Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo (CCM)
Arusha.Meya
wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo (CCM), ametamba kuwa wanaofikiria
kumng’oa kwenye kiti chake wanaota ndoto za alinacha kwa sababu lazima
wazingatie kanuni za uendeshaji wa Mabaraza ya Madiwani.
Baada
ya kushinda kata nne za Arusha kwenye uchaguzi mdogo juzi, Chadema
ilitamba kuwa kazi inayofuata ni kumng’oa Meya kutokana na kuwa na viti
vingi kwenye Baraza la Madiwani.
Lyimo aliliambia Mwananchi kuwa pamoja na Chadema kuwa wajumbe wengi kwenye Baraza la Madiwani, bado hawana ubavu wa kumtoa.
Alisema
ili kumtoa katika nafasi hiyo wanahitaji kuwa na theluthi mbili ya
wajumbe . Lyimo alisema maana yake ni kuwa ili ang’oke lazima Chadema
waungane na madiwani wa CCM ndiyo watafanikisha azma hiyo.
“Sharti
la kumng’oa madarakani Meya au Mwenyekiti wa halmashauri ni kupata
theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. Najiuliza wenzetu watafikiaje
kiwango hicho hadi waanze kutamba kuning’oa madarakani,” alisema Lyimo.
Jiji
la Arusha lina jumla ya wajumbe 32 kwenye Baraza la Madiwani ambapo
ukimtoa Meya, wajumbe wanaostahili kupiga kura wanasalia 31 hivyo
kufanya wenye nia ya kumng’oa kiongozi huyo kuhitaji zaidi ya kura 24
kutimiza lengo lao.
Baada
ya kunyakua viti vyote vinne kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili
iliyopita, Chadema imefikisha wajumbe 15 kwenye baraza ikiwa ni
madiwani 12 pamoja na wabunge watatu, wawili wa viti maalumu na mmoja wa
jimbo.
Kwa
upande wake, CCM kimebakia na wajumbe 14, ikiwa ni madiwani 11 na
wabunge watatu wa viti maalumu, huku TLP ikiwa na wajumbe wawili ambao
ni diwani mmoja wa kata na mwingine wa viti maalumu.
Kata
ya Sombetini ambayo awali ilishikiliwa na CCM iko wazi baada ya
aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo kujivua uanachama na kuhamia
Chadema.
Kutokana
na mchanganuo huo, Meya Lyimo alisema hana hofu ya kupoteza nafasi yake
kwa sababu ili Chadema wafikie lengo hilo, ni lazima waungwe mkono na
wajumbe kutoka CCM, jambo alilosema ni ndoto ya kutokea.
“Nakusisitizia
ndugu yangu, mimi nipo na nitaendelea kuwepo hadi mwisho wa kipindi
changu kwa uwezo na msaada wa Mwenyezi Mungu. Hakuna wa kuning’oa. Hata
leo nilikuwa ofisini kutekeleza majukumu yangu ya kuongoza kikao cha
kamati ya fedha,” alitamba Lyimo.
Meya
huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema kuacha kupoteza muda na nguvu
nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa madarakani, badala yake watumie muda
na nguvu hizo kuwatumikia wananchi waliowaamini na kuwapigia kura kwenye
uchaguzi.
Alisema
kwa nafasi yake ya Umeya, atashirikiana na madiwani wote kutatua kero
na kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi bila kujali tofauti zao
kiitikadi kwa sababu suala la maendeleo halina itikadi, dini wala
ukabila.
Akizungumzia
kiti cha Umeya, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa
alisema ajenda kuu ya Chadema ni kupata wingi wa kura na hivyo kuwa na
uamuzi katika Baraza la Madiwani limefanikiwa baada ya kurejesha kata
zake zote nne.
“Hata
kama wenzetu wataendelea kubaki na Meya wao wa ‘kuchonga’, bado uamuzi
wote unayohitaji kura kwenye baraza la halmashauri yatasimamiwa na
kuongozwa na Chadema. Hilo ni faraja na ishara njema ya kunyakua uongozi
wa halmashauri na nchi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Golugwa.
Tangu
achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka 2010, Meya Lyimo amekuwa akipingwa
na Chadema kwa madai kuwa hakuchaguliwa kihalali ambapo Januari 5,
2011, chama hicho kikuu cha upinzani kiliitisha maandamano makubwa
kumpinga ambayo yaliishia kwa watu kujeruhiwa na kuuawa baada ya polisi
kuyasambaratisha.
MWANANCHI