Wafuasi wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani
Mohammed Morsi wamefanya maandamano makubwa mjini Cairo, huku waumini wa
dini ya Kiislamu wakiadhimsiha Ijumaa ya kwanza tangu kuanza kwa mwezi
mtukufu wa Ramadan.
Wafuasi wa kiongozi huyo wa vugu vugu la Muslim
Brotherhood walijikusanya Mashariki mwa mji huo, kushinikiza utawala wa
kijeshi kumrejesha madarakani kiongozi wao.
Wapinzani
wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa
madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.
Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema
vuguvugu la Muslim Brotherhood huenda liliwatenga raia wengi wakati wa
utawala wa Morsi, lakini bado raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi
kuingilia masuala ya siasa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo. Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri. Marekani inatarajiwa kupeleka ndege nne za kivita aina ya F-16 nchini Misri, lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini. Serikali ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia mapinduzi. Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa madarakani.