Mahakama
nchini Kenya imesimamisha utekelezaji wa nyongeza ya mishahara ambayo
wabunge wa nchi hiyo walipendekeza kujiwekea. Chama cha mawakili nchini
Kenya kiliwasilisha ombi la kutaka kuwekewa amri ya kisheria wabunge hao
siku moja baada ya wabunge hao kupiga kura ya pamoja kutaka wajoingezee
mishahara.
Wanaharakati wamekuwa wakipinga jaribio hilo huku
wakiandaa maandamano katika barabara za jiji la Nairobi wakimuomba rais asiidhinishe kura hiyo.
Hapo jana Rais Uhuru Kenyatta aliwafokea
wabunge hao kwa uamuzi wao huku akisema kuwa mishahara ya wafanyikazi
wote wa Umma inadhibitiwa na tume ya mishahara iliyoundwa.
Wabunge hao wameelezea hasira zao juu ya
tamko la Rais Uhuru Kenyatta na tume ya kudhibiti mishahara ya maafisa
wa serikali ambao wanasema waache vitimbi vyao vya kutaka kuongezwa
mishahara.
Wanatishia kubadilisha sheria ya idadi ya
maafisa wanaoweza kuhudumu katika tume za serikali hadi watatu ,
kupunguza mishahara ya maafisa wa serikali kwa asilimia hamsini na saba
na kuwaondolea wananchi wanaopata chini ya shilingi elfu hamsini kama
ajira uwezo wa kutozwa kodi.
Wabunge hao hata hivyo hawaoni ubaya
wowote wa kulalamika kuwa mishahara yao inapunguzwa wakisema wanasubiri
tume ya bunge kuwalipa mishahara yao ya laki nane na hamsini kutoka laki
tano.