Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasai, Rajab Baraka alipozungumza na MTANZANIA kuhusu kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa aliyedai chama hicho hakimtambui John Tendwa kuwa ndiye msajili wa vyama vya siasa.
Katika madai yake Dk. Slaa alidai Tendwa anakipendelea CCM katika kutoa haki ya demokrasia na hatendi haki kama mlezi wa vyama vyote vya siasa nchini.
Dk. Slaa alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari na kusisitiza hata katika barua zao za mawasiliano kwenda kwa ofisi ya msajili chama hicho hakitumii jina la John Tendwa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Chadema kinaitambua ofisi ya Msajili wa Vyama tu lakini hakimtambui Tendwa kuwa ndiye msajili wa vyama vya siasa nchini.
“Hatumpelekei hata barua huyu hatunzi sheria siyo mtu wa kulea vyama ni mlezi wa chama kimoja, hayuko serious na hatushirikiani naye mpaka aondoke madarakani.
“Tukiandika barua hatuweki jina lake lakini tunaitambua ofisi yake, hata yeye mwenyewe analijua hilo na akijibu barua zetu haweki jina lake,” alidai Dk. Slaa.
Akijibu hoja hizo, Naibu Msajili alisema Chadema hawana ubavu wa kutomtambua Tendwa kwa sababu amewekwa kisheria na ofisi yake ipo kisheria.
Alisisitiza Tendwa ataendelea kuwa mlezi wa vyama vyote na siyo chama kimoja kama inavyodaiwa na kuvitaka vyama vyote kuheshimu sheria iliyomuweka madarakani msajili huyo.