Kufuatia
taarifa za uzushi zinazosemekana zilitokana na kikao cha wabunge wote
wa CCM (CCM party caucus) zilizoenezwa kwenye vyombo mbalimbali vya
habari na haswa kwenye mtandao wa kijamii na watu wenye nia ovu ya
kutaka kuharibu jina zuri la Mhe. Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla (Mb.) kwa kuchafua taswira yake na heshima kubwa
aliyojijengea kwa muda mrefu kwenye jamii, tumeelekezwa kutoa taarifa
hii yenye lengo la kukanusha na kuweka kumbukumbu sawia kwa lengo la
kuuelewesha umma.
Kwanza,
anasema Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), hana tabia za kuwagawa watu
kwa matabaka ya itikadi zao, dini ama makabila yao. Anasema msingi huu
wa kuishi kwa kushirikiana na kupendana anautoa nyumbani kwao Nzega
alipozaliwa na kukulia, kwa babu yake aliyekuwa Sheikh na muasisi wa
Taasisi ya kiislam ya Nusratul qadiriyya (zawia) ambayo ilikuwa na
wafadhili wakuu wakristo na kila mwaka walikuwa wakishiriki kwa hali na
mali kwenye maulid na dua nyingine mbalimbali; miongoni mwa walezi na
wafadhili hao ni pamoja na Hayati Chief Humbi Ziota, Mhe. Lucas Lumambo
Selelii (Mb. Mstaafu wa Nzega na Katibu wa Makanisa ya Pentekoste Mkoa
wa Tabora), Mhe. Steven Maziku Kahumbi (Mb. Mstaafu wa Bukene), Hayati
Mhe. Mzukila (Mb. Mstaafu wa Nzega) – ambao walikuwa ni wa dini ya
kikristo. Ni msingi huo uliomfundisha yeye kuwa mstari wa mbele kwenye
kuunga mkono jitihada za watu wa dini zote na hata wasio na dini katika
shughuli zao za kuendeleza imani zao ama kufanya shughuli za maendeleo
bila kuingilia uhuru ama itikadi zao.
Ni
katika msingi huo huo amekuwa akishiriki kujitolea kujenga makanisa,
misikiti na hata kuchangia kazi za wasanii wa kwaya mbalimbali bila
kubagua kwa misingi ya udini. Watu wa Nzega ni mashuhuda kwa hili. Na
zaidi ya hapo, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) hawezi kuwa wa mstari
wa mbele kuhamasisha ubaguzi wa kidini, jambo ambalo kila siku
analipinga hadharani, na kwamba yeye binafsi ana Ndugu wa damu wenye
wazazi wa kikristo, na waliooa ama kuolewa na wenza wenye dini ya
kikristo na kuzaa watoto na wajukuu wa dini ya kikristo. Na pia si
muumini wa kutafuta umaarufu kunuka unaotokana na kuwagawa watu kwa hoja
dhaifu na mfu kabisa za udini.
Pili,
Mhe. Hawa Ghasia (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(TAMISEMI), HAKUWEPO KABISA kwenye kikao, hivyo yote yanayosemwa na
wazushi hawa ni ya uongo na hayana msingi wowote. Maana Mhe. Ghasia,
asingeweza kumshambulia Mbunge Mwenziye ilhali hakuwepo kabisa kwenye
mkutano huo.
Tatu,
Mhe. Munde Tambwe Abdallah (Mb.), HAKUZUNGUMZA hata mara moja. Hivyo
yote yanayosemwa dhidi yake ni uzushi na uongo wa kupindukia. Nne, Mhe.
Bernard Membe (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa ni rafiki yake mkubwa na wa karibu sana na kama ingetokea
akasemwa kwa nia ya ubaya ama kumharibia sifa na yeye akiwemo kwenye
kikao hicho, bila shaka yoyote ile angesimama kumtetea. Hivyo hili la
Mhe. Membe kusemwa, halikuwepo na ni UONGO wenye nia ovu ya kuwagawa
wanaCCM katika makundi “hasimu ya kulazimisha” ambayo hayapo.
Tano,
anawataka watu wenye mradi wa kumchafua wakome mara moja maana mradi
huu ni dhahiri kabisa haujawalipa mpaka sasa na kamwe hautowalipa. Kama
ni vita za Urais ama Ubunge basi wasubiri 2015 watapambana. Taarifa hizo
za kizushi zilizosambazwa na namna zilivyowekwa ni wazi kabisa
zinalenga kumchafua Mhe. Bernard Membe (Mb.), ambaye ni rafiki yake wa
karibu na anatajwa
tajwa kuwa na uwezekano wa kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwaka 2015, na kwa maana hiyo haihitaji akili ya Albert
Einstein kubaini kuwa ni nani aliye kazini kwenye hili.
Ametutaka tuwaambie hao watu kuwa yeye hayuko tayari kamwe kumuunga mkono mgombea wao, mwenye tuhuma za kifisadi, ambazo hazikwepeki na hazisafishiki, mwenye
tamaa ya mali na madaraka isiyokoma na kwa kuwa yeye siyo mnafiki,
analiweka wazi hili. Na kwamba kama ikitokea kweli Mhe. Bernard Membe
(Mb.) akachukua fomu ya kuwania Urais yeye Mhe. Dkt. Kigwangalla atakuwa
tayari kumuunga mkono na kumfanyia kampeni ya kufa na kupona kwa kuwa
anaamini katika usafi na uzalendo wake, umakini wake na uwezo wake wa
kazi. Na kwa kuwa anaamini kuwa kama Mhe. Membe atakuwa Rais, basi nchi
itakuwa kwenye mustakabali mwema.
Anawasishi
wanahabari kusimama kwenye weledi na kuacha kuandika mambo ambayo
hawana uhakika nayo na bila hata ya kuwahoji wahusika.
Taarifa hii imetolewa leo Tarehe 24/Mei/2013 na;
TeamHamisiKigwangalla
Ofisi ya Mbunge,
Jimbo la Nzega.




