Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Dar
es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba ametangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa mikutano ya Mabaraza ya
Katiba ya wilaya, huku akiwaonya watu wa kada mbalimbali vikiwemo vyama
vya siasa kutokuingilia mikutano hiyo.
Vilevile
Jaji Warioba alieleza sababu za Tume hiyo kupendekeza Serikali tatu,
huku akisisitiza kuwa suala hilo lilikuwepo tangu siku nyingi na Tume
iliamua kupendekeza Serikali tatu kwa kuwa ndiyo ilikuwa njia pekee ya
kuulinda muungano.
Kauli
hiyo inaonekana kama kukijibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
kimependekeza kuwepo kwa Serikali mbili, ikiwa ni siku chache baada ya
kutolewa kwa Rasimu ya Katiba.
Mikutano
hiyo inafanyika baada ya Juni 3 mwaka huu, Tume hiyo kutoa rasimu ya
Katiba na kusambaza katika vijiji, mitaa na shehia kwa ajili ya
kujadiliwa na wananchi, ambao nao watachangia mawazo yao kwa wawakilishi
wao waliowachagua kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, inaeleza kuwa mikutano hiyo itaanza
Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu na kutakuwa na jumla ya Mabaraza 177,
Tanzania Bara 164 na Zanzibar 13.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Tayari
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mikakati kabambe ya kuhakikisha
kuwa mapendekezo yake yanapitishwa huku kikitumia wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba wakiwemo wa ngazi ya mtaa, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye akiwaeleza wajumbe wa mabaraza ya Katiba jijini
Dar es Salaam juzi azma ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.
Wakati
CCM wakieleza hayo, Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) inakutana leo na kesho katika kikao cha dharura jijini Dar es
Salaam ili kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anayemaliza muda wake,
Profesa Issa Shivji, Juni 21 mwaka huu alisema kama Rasimu ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano ikikubaliwa bila mabadiliko makubwa
itasababisha kuvunjika kwa Muungano.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema hairuhusiwi kwa
makundi, vyama vya siasa au mtu yeyote kuingia katika mabaraza hayo kwa
lengo la kushawishi kukubaliwa na maoni ya aina fulani. Alitoa ufafanuzi
huo baada ya kuulizwa swali na gazeti hili, juu ya taarifa zilizopo
kwamba baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeandaa rasimu zao kwa lengo
la kuwashawishi wajumbe wa mabaraza kupitisha maoni yao.
“Mikutano
na Mabaraza ya Katiba siyo ya kupiga kura bali ni kujadili na kutoa
hoja ambazo zitakuwa na msingi kwa masilahi ya taifa na siyo kutetea
masilahi ya kundi au watu fulani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza;
“Hilo
la vyama kuandaa rasimu zao kwa lengo la kuingilia utaratibu huu
sijalisikia, ila kikubwa ni kwamba si ruhusa kuingilia mchakato huu kwa
sababu utafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” alisema Warioba na
kusisitiza; “Wananchi watoe maoni ambayo yatasaidia kuiboresha rasimu
iliyotolewa kwa kuweka mbele masilahi ya taifa na kuepuka ubinafsi wa
mtu mmojammoja au makundi ya aina yeyote.”
Alisema
Tume yake itapokea maoni na mapendekezo yote ambayo yatakuwa na lengo
la kuiboresha rasimu ambayo itaweka umoja wa kitaifa na siyo kuwagawa
Watanzania.
“Tunazidi
kuwaomba wasiishie kutoa maoni na hofu zao, bali wasaidie tume kutoa
mapendekezo ambayo yataisaidia tume katika kazi yake ya kuwapatia
Watanzania katiba iliyokuwa bora,” alisema.
Akizungumzia
sababu za kupendekeza Serikali tatu, Warioba alisema kama
wangependekeza Serikali ya mkataba ilikuwa lazima kuvunjwa kwa muungano
na kuwepo kwa Serikali mbili ambazo baadaye zingekaa na kuamua
kushirikiana ama laa, jambo ambalo lingekuwa gumu.
“Wapo
waliotaka Serikali mbili, lakini katika hilo wapo waliosema kuwa
Zanzibar wana wimbo wao wa taifa na bendera, pia wamejiunga na OIC na
hata Katiba yao inasema kuwa Zanzibar ni nchi, Watanganyika nao
wangeanza kuhoji Tanganyika iko wapi,” alisema.
Alisema
ndiyo maana walipendekeza Serikali tatu na kwamba kama wangeamua
kuvunja muungano operesheni za sheria tulizonazo zingewatenganisha
wananchi, kama soko la pamoja, sheria ya ardhi, mwingiliano wa pande
mbili, biashara, matibabu na shule.
Alisema
Serikali tatu ndiyo suluhisho la kudumisha muungano kuliko Serikali
moja au mbili, na kwamba katika kura ya maoni jambo la uwepo wa Serikali
tatu linategemea uamuzi wa viongozi.
Akizungumzia
idadi ya wajumbe wa mabaraza hayo alisema Tanzania Bara kutakuwa na
wajumbe 18,174 na Zanzibar 1159 na kwamba tume itatumia siku 54
kuendesha Mabaraza ya Katiba nchi nzima.
“Ili
kuweza kufika sehemu zote za nchi, tume imejigawa katika makundi 14 na
kila kundi litaendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya wilaya katika
Mamlaka za Serikali za mitaa 12 au 13 na mikutano itafanyika kwa siku
tatu,” alisema.
Alisema
mikutano ya kwanza itafanyika katika mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara,
Kigoma, Tabora, Lindi, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mkoa wa Kusini
Unguja, Mbeya, Rukwa, Mtwara na Njombe.
CCM
Tangu
rasimu hiyo ilipotolewa mapema Juni mwaka huu, chama hicho kilionyesha
kutokuridhishwa na rasimu hiyo na kuahidi kuipeleka kwa wanachama wake.
Katika
kuonyesha kutokuridhshwa huko, Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye
aliwaeleza wajumbe wa Mabaraza ya Katiba jijini Dar es Salaam juzi azma
ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.
Nape
ambaye aliitumia siku nzima ya Alhamisi kuzungumza na wajumbe hao wa
mabaraza, alisema wameandaa rasimu yao ambayo imeandikwa vitu
wanavyohitaji na wanachama wote wanapaswa kuvisimamia.
Alisema
ili kurekebisha kasoro hizo CCM kimeandaa rasimu ambayo imetengenezwa
katika mazingira ya kisiasa na kitaalamu ambapo haitokuwa mzigo kwa
chama hicho.
Alisema katika vitu muhimu ambavyo wanapaswa wajumbe wa chama hicho kuvipigania ni pamoja na suala la Serikali tatu.
Nape
alisema kipengele cha Serikali tatu ambacho kinaitwa Serikali ya
shirikisho kinapaswa kupiganiwa kifutwe kutokana na nchi kutokufikia
hatua ya kuwa shirikisho.
Alisema kitengo cha kuweka Serikali tatu kinaweza kuongeza urasimu pamoja na kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali hizo.
Alisema
harakati za kutangaza rasimu ya CCM zinafanyika nchi nzima kwa kutumia
makada wa chama hicho katika baadhi ya mikoa ambapo katika Visiwa vya
Zanzibar zoezi hilo lilifanyika Julai tatu.
Alisema
rasimu hiyo inatarajiwa kwenda kupelekwa katika kikao cha Wajumbe wa
Halmshauri Kuu (NEC) itajadiliwa na wajumbe wote ili kuweza kupata
mawazo mengine ya wajumbe.
Chadema nao wakutana
Taarifa
iliyotolewa na chama hicho imetaja mambo mengine yatakayojadiliwa kuwa
ni pamoja na taarifa ya hali ya siasa nchini, taarifa juu ya mfumo wa
uendeshaji wa chama kwa kanda (uzinduzi) na taarifa juu ya uchaguzi
mdogo wa madiwani katika kata 26, uliofanyika Juni 16, 2013.
Kauli ya Shivji
Kauli
hiyo ya Shivji aliitoa katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, wakati akitoa mhadhara wa kuaga wadhifa wake wa Mwenyekiti wa
Kigoda hicho kwa Wanakigoda wenzake na jumuiya ya chuo hicho.
Profesa
Shivji aliainisha upungufu uliomo katika rasimu hiyo iliyoandaliwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambapo alisema yanaweza kusababisha
kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja Muungano.
Alibainisha
rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu ukuu wa Katiba ya
Muungano juu ya katiba nyingine za washirika wa Muungano, hali
itakayosababisha migongano na kutokuelewana kati ya mamlaka za washirika
wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema
kuwa Ibara ya nane ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa ina kasoro kubwa kwani imeeleza kuwa
ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano
tu na si vinginevyo.
MWANANCHI