Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas
…………………………………………….
(Na. Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Dar es Salaam
Jeshi
la Polisi mkoani Arusha limekanusha taarifa ya kuachiwa huru kwa
mtuhumiwa wa ujangili Bw. Frank William Silangei maarufu kwa jina la
“Ojung’s Mwarusha” mkazi wa Ngaramtoni Kibaoni iliyotolewa na gazeti
moja la kila wiki.
Akizungumza
katika mahojiano kwa njia ya simu na Idara ya habari MAELEZO leo jijini
Dar es Salaam, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amesema
kuwa mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 32 hivi sasa yuko mahabusu na
taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea kufanyika.
Kamanda
Sabas ameeleza kuwa mtuhumiwa Silangei hajaachiwa huru kama
ilivyoripotiwa na gazeti hilo linalotoka kila Alhamis katika ukurasa
wake wa kwanza na wa pili na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo
liko makini katika kutekeleza majukumu yake.
“Si
kweli hajaachiwa, natamani ungekuwa hapa Arusha nikakupeleka mahabusu
ukamuona mtuhumiwa kwa macho yako”, amesema Kamanda Sabas.
Kamanda
Liberatus Sabas amesema Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea na
jitihada zake za kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya ujangili
vinatokomezwa na yeyote atakayehusika na vitendo hivyo atachukuliwa
hatua za kisheria.