Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Friday, May 17, 2013

Kesi ya Mkurugenzi wa Richmond kuunguruma upya, ni baada ya DPP kuikatia rufaa




MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imefuta hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Saalam, iliyomuachia huru mkurugenzi wa kampuni ya Richmond Ltd, Naeem Adam Gire, limeandika gazeti la Tanzania Daima la leo

Gire alikuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa umma.

Hukumu hiyo ilitolewa kutokana na rufaa Na.126/2001 iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi(PICHANI) dhidi ya uamuzi wa kesi ya kutoa taarifa za uongo kwa Shirika la Umeme la TANESCO Na. 15/2009 iliyokuwa ikimkabili Gire ambapo mwaka juzi Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alimuona hana kesi ya kujibu.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Lawrance Kaduri ambaye katika hukumu yake hiyo alisema alisikiliza hoja za mawakili wa serikali waliokuwa wakimwakilisha muomba rufaa (DPP), Frederick Manyanda na Oswald Tibabyekomya na mjibu rufaa alikuwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa.

“Baada ya kusikiliza hoja zote mbili na pia nimeangalia nakala ya hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomuachia huru Gire kwa maelezo kuwa hana kesi ya kujibu.

“Mahakama hii imefikia uamuzi wa kuufuta uamuzi huo kwa sababu imebaini kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha ulioletwa na upande wa jamhuri kule katika Mahakama ya Kisutu ambapo umejitosheleza kumfanya Gire apande kizimbani na aanze kujitetea,” alisema Jaji Kaduri.endelea kupitia na kukopi  audifacejackson blog.Jaji Kaduri alisema anakubaliana na hoja za wakili wa Tibabyekomya iliyodai kuwa Hakimu Lema alikosea kisheria katika uamuzi wake; alisema kuwa kosa la kughushi limeshindwa kuthibitika, uamuzi ambao jaji huyo alisema hakimu Lema alisema alitumia sheria ambayo ilishapitwa na wakati kwa kusema kosa la kughushi limeshindwa kuthibitika.



Alisema kwa mujibu wa hati ya mashtaka kosa hilo la kughushi, Gire anadaiwa kulitenda Machi 13, 2006 Dar es Salaam, kwa nia ovu; alighushi nguvu ya kisheria ya Machi 13, 2006 kwa lengo la kuonyesha Mohamed Gire ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond Development Company LLC ya Texa America.



Aliongeza kuwa Gire alisaini hati ya nguvu ya kisheria inayompa mamlaka Naeem Adam Gire (mjibu rufaa) wa hapa jijijini kuendelea na shughuli za kibiashara za kampuni hiyo hapa nchini kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 335(d) (iii) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.



“Hivyo basi mahakama hii inakubaliana na mawakili wa mwomba rufaa (DPP), kuwa kosa hilo la kughushi hati ya nguvu ya kisheria liliweza kuthibitishwa na upande wa jamhuri hivyo mahakama hii inatamka wazi Hakimu Lema alikosea kisheria kusema upande wa jamhuri ulishindwa kuthibitisha kosa la kughushi hati ya nguvu za kisheria na kuwasilisha nyaraka hizo ambazo zilighushiwa kwa maofisa wa umma kwa lengo la kuonyesha kampuni hiyo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme hapa nchini wakati si kweli ili ipewe zabuni,” alisema Jaji Kaduri.



Aidha Kaduri alisema mahakama yake imejiridhisha kuwa kosa la kwanza na la pili (kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo) limeweza kuthibitishwa na upande wa jamhuri, hivyo mahakama yake inaamuru kesi ya msingi iliyokuwa imemalizika kwa Gire kuachiliwa huru baada ya kuonekana hana kesi ya kujibu, irudi upya katika Mahakama ya Kisutu na Gire anaanze kujitetea.



Mwaka juzi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waliandware Lema, alimwachilia huru Gire baada ya kumuona hana kesi ya kujibu na hakimu huyo alikwenda mbali zaidi na kusema upande wa jamhuri uache kufungua kesi kwa kukurupuka na kwamba mwisho wa siku mahakama inapowaachilia huru washtakiwa, matokeo yake mahakama inakuja kubebeshwa lawama.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...