BABA WA MTUHUMIWA WA UGAIDI ULIOTOKEA KANISANI JIJINI ARUSHA ANENA MAZITO.....SOMA HAPA.
Joseph Lomayani (18),dereva mwingine wa pikipiki anayedaiwa kuhusika na kurusha bomu kanisani, jijini Arusha.
Joseph Lomayani (18), ni dereva mwingine wa pikipiki kukamatwa kwa
tuhuma za kuwarushia bomu waumini waliokusanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti jijini hapa jumapili ya Mei 5, mwaka huu.
Wa kwanza kukamatwa alikuwa Victor Ambroce Kalisti (20). Wote kwa
pamoja walikuwa na kituo (kijiwe) cha kufanyia biashara zao za bodaboda
eneo la kwa Mrombo nje kidogo ya jiji la Arusha, barabara iendayo Simanjiro, mkoani Manyara.
Joseph ni mtoto wa watatu kuzaliwa kati ya watoto saba wa Lomayani
Sautie Metivani (47) na kati yao wasichana ni watatu na wavulana ni
wanne. Mkewe ametangulia siku nyingi mbele ya haki.
Babake
anamwelezea Joseph kuwa alimaliza darasa la saba Shule ya Msingi Terrat
mwaka 2010, lakini kutokana na umri aliokuwa nao kuwa mkubwa mwaka
uliofuata alipata nafasi ya kuanza masomo ya sekondari katika shule ya
watu wazima kupitia mpango wa Memkwa.
Hata hivyo, anasema
kutokana na mila za kwao Wamasai, alimpeleka mtoto wake kutahiri hali
ambayo ilimfanya ashindwe kuendelea na masomo yake kwa mwaka huo
kutokana na kutumia muda mwingi kwa shughuli za utamaduni wa kutahiri na
pia shule kuwa mbali na nyumbani kwao.
Hata hivyo, anasema alimtafutia shule nyingine ya aina kama hiyo ambayo ipo eneo la Olasiti. Alipoanza hiyo shule, Lomayani anasema, mtoto wake aliwakuta wenzake wapo mbali kimasomo. Akashindwe kumudu.
“Alipoanza hiyo shule aliwakuta wenzie wapo mbali, akaniambia, baba,
kwenda kusoma tena pale kichwa yangu haikamati, hivyo, sitaweza
kuendelea tena na hiyo shule, nitakuwa kama vile ninaswagwa tu,”
ananukuu maelezo ya mtoto wake.
“Baada ya hapo, nilimtafutia
kazi ya ufundi wa karakana ya magari. Ilikuwa mwaka huo huo wa 2012 na
gereji hiyo ipo kule kwa Mrombo inayomilikiwa na Olii,” anasema.
Lakini anasema baadaye mwanaye aliugua na kushindwa kuendelea na
mafunzo ya kazi hiyo, hivyo akawa yupo tu akiendelea na shughuli za hapa
na pale nyumbani kwake.
Kuendelea kukaa nyumbani bure
kulimchosha, na kama wiki moja kabla ya mlipuko wa bomu kanisani,
alikuwa amepata pikipiki ya Lomyaki Sindiyo, hivyo akawa anaiendesha kwa
makubaliano ya kumlipa fedha kila wiki.
“Alianza kuendesha
pikipiki hiyo kama wiki moja iliyopita, na wakati yupo pale kijiweni
siku ya Jumapili, Victor Ambroce alimwachia simu yake amkamchajie na
yeye Victor alikuwa amepata mteja na sijui huyo mteja alikuwa anampeleka
wapi,” anadai.
Lomayani anadai kuwa majira ya saa tano hivi
asubuhi, alimpigia mwanaye simu akimuuliza yupo wapi naye akamjibu kuwa
yupo kwa Mrombo.
“Nilimwambia njoo nyumbani uchukue hela
ukatulee mboga na baada ya kuileta (Joseph) akaendelea na shughuli
zake,” anadai na kuongeza, mlipuko wa bomu kanisani hapo aliusikia
majira ya saa mchana kupitia redio moja ya kijamii ya mkoani hapa.
KUKAMATWA KWA JOSEPH:
Anasema ilikuwa saa 12 asubuhi ya Jumatatu iliyopita, askari polisi
walifika pale nyumbani kwake eneo la Mrombo CCM, na kumuuliza:
“Tunamhitaji Joseph kwani ana simu ya Victor aliyoichukua.”
“Wakaenda kumwamsha Joseph anakolala na kumuuliza simu ya Victor ipo
wapi naye akawawaambia ameiacha dukani kwa George huko huko kwa Mrombo
CCM anasema na kuongeza:
“Polisi walienda naye kuichukua ile
simu na wakamchukua na George pia na kuwapeleka kituoni na baada ya hapo
kulingana na mimi ninavyomjua mtoto wangu hanaga tabia mbaya kabisa na
wanaweza kuchunguza hilo.”
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, George ni mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.
“Mimi nasikitika sana mtoto wangu kusingiziwa kuwa ni mmoja wa watu
wanaohusishwa kurusha bomu kanisani. Maaskari hapo hawakuwa hawajatenda
vyema.
“Mtoto wangu anaenda kutoswa bila sababu, nikiwa mzazi wake nakiri kabisa huyo mtoto hajafanya suala hilo,” anasema.
Katika tukio hilo la bomu watu watatu walifariki dunia huku wengine zaidi ya 67 wakijeruhiwa, baadhi yao vibaya.
Wengine wamehamishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) kwa uchunguzi na matibabu zaidi