RAIS
Jakaya Kikwete anatarajiwa kufanya kikao cha siku mbili na wabunge wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujadili masuala mbalimbali ya taifa, ikiwamo
utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika majimbo yao.
Katika
kikao hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, anatarajiwa kuwapa
nguvu wabunge wake katika kueleza masuala mbalimbali, ikiwamo hatua ya
Serikali kupitisha bajeti, huku miradi ya maendeleo ikisuasua katika
utekelezaji kwa madai ya kukosekana kwa fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, alisema kikao hicho ni cha kazi na kitakuwa kinatoa nafasi zaidi
kwa wabunge kueleza masuala yanayoh
Nape alisema kikao hicho hakina
uhusiano wa aina yoyote na matukio yanatokea bungeni hivi sasa, bali ni
ratiba ya kikao cha kazi za Mwenyekiti katika kupima utekelezaji wa
ilani na miradi ya maendeleo katika majimbo mbalimbali ambayo yapo chini
ya wabunge wa CCM.
“Hiki ni kikao cha kazi, ninapenda
kueleweka kuwa CCM ndiyo iliyokabidhiwa jukumu la kuongoza nchi hii na
wabunge wa chama chetu ndiyo wanaisimamia ndani ya Bunge, hasa katika
kuhoji masuala mbalimbali yanayohusu nchi na watu wake.
“Kikao kitafanyika Mei 18-19 mwaka huu na wabunge watakuwa na uhuru wa kusema jambo lolote mbele ya Mwenyekiti wao.
“Katika siku hiyo ya kwanza itakuwa ni fursa kwa wabunge kusema masuala mbalimbali ambayo wanahisi ni muhimu kwa chama chao.
“Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti
atakuwa akisikiliza na atakuja siku ya pili kwa ajili ya kutoa majibu
kwa wabunge pamoja na hatua mbalimbali za kuchukua na ajenda kubwa ni
ushauriano baina ya wabunge na serikali yao.
“Tunapenda kueleza jamii na
Watanzania kwa ujumla kuwa CCM hivi sasa imefanya mambo kadhaa, hasa
katika kuhakikisha inaisimamia vema Serikali yake, ikiwamo katika
utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ambayo ndiyo mkataba kati ya Serikali
na wananchi.
“Ni wazi kabisa hivi karibuni kuna matukio yaliyotokea bungeni, likiwamo lile la Mbunge wa Nkasi Kaskazini.
“Kikao hiki hakina uhusiano kabisa na
jambo hilo, bali ni kuwakutanisha pamoja wabunge wetu ili nao waweze
kutoa madukuduku yao mbele ya Rais hasa katika utekelezaji wa ilani ya
chama chetu,” alisema.
Nape alisema kwa muda mrefu wabunge
wamekuwa wakilalamikia hatua ya serikali kushindwa kutekeleza miradi ya
maendeleo kutokana na madai ya fedha kutopelekwa kwa wakati kama
ilivyoamulia kwa Bunge.
“Ni wazi kabisa siku zote Katibu Mkuu
wetu Abdulrahman Kinana amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
mawaziri wanawajibika kwa moja kwa moja kwa chama na si vinginevyo,
kwani upimaji wa ilani hupimwa na chama kwa kupata taarifa za
utekelezaji wake wa kina,” alisema Nape.
Mgombea ubunge Chambani
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi
alisema aliweka wazi uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichoketi Mei 14,
mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine kilipitisha jina la mgombea
ubunge katika jimbo la Chambani.
Alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM imemteua Mattar Sarahan Said kuwa mgombea wake wa
ubunge katika jimbo hilo katika Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Nape alisema CCM imewateua Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Idd kuzindua kampeni hizo na Mwenyekiti
mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi
atafunga kampeni hizo.
Bomu Arusha
Alisema mbali na hatua hiyo, Kamati
Kuu ilipokea taarifa za tukio la mlipuko wa bomu Arusha na kuridhishwa
na hatua za haraka zilizochukuliwa na serikali kwa kuitaka iwe inatoa
taarifa za mara kwa mara kwa wananchi kutokana na uzito wa jambo hilo.
“Kamati Kuu ilipokea taarifa ya
serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuhusu
tukio la bomu Arusha na kutokana na maelezo ya Serikali, CC imeagiza
hatua zaidi zichukuliwe kuhusu tukio hili, ikiwamo kung’oa mzizi wake
kabisa kuweza kulinda amani na mshikamano wa nchi yetu.
“Ninajua kuna baadhi ya vyama hivi
sasa tayari vimeshatoa matamko kuitaka serikali iombe radhi … lakini kwa
hivi sasa si sahihi hata kidogo, ndiyo maana sisi CCM tunasema kuwa
tuvute subira kwanza kwa kuiachia serikali jambo hili hadi mwisho kuliko
kufanya hivyo,” alisema Nape.