Misri imeishutumu Iran hii leo kwa kuingilia masuala yake ya ndani baada
ya nchi hiyo kulikosoa jeshi kwa kumuondoa rais aliyechaguliwa kihalali
Mohammed Mursi.
Hivi sasa wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Misri imesema jambo la kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake kamwe halitakubalika.
Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu Hazem al-Beblawi, amesema hatazuia chama cha udugu wa kiiislamu kupata nyadhifa katika baraza lake la mawaziri bora tu wawe na ujuzi wa kushikilia nyadhifa hizo.
Hata hivyo taarifa hii inakuja wakati bado polisi nchini humo wakiendelea na oparesheni ya kuwakamata viongozi wa chama hicho. Akizungumza na chombo cha habari cha AFP Belawi amesema bado mpaka sasa yuko katika harakati ya kuunda serikali yake ya mpito.
Chama cha Udugu wa kiislamu chakataa mualiko
Chama cha Mohammed Mursi tayari kimekataa mualiko wa kujiunga na serikali hiyo mpya na kuitisha maandamano makubwa hapo kesho dhidi ya kile wanachokiita mapinduzi.
Huku hayo yakijiri polisi nchini Misri wanamtafuta kiongozi mkuu wa chama hicho Mohamed Badie, baada ya amri ya kukamatwa kwake kutolewa akishutumiwa kuchochea ghasia. Amri ya kukamatwa Badie imetolewa na mwendesha mashtaka mkuu wa Misri.
Kutokana na Ghasia zinazoendelea nchini Misri sasa Shirila la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa -FAO- limesema hali hiyo huenda ikapelekea uhaba wa chakula.
Marekani bado inaendelea kulifadhili jeshi la Misri
Wakati huo huo Marekani inaendelea na mpango wake wa kupeleka ndege za kivita aina ya F-16 nchini Misri, kando na kuwa na mjadala juu ya mapinduzi yaliofanywa dhidi ya Mohammed Mursi.
Ndege hizo za kivita ni katika mpango uliotiwa saini mwaka wa 2010 wa dola hizo milioni 1.3 zinazojumuisha pia ndege 20 za kivita.
Ndege nane zimeshapelekwa nchini Misri tangu mwezi wa Januari nyengine nne zinatarajiwa kufikishwa katika wiki kadhaa zijazo huku nyengine nane zikitarajiwa kupelekwa baadaye mwaka huu.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman