Serikali
imetangaza viwango vipya vya chini vya mishahara kisekta ambavyo
vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine ambavyo ni kuanzia
Sh40,000 hadi Sh400,000 kwa mwezi kuanzia Julai Mosi mwaka huu. Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira,
Ridhiwani Wema, watakaolipwa kima kidogo zaidi cha Sh40,000 ni
wafanyakazi wa nyumbani ambao wameajiriwa na watu wa kawaida huku
wakiishi kwenye nyumba za waajiri wao.
Kwa
upande mwingine, katika viwango hivyo, kima kikubwa katika viwango
hivyo cha Sh400,000 kitalipwa kwa wafanyakazi wa sekta za mawasiliano
zikiwamo kampuni za simu, kampuni za kimataifa za nishati, madini na
taasisi za fedha.
Katika
viwango hivyo, mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na
watu wa kawaida lakini ambao hawaishi kwenye nyumba za waajiri wao
itakuwa Sh80,000.
“Viwango vya
chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na
mabalozi wa kigeni na wafanyabiashara maarufu wanatakiwa kulipwa
Sh150,000 kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.
Wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na maofisa wa Serikali watalipwa Sh130,000 kwa mwezi.
Kima cha chini cha mshahara katika huduma za kilimo ni Sh100,000 na huduma za afya Sh132,000.
Kwa upande
wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, posta na usafirishaji wa vifurushi
‘courier services’, kima cha chini kitaanzia Sh150,000.
Viwango vya
chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa hoteli za kitalii kuanzia Julai
Mosi, mwaka huu ni Sh250,000, wakati kwa hoteli za kati ni Sh150,000 na
migahawa, nyumba za wageni na baa ni Sh130,000.
Kampuni za
ulinzi za kimataifa zitapaswa kulipa kiwango cha chini cha mishahara cha
Sh150,000 kwa wafanyakazi wake sawa na kampuni ndogo za huduma za
nishati. Kampuni ndogo za ulinzi zitatakiwa kulipa Sh100,000.
Kima cha
chini kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kitakuwa Sh300,000,
sawa na wale wa utoaji na uingizaji wa mizigo. Wafanyakazi wanaofanya
katika sekta ya usafirishaji wa majini, uvuvi na nchikavu wakitakiwa
kulipwa Sh200,000.
Kima cha
chini kwa kampuni za makandarasi daraja la kwanza kitakuwa Sh325,000,
makandarasi daraja la pili hadi la nne Sh280,000 na makandarasi daraja
la tano hadi saba Sh250,000.
Wafanyakazi
katika kampuni za uuzaji wa magari watatakiwa kulipwa Sh300,000 na
madalali wa bima watalipwa Sh200,000. Kampuni za wachimbaji wadogo wa
madini zitalazimika kulipa mshahara usiopungua Sh200,000 kwa wafanyakazi
wake.
Mishahara ya
chini kwa wafanyakazi wa shule za awali, msingi na sekondari za binafsi
ni Sh140,000 huku wafanyakazi wa viwandani wakipaswa kulipwa Sh100,000.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Kazi imesema sekta ambazo hazijaorodheshwa, wafanyakazi wake watatakiwa kulipwa kuanzia Sh100,000.
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi