Watetezi
kutoka mikoani ambao ni wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu Nchini (THRD-Coalition), waliokutana kwa siku tatu jijini Dar
es Salaam, pamoja na kupata mafunzo adhimu ya usalama kwa watetezi
yatolewayo na THRD-Coalition, pia walifanya tathmini ya hali ya usalama
kwa watetezi nchini; asasi za haki za binadamu, waandishi wa habari na
watu wanaojitolea katika eneo la msaada wa kutetea wenzao yaani
(volunteers). Tathmini imeonyesha kwamba yapo mambo kadhaa
yanayosababisha kukosekana kwa usalama kwa watetezi nchini na kupotea
kwa amani.
1. Utendaji wa Vyomba Serikali na Vuguvugu la Kisiasa
Serikali
ndicho chombo chenye jukumu la kuwalinda watetezi wa haki za binadamu
na watu wengine waliomo ndani ya mipaka ya nchi yetu, wao na mali zao.
Vitendo vya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, kuteka, kutesa,
kung’oa meno, na macho, kukata vidole na hata kuwarushia bomu waamini
wakiwa katika maeneo ya maombi ni ishara ya dhahiri ya serikali
iliyoshindwa kutimiza majukumu yake. Vitendo vya baadhi ya viongozi
nchini hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa kuwakandamiza watetezi wa
haki za binadamu kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwafungulia kesi za
kubambikiza vimefikia kiwango cha kutovumilika. Matamko mengi
yanayotolewa na viongozi wa juu wakiwamo mawaziri dhidi ya watetezi na
asasi za haki za binadamu nchini yanaonyesha kuwa ni viashiria vya
vitisho vya kiusalama wazi wazi kwa watetezi nchini. Pia watetezi
wamekuwa wakishutumiwa kuwa ni wapinzani kwa sababu kazi zao zimekuwa
zikilinganishwa na kazi za vyama vya upinzani na za kiuchochezi.
Kuwa
mtetezi ni kiungo muhimu katika kuibua na kufichua maovu ili kujenga
utawala unaoheshimu haki za binadamu, lakini siku zote tumejikuta
tukihatarisha maisha yetu. Katika mazingira ya aina hiyo watetezi
hawawezi kujiweka katika kundi salama hata kidogo, bali kwamba usalama
wao umo hatarini kwa sababu kazi nyingi wanazozifanya huwalazimisha
kuikosoa serikali pale inapokuwa haitimizi wajibu wake kuhusiana na
kulinda haki za msingi za binadamu na haki nyinginezo stahiki. Mifano
halisi ya migongano kati ya asasi na serikali ni kesi za kugombea ardhi
Pugu, Loliondo, Bagamoyo na migogoro isiyoisha katika migodi mkoani
Mara.
2. Wamiliki wa vyombo vya habari
Katika
kudadisi ni kwa nini wanahabari wanakabiliwa na changamoto nyingi za
kiusalama iligundulika kwamba wamiliki wa vyombo hawana mikakati mizuri
juu ya suala zima la usalama kwa waandishi wao. Pia malipo finyu kwa
wanahabari ilionekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu baadhi yao
hawapati malipo ya uhakika wala mikataba. Hali hiyo husababisha
waandishi waishi maisha ya kubahatisha na wakati mwingine hujikuta
wakishawishika kuingia katika makundi ya kisiasa ili kuanza kuvitumikia
‘vyanzo vyao’ jambo ambalo husababisha wakiuke maadili ya kazi zao na
mwisho hushambuliwa na wale wanaoguswa na habari za aina hiyo. Aidha
watetezi wanawasihi wamiliki kuanza kuweka mikakati ya kiusalama kwa
waandishi na kuboresha mishahara kwa waandishi ili wafanye kazi kwa
uhakika zaidi.
3. Jeshi la Polisi
Jeshi
la Polisi wawe makini na matumizi ya silaha za moto na nguvu za ziada
ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu wa kudumu. Katika
purukashani nyingi za kisiasa jeshi hilo limeshindwa kabisa kuonyesha
kwamba linafanya kazi ya kuutumia umma wa Watanzania wote na badala yake
limekuwa likichukua mwelekeo wa kuwatumikia wanasiasa au chama fulani.
Aidha askari polisi wanakumbushwa kwamba wao ni sehemu ya jamii na hao
wanaowatesa ni ndugu zao wa karibu wadogo zao mama zao n.k. Jeshi la
Polisi litambue kuwa kazi za watetezi wa haki za binadamu ni kazi halali
zinazolindwa kisheria na wanajukumu la kuweka mazingira mazuri ya
watetezi kufanya kazi zao bila kutekwa, kuteswa ama kungo’lewa macho,
meno, kucha n.k. Mfano halisi wa mapungufu ya jeshi hilo ni kukamatwa
kwa askari hivi karibuni waliokuwa na fuvu la kichwa cha mtu mkoani
Morogoro kwa lengo la kumbambika mtu kesi ya jinai. Tunaisihi Serikali
na Jeshi la Polisi kuanza kutekeleza Tamko la Umoja wa Mataifa la tarehe
15 Machi 2013 linalotaka mataifa yote kutambua umuhimu na uhalali wa
majukumu ya watetezi wa haki za binadamu katika kutetea haki za binadamu
demokrasia, utawala wa sheria, kama nyenzo la kuhakikisha usalama wao
ikiwa ni pamoja na kuheshimu uhuru wa asasi zao na kuepuka kunyanyapaa
shughuli za asasi za kiraia.
4. Wanaharakati na Watetezi wa Haki za Binadamu
Wanaharakati
wote na watetezi wa haki za binadamu wasichukue upande wowote katika
masuala ya itikadi za kisiasa kwani wao ni watu wa kati. Pia
wanaharakati wasijiingize katika matumizi ya nguvu au kupambana na Jeshi
la Polisi. Aidha wanaharakati wametakiwa kuwa waelimishaji wa umma na
kujizuia kujiingiza katika mambo yaliyopandikizwa na watu wasioitakia
mema nchi yetu kama vile udini na migogoro isiyoisha ya kugombea ardhi,
maeneo ya malisho, ukabila n.k.
5. Vurugu za Udini
Kwa
miaka mingi Tanzania haikuwahi kupata misukosuko ya udini kama
inayotokea sasa. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni uhasama wa kidini
umezidi kushamiri. Watetezi kwa umoja wetu tunaamini Tanzania hatuna
udini bali kinachoendelea ni ajenda za watu fulani kwa maslahi binafsi
ama ya kifedha, kidini au kisiasa. Kwa sasa nchi inaweza kutumbukia
katika machafuko ya kidini endapo viongozi wa dini zote, wanasiasa na
serikali hawatachukua hatua za makusudi kuwakomesha wachache hao ambao
wanataka kuondoa amani ya nchi. Katika mazingira haya pia mtetezi wa
haki za binadamu hawezi kubakia salama na ndio maana tunakemea kwa
nguvu zote vitendo hivi viovu.
6. Watanzania Wote Kwa Ujumla
Watanzania
katika ujumla wao wameaswa kuwa makini hususani wakati huu tunapoelekea
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wapo watu wanaochomekea ajenda zao
kwa malengo wanaoyafahamu wao wenyewe na hivyo kuligawa taifa katika
misingi ya udini na mambo mengine kama hayo yasiyo na tija wala manufaa
kwa nchi yetu. Aidha Watanzania wameshauriwa kuirejea kazi nzuri ya
kuwaunganisha ambayo iliifanya nchi hii ifahamike kama kisiwa cha amani
miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.
Mwisho
tunaungana na watanzania wengine kulaani kitendo cha kutupa mabomu
katika mikusanyiko ya watu kama ilivyotekea kule Arusha. Tunawapa pole
wafiwa na majeruhi wote. Na kutaka watanzania wote bila kujadili itikadi
zao kuendelea kulaani vitendo hivi vya kinyama.
TAMKO
HILI LIMEANDALIWA NA WATETEZI 30 WA HAKI ZA BINADAMU TOKA MIKOA
MBALIMBALI KWA NIABA YA WENZAO KATIKA AZIMIO LA KUIREJESHA NCHI HII
KATIKA HALI YA AMANI NA UTULIVU