Dodoma. Waziri wa Viwanda na
Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema wizara yake itachukua hatua za
haraka ili kudhibiti matumizi ya pombe zinazowekwa kwenye pakiti maarufu
kwa jina la viroba ambazo zinaathiri afya za Watanzania wengi.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya
wizara yake bungeni Dodoma jana, Dk Kigoda alisema wizara yake
itawasiliana na wadau mbalimbali ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Dk Kigoda, ambaye pia ni Mbunge wa Handeni,
aliwataja wadau hao kuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Afya na
Ustawi wa Jamii, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Fedha na wamiliki wa
viwanda vinavyotengeneza pombe hizo. “Tumelipokea suala la matumizi ya
viroba kwa uzito wa hali ya juu na tutatoa uamuzi wa haraka baada ya
kufanya mazungumzo na sekta mbalimbali,” alisema Dk Kigoda.
Alisema wizara yake kwa kushirikiana na wizara
nyingine itatafuta njia mbadala kuepusha madhara kwa wanaotumia viroba
ambavyo alisema vina athari kubwa kiuchumi na kijamii.
Alitahadharisha kuwa lazima hatua hiyo ichukuliwe
kwa umakini kwani endapo vitapigwa marufuku, lazima sheria mpya ya
kuzuia kinywaji hicho itungwe.
Tulichobaini
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuhusu unywaji
huo umeonyesha kuwa, idadi kubwa ya watu wanafanya kazi na kutembea
wakiwa wamelewa.
Hivi karibuni imegundulika kuwa wanafunzi wengi wa
shule za sekondari wamekuwa wakitumia vinywaji hivyo kwa kujificha
mithili ya wavuta bangi vichochoroni.
Gazeti hili pia liligundua kuwa wanafunzi hao wanaweza kupata vinywaji hivyo kwa urahisi kwa kuwa gharama yake ni ndogo.
Imebainika kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakifika
kwenye vibanda vya wauza vocha na hata baa za vichochoroni na kutaka
wauziwe vinywaji hivyo ambavyo wamevibatiza jina la juisi.
Mathalan, mmoja wa wauza vinywaji katika eneo la
Gereji External, Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) alisema wanafunzi
wamekuwa wakifika dukani kwake asubuhi wakitaka viroba na kila
akiwauliza husema wanakwenda kuwapa walinzi (hongo) kwa kuwa wamechelewa
kufika shule.
Pombe hizo kwa sasa zinauzwa na wauza karanga, sigara na magazeti katika maeneo ya miji mikubwa nchini.