Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Sunday, May 19, 2013

Changamoto ya Upungufu wa Madawati Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yapatiwa Ufumbuzi.

IMG_9095
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kuhusiana na mfuko wa Ilala “Mayors Ball” kwa ajili ya kuchangisha fedha za kununulia madawati kwa shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya Manispaa ya Ilala. Katikati ni Afisa Elimu Msaidizi upande wa Takwim Manispaa ya Ilala Wema Kajigile na kushoto ni Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala Bi. Tabu Shaibu.
-Kauli mbiu ni Kalisha mmoja, boresha Elimu.
Msimu wa mfuko wa uchangishaji wa Mayors ball una nia ya kuwa alama ya Meya wa Ilala kwa kuwaleta pamoja viongozi wa idara mbalimbali Tanzania katika tukio moja kwa dhumuni la kusaidia na kuhudumia jamii.
Madhumuni ya waanzilishi wa mfuko wa Ilala Mayors Ball ni kujikita katika uchangishaji wa fedha ambazo zitatumika kuwasaidia wakazi wa Ilala moja kwa moja. Michango ambayo itakusanywa katika kila msimu wa mfuko wa Mayor’s ball itakabidhiwa kwa vituo ambavyo vitakuwa vimependekezwa katika kila msimu kupitia maombi maalumu.
“Kwenye kila taifa llililoendelea kuna watu walioelimika. Ili kutengeneza mazingira mazuri ya utoaji elimu kwa watoto wetu na taifa lijalo, vitu mbalimbali ni muhimu kimoja wapo ikiwa ni dawati, hivyo basi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali na jamii nzima kwa ujumla katika msimu wa Mayor’s ball mwaka huu tutahakikisha kwamba wanafunzi wa manispaa ya Ilala wanakaa kwenye madawati”. Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Jerry Silaa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala wakati akizindua kampeni hiyo katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro tarehe 17 Mei 2013.
Mwaka huu mradi wa mayor’s ball ambao imepewa jina la “Dawati ni Elimu” inakuja na kauli mbiu isemayo “Kalisha mmoja, boresha Elimu.”
Mayor’s ball mwaka huu imekusudia kuchangia shilingi Bilioni 4.98 kwa ajili ya madawati katika shule za msingi na sekondari 30,487 za manispaa ya Ilala ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2013/14.
“Kwa ajili ya kujenga mfuko wa Mayor’s ball kutakuwa na matukio mbalimbali kama vile mechi za mpira wa miguu, matamasha ya muziki, maonesho ya mavazi na matembezi ambayo yatajumuisha watu wa kaliba mbalimbali katika jamii kama moja ya juhudi za kuunga mkono mfuko wa uchangishaji.” Alisema Mustafa Hassanali mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya 361 Degrees ambayo imebuni na kusimamia mikakati na mchakato mzima wa mradi huo kwa ajili ya ofisi ya Meya ikiwa ni sehemu ya mpango wa mahusiano ya kikazi baina ya pande hizo mbili.
Mpaka sasa kuna madawati 55,755 ambayo yanatumika kati ya madawati 86,242 ambayo yanahitajika. Hivyo basi kuna upungufu wa madawati asilimia 35.35, ili kuweza kukabiliana na upungufu huu inatakiwa kuundwa kampeni za kijamii ambapo basi kila mmoja ataweza kuchangia kiasi chake ili kuweza kuzipatia madawati shule katika manispaa ya Ilala.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...