Kufuatia harakati za kudai haki za wasanii wa Tanzania katika miito ya simu zilizoanzishwa na Mh: Lugemalila Mutahaba mdau wa muziki Tanzania na kusimamiwa na MB wa KIgoma Kaskazini Zitto Zuberi
Kabwe, matumaini yanaanza kuonekana baada ya serikali kupitia
Waziri DR; Abdallah KIgoda kutoa maagizo yake juu ya hilo
Waziri
wa Viwanda na Biashara DR ABDALLAH KIGODA ameagiza mabadiliko ya kanuni katika Sheria ya
Hakimiliki ili kuhakikisha kwamba Wasanii wa muziki hapa nchini wanapata
mapato stahiki katika biashara ya #RBT . Mirahaba katika biashara ya
miito ya simu na matangazo ya televisheni na radio Ni mapato muhimu
sana Kwa wasanii. Angalau sasa tunaona Mwanga. Tutaendelea kuishinikiza
serikali kulinda wasanii na Hakimiliki zao
HII NDIYO BARUA YA MH. ZITTO ALIYOANDIKA KWENDA KWA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA DR. ABDALLAH KIGODA
Kwenda kwa: DR ABDALLAH KIGODA, Waziri wa Viwanda na Biashara
Kuhusu: BIASHARA YA MIITO YA SIMU (RINGBACK TONES)
Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kuhusu biashara ya mauzo ya nyimbo
kama miito kwenye simu. Malalamiko haya yalianzia kwa wasanii wenyewe na
baadaye mimi binafsi niliwasilisha hoja zao Bungeni mwaka 2012. Hata
hivyo, hadi sasa malalamiko haya bado hayajapatiwa ufumbuzi na hivyo
wasanii kuendelea kunyonywa. Tatizo kubwa katika biashara hii ni USIRI
na UNYONYAJI kwa wasanii wa Tanzania. Suala la USIRI lipo Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Suala la Unyonyaji lipo Wizara ya
Viwanda na Biashara.
USIRI
Biashara hii ya “Ring Back Tones” (RBT) hufanywa na Kampuni za simu
(Network providers) kwa kununua maudhui kutoka wachuuzi (Content
Providers) ambao nao huingia mikataba na Wasanii (Content Creators).
Hakuna sheria yoyote au Kanuni hapa nchini inayoongoza biashara hii na
hivyo “Network providers” na “Content Providers” kuwa watu pekee wenye
taarifa zote za biashara hii. Kampuni za simu hujumuisha mapato ya
biashara hii na mapato yake mengine (Not Ringfenced), hawatoi taarifa za
manunuzi ya nyimbo (au ‘content’ nyingine yeyote) kwa wadau na hasa
wasanii. Wachuuzi (Content Providers) nao hawatoi taarifa za mauzo kwa
wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii kuwasainisha mikataba
inayowanyonya. Matokeo yake ni kwamba msanii hupata kiasi cha asilimia
mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake. Hivi sasa biashara hii
inathamani (turnover) ya takribani shilingi 44 bilioni kwa mwaka.
Suluhisho:
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano iandike kanuni (regulations)
zitakazolazimisha makampuni ya simu kuweka wazi mapato yatokanayo na
biashara ya RBT (Miito ya simu) kila baada ya miezi 4 (disclosure
rules). Kanuni hizi zielekeze makampuni kutoa taarifa za mauzo kwa kila
kazi (nyimbo/vichekesho etc.)
UNYONYAJI
Kutokana na usiri ulioelezwa hapo juu, wasanii wamekuwa wakinyonywa
kimapato. Kwa mfano Msanii hulipwa mapato yatokanayo na ununuzi wa awali
wa kazi yake (wimbo) katika mwezi (downloads).
Lakini mapato yatokanayo na “subscriptions” ambapo mlaji hukatwa
shilingi 30 kila siku msanii hapati chochote. Hivyo katika mapato ya sh.
1,300 kila mwezi kwa kila mteja kwa kila wimbo, msanii hupata mgawo
wake kutoka shilingi 400 tu za ‘downloads’ na ndio maana wasanii wote
nchini hupata 2.5% ya shilingi 44 bilioni zinazokusanywa na Kampuni za
Simu.
Nchini Marekani biashara ya miito ya simu (RBT) imetafsiriwa kama
maonyesho (Public Performances) na hivyo “copyright Association” ya
Marekani imeweka kiwango cha chini cha mrahaba (royalty) ambacho msanii
hulipwa. Marekani msanii hulipwa asilimia 10 ya patoghafi linalozalishwa
na kazi yake kama muito wa simu.
SULUHISHO
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iandike kanuni kwamba
mauzo ya kazi za wasanii kama miito ya simu inachukuliwa kama
‘performance’ na kwamba Kampuni za simu zitalipa sio chini ya asilimia
12 (12%) ya mapato ghafi, ambapo asimilia 10% itakwenda kwa msanii na
asilimia 2% COSOTA kwa ajili ya usimamizi na Ulinzi wa kazi za Wasanii.
HITIMISHO
Kanuni za Uwazi (disclosure rules) katika biashara hii ya ‘Ring Back
Tones’ na mgawo wa haki wa mapato (fair and just revenue share) ndio
suluhisho endelevu na litakaloleta tija kwa wasanii wa Tanzania na hata
Serikali kukusanya mapato stahili. Kanuni (Regulations) zinazopendekezwa
zianze kutumika kuanzia tarehe 1/7/2013
Kabwe Z. Zitto, Mb Kigoma Kaskazini Dodoma, 13 Mei 2013.