Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Tuesday, July 9, 2013

SUMATRA yafungia mabasi 3 kwa kutelekeza abiria

 

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeyafungia kwa siku 30 mabasi matatu ya kampuni ya Falcon na Mwasha Express, kwa kutelekeza abiria ili iwe fundisho kwa wengine.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo anayeshughulika na Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Leo Ngowi, alisema jana kuwa mabasi hayo, Falcon Coach lenye namba za usajili T810AYJ linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Bukoba na mawili ya kampuni ya Mwasha Express yenye namba T882ARE na T912AIE, yasafirishayo abiria kati ya Mbeya na Sumbawanga yalianza kutekeleza adhabu hiyo Julai 02.

Ngowi alisema, hatua hizo zilitokana na ushirikiano mzuri uliotolewa na abiria wa mabasi hayo kwa Sumatra, kupitia njia mbalimbali, ikiwemo mawasiliano ya simu, ambapo wahusika walizifanyia kazi na kubaini ukweli kwamba mabasi hayo yamekuwa yakitelekeza abiria njiani kila mara yanapoharibika na kuwafanya wateseke.

”Pamoja na kuzuia mabasi hayo yasifanye safari, tuliwaandikia barua wamiliki wa kampuni za mabasi hayo, ili
warejeshe leseni na ratiba za safari za mabasi hayo ifikapo Julai 6 na walifanya hivyo,” alisema.

Ngowi alisema basi la Falcon liliwatelekeza abiria katika eneo la Gairo, Dodoma wakati likienda Bukoba kutoka Dar es Salaam Juni 28, mwaka huu na licha ya wahusika kuombwa watoe usafiri mwingine wa kuwafikisha wasafiri hao mahali waendako, walifanya ujanja na kuwaacha mahali hapo bila msaada wowote.

Aliongeza kuwa gari hilo liliharibika saa 6:00 mchana na abiria zaidi ya 50 waliokuwemo katika gari hilo, waliendelea kuwepo kwenye eneo la tukio kwa muda wote bila msaada, hadi alipofika Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Khalfan Karamagi na kusikiliza malalamiko yao na kuwasiliana na Mamlaka.

‘’Abiria wa Falcon waliteseka kwa saa zaidi ya 18 huku wakiwa wamelipa nauli. Kutokana na hilo, tumelifungia basi hilo na kuamrisha mengine yote ya kampuni hiyo yanayotumia njia hiyo yasiendelee na safari hadi yatakapofanyiwa matengenezo kwa sababu ni mabovu.

Tunafuatilia hilo kwa karibu na tutayakagua kujiridhisha kabla ya kuyaacha ‘yaumize’ abiria,” alisema Ngowi.

Kuhusu mabasi ya Mwasha Express, Ngowi alisema, licha ya kuwa na tabia ya kutelekeza abiria yanapoharibika, yamekuwa yakikatisha tiketi na kutowachukua abiria kutoka vituoni, jambo lililo kinyume cha sheria na taratibu za usafirishaji wa abiria.

“Juni 12, tulipata malalamiko kutoka kwa abiria waliokuwa wasafiri kwa mabasi hayo kutoka Mbeya kwenda Sumbawanga kwamba walitelekezwa kituoni bila kupewa taarifa au msaada wowote na wahusika wa mabasi hayo. Tulifuatilia na kubaini kuwa walikaa kituoni hapo bila mafanikio kwa muda mrefu huku wenye mabasi wakiwa hawana la kufanya kutokana na mabasi yao kuwa mabovu”.

“…Huu ni ukiukwaji wa sheria namba 21 na 22 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji kwa magari ya abiria ya mwaka 2007 na kanuni namba 11 (1)(b) ya viwango vya ubora na usalama ya mwaka 2008. Kwa sababu hiyo, nao tumewaamuru wasifanye biashara kwa basi nililolitaja hadi siku 30 ziishe na magari yao mengine mabovu nayo yasifanye safari hadi yatengenezwe”.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...