Mh. Zitto Kabwe.
PENDEKEZO BINAFSI LA MBUNGE KUHUSU KUZUIA UNYONYAJI DHIDI YA WASANII WA TANZANIA KATIKA BIASHARA YA MIITO (RING BACK TONES)
Kwenda kwa: DR ABDALLAH KIGODA, Waziri wa Viwanda na Biashara
Kuhusu: BIASHARA YA MIITO YA SIMU (RINGBACK TONES)
Kumekuwa
na malalamiko makubwa sana kuhusu biashara ya mauzo ya nyimbo kama
miito kwenye simu. Malalamiko haya yalianzia kwa wasanii wenyewe na
baadaye mimi binafsi niliwasilisha hoja zao Bungeni mwaka 2012. Hata
hivyo, hadi sasa malalamiko haya bado hayajapatiwa ufumbuzi na hivyo
wasanii kuendelea kunyonywa. Tatizo kubwa katika biashara hii ni USIRI
na UNYONYAJI kwa wasanii wa Tanzania. Suala la USIRI lipo Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Suala la Unyonyaji lipo Wizara ya
Viwanda na Biashara.
USIRI
Biashara
hii ya “Ring Back Tones” (RBT) hufanywa na Kampuni za simu (Network
providers) kwa kununua maudhui kutoka wachuuzi (Content Providers)
ambao nao huingia mikataba na Wasanii (Content Creators).
Hakuna
sheria yoyote au Kanuni hapa nchini inayoongoza biashara hii na hivyo
“Network providers” na “Content Providers” kuwa watu pekee wenye
taarifa zote za biashara hii. Kampuni za simu hujumuisha mapato ya
biashara hii na mapato yake mengine (Not Ringfenced), hawatoi taarifa za
manunuzi ya nyimbo (au ‘content’ nyingine yeyote) kwa wadau na hasa
wasanii. Wachuuzi (Content Providers) nao hawatoi taarifa za mauzo
kwa wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii kuwasainisha mikataba
inayowanyonya. Matokeo yake ni kwamba msanii hupata kiasi cha asilimia
mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake. Hivi sasa biashara hii
inathamani (turnover) ya takribani shilingi 44 bilioni kwa mwaka.
Suluhisho:
Serikali
kupitia Wizara ya Mawasiliano iandike kanuni (regulations)
zitakazolazimisha makampuni ya simu kuweka wazi mapato yatokanayo na
biashara ya RBT (Miito ya simu) kila baada ya miezi 4 (disclosure
rules). Kanuni hizi zielekeze makampuni kutoa taarifa za mauzo kwa kila
kazi (nyimbo/vichekesho etc.)
UNYONYAJI
Kutokana
na usiri ulioelezwa hapo juu, wasanii wamekuwa wakinyonywa kimapato.
Kwa mfano Msanii hulipwa mapato yatokanayo na ununuzi wa awali wa kazi
yake (wimbo) katika mwezi (downloads).
Lakini
mapato yatokanayo na “subscriptions” ambapo mlaji hukatwa shilingi 30
kila siku msanii hapati chochote. Hivyo katika mapato ya sh. 1,300 kila
mwezi kwa kila mteja kwa kila wimbo, msanii hupata mgawo wake kutoka
shilingi 400 tu za ‘downloads’ na ndio maana wasanii wote nchini hupata
2.5% ya shilingi 44 bilioni zinazokusanywa na Kampuni za Simu.
Nchini
Marekani biashara ya miito ya simu (RBT) imetafsiriwa kama maonyesho
(Public Performances) na hivyo “copyright Association” ya Marekani
imeweka kiwango cha chini cha mrahaba (royalty) ambacho msanii hulipwa.
Marekani msanii hulipwa asilimia 10 ya patoghafi linalozalishwa na kazi
yake kama muito wa simu.
SULUHISHO
Serikali
kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iandike kanuni kwamba mauzo ya
kazi za wasanii kama miito ya simu inachukuliwa kama ‘performance’ na
kwamba Kampuni za simu zitalipa sio chini ya asilimia 12 (12%) ya
mapato ghafi, ambapo asimilia 10% itakwenda kwa msanii na asilimia 2%
COSOTA kwa ajili ya usimamizi na Ulinzi wa kazi za Wasanii.
HITIMISHO
Kanuni
za Uwazi (disclosure rules) katika biashara hii ya ‘Ring Back Tones’ na
mgawo wa haki wa mapato (fair and just revenue share) ndio suluhisho
endelevu na litakaloleta tija kwa wasanii wa Tanzania na hata Serikali
kukusanya mapato stahili. Kanuni (Regulations) zinazopendekezwa zianze
kutumika kuanzia tarehe 1/7/2013
Kabwe Z. Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini
Dodoma, 13 Mei 2013.