Wakili wa
mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki
Zanzibar, amewasilisha ombi la mteja wake la kumkataa Jaji Mkusa Isaac
Sepetu, kuendelea na kesi hiyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye. Ombi
hilo liliwasilishwa na Wakili Abdalla Juma katika Mahakama Kuu Zanzibar
jana, akidai mteja wake hana imani na Jaji Sepetu na kutaka ajiondoe
kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.
Alisema kutokana na mwenendo wa kesi unavyokwenda, mteja wake haamini kama Jaji huyo atatenda haki.
Alisema Machi 28, mwaka huu aliwasilisha ombi dhidi ya Jeshi la Polisi
kumshikilia mteja wake kwa zaidi ya saa 24 bila ya kumfikisha mahakakani
na kutaka mteja wake aachiwe huru kama polisi wameshindwa kukamilisha
upelelezi kwa wakati.
Alisema alikosa imani mapema baada ya Jaji huyo kuendesha kesi yake
pamoja na ombi hilo, jambo ambalo alidai mteja wake alikuwa na wasiwasi
maombi hayo na kesi yake mojawapo halitafanikiwa kwa vile yote yapo kwa
Jaji mmoja.
Wakili huyo pia alidai kuwa mteja wake alidhani Jaji huyo atajitoa
kwenye jambo mojawapo ili haki itendeke, lakini hakufanya hivyo na
kulitupilia mbali ombi la mteja wake.
Mapema, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Abdallah Mgongo, aliomba
mahakama kuahirisha kesi hiyo kutokana na kuwa upelelezi unaendelea kwa
kupeleka vinasaba kwa Mkemia Mkuu Dar es Salam na kufuatilia mitandao ya
simu.
Jaji Sepetu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 16, mwaka huu kwa kutolea maamuzi baada ya kupokea ombi la kutakiwa kujiondoa.
SOURCE: NIPASHE



