KUAMINI ni
tendo la hiyari. Ila ni wazi kuwa mwendo huu wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), juu ya siasa za Tanzania inajiweka kubaya.
Hili
ukilisema wapo watakaobisha. Watavaa vibwaya kuporomosha matusi kadri ya
uwezo wao. Hao ni wale wasiopenda kuambiwa ukweli. Wakiambiwa
wanachukia.
Hata hivyo,
ukweli siku zite unauma lakini unasaidia kumuweka mtu huru na lazima
tujuwe kuwa kuamini ni tendo la hiyari. Leo hii ambapo baadhi yao
wanaamini Chadema ndio kila kitu, ukiwaambia juu ya njia mbaya
wanayopita ni ngumu kukuelewa.
Ni wazi
Chadema kwa sasa ndio Chama Cha upinzani katika siasa za Tanzania Bara.
Nasema Tanzania Bara kwakuwa chama hicho kinachoongozwa na mwenyekiti
wake Freeman Mbowe, upande wa pili wa Muungano, yani Zanzibar hawana
chao.
Kule hakuna
anayeiamini Chadema. Ingawa Wazanzibar wengi hawaiamini Chadema kwa
sababu za kidini, ila hata mwenendo wao wenyewe, kuangalia sana Kanda ya
Kaskazini kunasababisha kuibua maswali kama wengine wanawajitaji.
Katika
Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chambani, uliofanyika mjini Zanzibar ambapo
Chama Cha Wananchi CUF kiliibuka mshindi kwa mgombea wao kinyang’anyiro
hicho cha Ubunge, Chadema waliambulia kura 11 tu.
Katika hali
ya kushangaza zaidi, chama kipya ambacho hakina hata mwaka mmoja, yani
ADC, chenyewe kilipata kura 112, ikiwa ni ishara kuwa katika visiwa
hivyo Chadema hawana chao.
Katika
mchanganuo wa kura hizo katika jimbo la Chambani, Chama Cha Mapinduzi
CCM wenyewe walipata kura 202, wakati CUF wao 2708 na kunyakua jimbo
hilo.
Sio Zanzibar
tu, ila katika sehemu nyingi za Tanzania Bara, pia Chadema haijulikani
na haina heshima. Hii ni kwasababu sera na mpangilio wao haueleweki.
Wanachoweza
wao ni kubuni matamko yasiyokuwa na mashiko kwa Watanzania wote, ukiacha
wale waliokuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Mbeya Mjini na
baadhi ya maeneo wanapokubalika.
Wajuzi wa
mambo ya siasa wanajua kuwa ili chama kifanikiwe kushika dola, walau
kinastahili kuungwa mkono na watu wengi. Chama kinachojulikana Tanga tu
na kuheshimiwa, kamwe haiwezi kuwa njia ya kuwapatia Dola.
Wakati haya
yanaendelea kutokea, Chadema wanajikuta wakiubua maswali yasiyokuwa na
majibu. Viongozi wao wa chama na serikali mtazamo wao unasua utata.
Kwa mfano,
mara baada ya kutokea mlipuko wa bomu uliosababisha vifo vya watu watatu
katika Mkutano wa Kampeni za udiwani uliofanyika jijini Arusha, Mbowe
kama Mwenyekiti alitangaza kuwazuia wabunge wake kuingia bungeni.
Lengo la
Mbowe lilikuwa ni kuwataka wabunge hao washiriki mazishi ya wafuasi wao
waliokufa kwa mlipuko wa bomu. Mazishi ambayao Chadema walijua kuwa
walitakiwa wasiandamane au kuaga kwa makundi kwasababu za kiusalama.
Kwakuwa
wanajua mtaji wao ni propaganda chafu dhidi ya wananchi na serikali yao
iliyopo madarakani, Chadema waligoma. Wakaamua kufanya wanavyotaka wao.
Hii
ilisababisha kuzua mgogoro baina yao ni Jeshi la Polisi. Jeshi ambalo
kila siku ya Mungu Chadema wamekuwa wakitoa lawama, wakiwadhihaki na
kuwatusi pia.
Mara kadhaa
tunasikia Jeshi la Polisi likitwa PoliCCM. Maneno mengi dhidi ya walinzi
hawa wa raia na mali zao yanatoka katika vinywa vya watu
wanaojipambanua kuwa wanahitaji kuwaongoza Watanzania.
Huu sio
mpango mzuri. Ili Watanzania waendelee kuwa na heshima na vyama vya
siasa, ni wazi Chadema kama Chama Kikuu cha upinzani Tanzania Bara,
lazima kijisahihishe.
Kabla ya kuzungumza jambo, lazima wakae na kufanyika tathimini. Huu ndio ukweli wa mambo.
Kinyume cha
hapo Chadema wataendelea kuwagawa wananchi, huku wale wanaowaunga mkono
pia wakitafakari uwapo wao. Kwa mfano, Chadema kwa kupitia kikao cha
Kamati Kuu kimetangaza kuwafundisha vijana wao namna ya kujilinda.
Hii ndio
kusema kuwa Chadema wameona jeshi halali la Tanzania limeshindwa
kuwalinda. Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekataza
vikundi vya namna hiyo, kikiwamo hiki cha Red Brigade kilichotangazwa na
Chadema.
Wataalamu wa
mambo wanahisi kuunda vikundi vya aina hii ni kuzalisha chuki na
machafuko. Kwa Chadema ambao wamekuwa wakilalamikia jeshi la Polisi
kesho vijana wao hawatafanya fujo?
Leo hii
wakiwa wakomavu na mafunzo hayo hawatawarushia mabomu askari wetu? Haya
ni maswali yanayotakiwa yajibiwe na kila Mtanzania juu ya siasa za
Tanzania, hususan Chadema.
Chama
ambacho dhamira yao inaweza kuyeyuka kama watashindwa kujiweka sawa.
Mwendo wao si mzuri. Kauli zao nyingi inaonyesha inatoka bila kufanyiwa
uchunguzi.
Kwa mfano,
Chadema wao waliweza kususia vikao halali vya Bunge kwa kisingizio cha
mazishi ya wafuasi wao. Mbaya zaidi, waligomea katika Bunge la Bajeti.
Bunge ambalo
tangu lilipomalizika, tayari kumekuwa na matokeo magumu ya kupandishwa
kwa kodi katika baadhi ya huduma, zikiwapo za simu za mikononi.
Leo hii
Mtanzania ambaye hata kula yake haijulikani, bado atapaswa kulipia kiasi
cha Shilingi 1,000 kwa namba yake (simcard). Hii ni kodi tofauti na
gharama nyingine za muda wa maongezi ambazo zimepanda mara dufu.
Ingawa
wabunge wa CCM wapo wengi bungeni, wakifikia 245 tofauti na wale wa
upinzani hususan Chadema, ila kuwapo kwao kungesaidia kuibua hoja katika
mrejesho wa hutuba ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa na wataalamu
wake.
Kitendo cha
uwapo wao, huenda kingezindua zile hoja zenye mashiko na Watanzania
wote. Lakini waligoma kuingia kwasababu ya Arusha, wabunge wao wote
wakiwapo huko, bila kujua kuwa Tanzania ina mikoa mingine inayohitaji
uwapo wa wapinzani.
Bado kuna
mikoa kama vile Mwanza, Geita, Morogoro, Tanga, Ruvuma, Pwani na
mingineyo, hivyo si vizuri pia kwa chama hiki kuangalia zaidi Kanda ya
Kaskazini.
Aidha
tunahitaji hoja zaidi badala ya kupayuka maana huko kunaoanyesha
mapungufu ya hadharani kabisa. Kwa mfano, katika makala yangu ya Mbunge
wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi Sugu, nilipinga
kumuita Mpumbavu Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wapo
waliokosoa na waliosifia pia. Katika makala ile, nilijaribu kusisitiza
wanasiasa wetu, viongozi wetu kupenda kuweka hoja badala ya mihemko
isiyokuwa na tija.
Huu ndio
ukweli. Hivyo hata hili suala la Red Brigade la Chadema linaweza kuwa
baya zaidi kama litatumiwa tofauti. Chadema lazima wajuwe wana kila
sababu ya kuilinda amani ya nchi yetu.
Sioo Chadema
tu, ila vyama vyote vya siasa vinastahili kupigania amani maana ndio
msingi wa maendeleo. Leo hii kama kila mtu ataweza kuunda vikosi
anavyojua mwenyewe tutasababisha mwingiliano na machafuko yasiyokuwa na
mpango.
Shughuli za
ulinzi wa Taifa letu tushiriki kwa pamoja, ila zaidi jeshi la Polisi
lina imudu zaidi kazi hiyo. Muhimu ni kuwapa moyo na kuwapa ushirikiano
pia.
Hakuna haja
ya mwanasiasa kutoa maneno ya kejeli kwasababu Dola ipo chini ya CCM.
Tusipokuwa makini na kufanya siasa za kuvumiliana, hata kesho Chadema
wakiingia Ikulu au ama CUF basi machafuko, lawama za mtindo huo
zitashika kasi.
Angalia
nchini Misri. Mwaka jana wananchi waliweza kuandamana kushinikiza rais
wao Hosni Mubarak ajiuzulu. Walifanikiwa. Mubarak alitoka na uchaguzi
huru wa kwanza kufanyika.
Lakini
wakati watu wakiwa hawajui kinachotokea, wananchi hao hao tena wanaingia
barabarani kumtaka rais wao Mohamed Morsi ang’oke kwa madai kuwa
ameshindwa kuliongoza Taifa hilo.
Pia
wakafanikiwa, hasa baada ya jeshi kumsaliti na kumuengua. Hii ni ishara
kuwa hata Tanzania hayo yanaweza kutokea. Kama wananchi watafundishwa
kufanya vurugu, maandamano, matusi na kejeli dhidi ya serikali au jeshi,
basi hata kama Chadema wakiingia Ikulu, mtindo huo utaendelea kushika
kasi.
Ni vyema
tukajifunza katika hili. Tanzania tunakabiriwa na changamoto nyingi has
azan ugumu wa maisha. Ni vyema basi tukatumia muda mwingi kuwaza namna
ya kujiletea maendeleo na sio kupanga namna ya kulisumbua Taifa kwa
namna yoyote ile.
Ni wakati wa
wanasiasa wetu kutumia busara na siasa za uvumilivu ili iwe nafasi ya
kujiletea maendeleo. Vyama vya upinzani kama kweli vinahitaji kuwakomboa
Watanzania kama wenyewe wanavyosema, wasimamie kwanza katika suala zima
la amani yetu inayoelekea ukingoni, ukizingatia kuwa kaatika siku za
hivi karibuni, kumekuwa kukitokea matukio ya kuogopwa, hasa ya utekwaji
na uteswaji.
+255 712 053949