Serikali imesema inajipanga upya kurudi Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu
ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Abdallah
Zombe, na wenzake wanane, waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuhusika
na mauaji ya raia wanne.
Hatua hiyo, ambayo imetangazwa na serikali jana, inachukuliwa zikiwa
zimepita siku nane baada ya Mahakama ya Rufaa kushindwa kuendelea
kusikiliza rufaa yake (serikali) ya kupinga hukumu hiyo.
Mahakama hiyo ilishindwa kuendelea na suala hilo baada ya kujiridhisha
kuwa hakukuwa na rufaa, ambayo ingesikilizwa na kutolewa uamuzi,
kutokana na taarifa ya kusudio la kuikata, kubainika kuwa ina dosari.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, aliliambia NIPASHE jana
kuwa wakati wowote kuanzia sasa watarudi katika mahakama hiyo kuiomba
kuisikiliza rufaa hiyo baada ya kuishughulikia.
“Amri ya Mahakama (ya Rufaa) iko wazi. Imeona kuna dosari. Sasa
tunachukua hatua. Tunaandika nyaraka zetu kurudi mahakamani (Mahakama ya
Rufaa),” alisema Feleshi.
Alipoulizwa lini watarudi mahakamani hapo, awali alijibu: “Hatuwezi
kusema hilo kwenye magazeti.” Lakini baadaye, alisema: “Any time” (muda
wowote).
Alisema haiwezekani kukaa kimya kuhusiana na rufaa hiyo.
Feleshi alisema iwapo katiba ingekuwa inafuatwa vizuri kuhusiana na
mashauri makubwa, makosa madogo madogo kama hayo yasingekuwa ni sababu
ya kukwamisha rufaa hiyo kufanyiwa kazi.
“Kulikuwa na makosa madogo madogo, badala ya kuandikwa Jaji Salum
Massati wa Mahakama ya Rufaa ambaye wakati huo alikuwa Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, iliandikwa Jaji Salum Massati wa
Mahakama ya Rufaa,” alisema Feleshi na kuongeza:
“Haya ni makosa madogo madogo. Lakini kama tungekuwa tunaifuatilia
Katiba kuhusu masuala yahusuyo mashauri makubwa kama hayo, yasingeweza
kukwamisha rufani hiyo. Watu watatu waliuawa, wajane wameachwa, yatima.
Hatuwezi kukaa kimya, tutashughulikia rufani hiyo.”
Alisema Jaji Massati wakati akitarajia kutoa hukumu alipewa taarifa ya
kuhamishiwa katika Mahakama ya Rufaa, na kwamba alitoa hukumu hiyo
akiwa tayari amehamishiwa katika mahakama hiyo.
Hata hivyo, hakutaja muda maalum wa kuipeleka rufaa hiyo tena mahakamani hapo baada ya kuifanyia marekebisho.
“Siwezi kukuambia ni lini. Lakini naona neno zuri la kukuambia ni kwamba
bado tunalishughulikia kwa ajili ya kupeleka mahakamani,” alisema
Feleshi.
Uamuzi wa kutupilia mbali rufaa hiyo, ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa.
Kasoro ambayo mahakama hiyo iliibaini kuwamo kwenye taarifa hiyo, ni ya
kumtaja Jaji Salum Massati, aliyetoa hukumu iliyowaachia huru Zombe na
wenzake, kuwa wakati alipotoa hukumu hiyo, alikuwa ni Jaji wa Mahakama
ya Rufaa, wakati usahihi alikuwa ni Jaji Kiongozi.
Awali, baada ya Mahakama ya Rufaa kubaini kasoro hiyo, upande wa Jamhuri uliomba uruhusiwe kuifanyia marekebisho taarifa yao.
Lakini katika uamuzi wake wa Mei 8, mwaka huu, mahakama hiyo ilisema
haiwezekani kufanya marekebisho katika kitu, ambacho hakipo.
Uamuzi huo ulisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elizabeth Mkwizu,
na kuunga mkono pingamizi lililowekwa awali na mawakili wa wajibu
rufani (Zombe na wenzake).
Mkwizu alisema DPP, ambaye ndiye alikuwa mwombaji rufaa, alipaswa kutoa
taarifa ya kusudio la kukata rufaa iliyo sahihi kwa kuwa ndiyo
inayotengeneza rufaa.
Kutokana na hali hiyo, alisema hukumu ya Jaji Massati ilikuwa ya haki na
halali na kwamba, ilitolewa na jaji sahihi kwani wakati ule alikuwa
bado hajaripoti Mahakama ya Rufaa.
Hata hivyo, alisema upande wa Jamhuri una haki na nafasi ya kufungua
upya jalada lingine kuhusu ‘rufaa’ yao kwa kuzingatia sheria ya ukomo wa
muda.
Jopo la majaji wa ‘rufaa’ hiyo namba 254/2009 walikuwa ni Edward Rutakangwa, Mbarouk Mbarouk na Betheka Mila.
Mwombaji rufaa (DPP) aliwakilishwa na mawakili; Vitalis Timon, Prudence
Rweyongeza, Mgaya Mtaki, Alexander Mzikila na Edwin Kakoraki.
Wajibu rufaa waliwakilishwa na mawakili; Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Denis Msafiri.
Rufaa hiyo ilikatwa na DPP, Oktoba 7, mwaka 2009, baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo.
Alidai upande wa Jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi uliojitosheleza,
ambao ungeweza kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana
hatia.
Awali, rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa mwishoni mwa mwezi uliopita,
lakini ilishindikana baada ya mahakama hiyo kubaini dosari hiyo.
Hukumu ya kuwaachia huru Zombe na wenzake, ilitolewa na Jaji Massati,
Agosti 17, mwaka 2009, kabla ya kuhamishwa Mahakama ya Rufaa.
Katika hukumu hiyo, Jaji Massati alisema amefikia uamuzi huo baada ya
upande wa Jamhuri kushindwa kupeleka ushahidi wa kutosha mahakamani
kuthibitisha mashtaka dhidi ya Zombe na wenzake kwamba, walihusika na
mauaji.
Mbali na Zombe, wengine waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka hayo,
walikuwa ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D
1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth
Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi.
Wote walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 walihusika katika mauaji ya
wafanyabiashara watatu wa madini wa Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro;
ambao ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lunkombe pamoja
na dereva wa teksi, Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai ya
kwamba walikuwa ni majambazi.
HABARI NA MUHIBU SAID
CHANZO: NIPASHE