Mwalimu Mkuu Msaidizi
wa Shule ya Sekondari Holili, Benson Samizi akizungumza na mwandishi wa The Habari hivi karibuni wilayani
Rombo
Geti la mpaka wa
Tanzania na Kenya eneo la Holili, Wilaya ya Rombo.
Baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Tanya wakifanya mazungumzo na mwandishi wa The Habari (hayupo pichani) shule
hii ni miongoni mwa sekondari zilizopo maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Kenya
wilayani Rombo.
Na Thehabari.com,
Rombo
SHUGHULI za biashara
zinazoendeshwa maeneo kadhaa ya mpakani mwa Tanzania na Kenya katika Wilaya
ya Rombo zimeathiri maendeleo ya elimu hasa kwa shule za sekondari
zilizopo pembezoni mwa maeneo hayo kwa kile wanafunzi kujiingiza katika
biashara hizo.
Uchunguzi uliofanywa
hivi karibuni wilayani hapa na mwandishi wa habari hizi umebaini baadhi
ya wanafunzi katika shule za sekondari kutumika katika biashara za
mipakani jambo ambalo linachangia wilaya hiyo kufanya vibaya kielimu
katika matokeo hasa ya kidato cha nne.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti baadhi ya walimu wakuu wa shule za Sekondari za Urauri,
Holili, Tanya, Nduweni pamoja na baadhi ya wadau wa elimu maeneo hayo
wamesema wapo baadhi ya wanafunzi wanajiingiza katika shughuli hizo
ambazo huathiri maendeleo ya taaluma.
Akizungumzia shule
yake, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Urauli, iliyopo Tarakea wilayani Rombo,
Sim Silayo alisema shughuli za biashara zinazofanyika mpakani mwa Tanzania
na Kenya eneo hilo zinaathiri taaluma kwani wapo wanafunzi ambao
hujiingiza katika shughuli hizo na kusahau masomo kwa vipindi tofauti.
Alisema baadhi ya
wanafunzi wanafanya biashara ndogo ndogo na wengine kufanya vibarua mpakani
jambo ambalo limekuwa likichangia taaluma kushuka katika shule hiyo, hasa
nyakati za kilimo na mavuno maeneo ya vijiji vya mpakani Kenya na
Tanzania.
"Kuna kipindi
mahudhurio yanakuwa mabaya kabisa hasa kipindi cha mavuno, kilimo na palizi...wanafunzi
wanakimbilia kufanya shughuli hizo kwa kulipwa, pia si wanafunzi tu
wanaofanya kazi hizi hata baadhi ya wazazi nao hujumuika kufanya vibarua
upande wa pili (Kenya) kwa madai kule malipo ni mazuri zaidi ya nchini
kwetu," alisema Silayo.
Kwa mujibu wa matokeo
ya kidato cha nne Shule ya Urauri mwaka jana, kati ya wanafunzi 92
waliofanya mtihani huo, ni wanafunzi sita tu ndiyo waliofanikiwa kufaulu
huku wanafunzi 44 wakipata daraja la nne na wanafunzi 42 wakiambulia
daraja sifuri.
Mwalimu Mkuu Msaidizi
wa Shule ya Sekondari Holili, Benson Samizi alisema pamoja na sababu nyingine
shughuli za mpakani zimekuwa zikichangia shule hiyo kufanya vibaya kwa
kile wazazi kushindwa kuwadhibiti wanafunzi wanaporudi nyumbani na kuwa
huru kufanya shughuli nyingine zinazowaathiri kitaaluma.
Alisema matokeo ya
kidato cha nne mwaka jana shule hiyo ilifanya vibaya kwani kati ya wanafunzi
94 waliofanya mtihani huo, hakukuwa na ufaulu wa daraja la kwanza, daraja
la pili na la tatu lilikuwa na mwanafunzi mmoja mmoja huku 39 wakipata
daraja la nne na wengine 50 kupata sifuri.
Akizungumzia hali hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya alikiri shule nyingi
kufanya vibaya hasa matokeo ya mwaka jana na kuongeza uongozi wake umeanza
kuchukua hatua kukabiliana na hali zote zinazoathiri maendeleo ya
kitaaluma kwa shule zake.
Alisema kwa hatua ya
kwanza halmashauri ilimgharamia mkaguzi wa shule ambaye alifanya ukaguzi
katika shule mbalimbali zikiwemo zilizofanya vibaya na kutoa mapendekezo.
Aliongeza kuwa ili
kukomesha utoro katika shule hizo viongozi wa serikali za vijiji
waliagizwa kuwashughulikia wazazi wanaoshindwa kuwabana watoto wao katika
kuhudhuria shuleni, ambapo baadhi walianza kutozwa faini mtoto anapokosa
shule jambo ambalo alisema limeanza kuleta mabadiliko.