea
hundi hiyo, Katibu mkuu wa Yanga , Bwana Lawrence Mwalusako alisema
Yanga inaishukuru sana Kilimanjaro Premium Lager kwa mchango wao.
Aliongeza kuwa Yanga ni timu nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi
imara pamoja na udhamini mkubwa kwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
‘‘Mafanikio
yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio ya kampuni na pia (TBL) na
bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla ambayo imekuwa ikitusaidia
sana. Kilimanjaro Premium Lager imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa
timu msukumo uliopelekea mafanikio haya,’’ alisema Mwalusako.
Mwalusako
aliongeza “Yanga sasa ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la
kimataifa la soka kutokana na mafanikio haya’’. “Tunaamini kuwa
kutokana na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager tutaendelea kukua na
kufanikiwa.’’