OFISA
Uvuvi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT ), Seleman Chasama (50),
amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na meno ya
tembo, yenye thamani ya Sh bilioni 4.2.Chasama alifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, na kusomewa
mashitaka na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi,
Nyigulila Mwasebo.Alisomewa mashitaka hayo chini ya Sheria ya Uhifadhi
wa Wanyamapori pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.Kwa mujibu wa sheria
hiyo, mshitakiwa akipatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo
kisichozidi miaka 15 au adhabu nyingine ikiwemo kulipa faini.Akisoma
mashitaka hayo, Wakili Kimaro alidai kuwa Julai 4 mwaka huu katika eneo
la Mbezi Makabwe Kinondoni Dar es Salaam, Chasama alikamatwa akiwa na
nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo 347, yenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 2.6 sawa na Sh bilioni 4.2.
Mshitakiwa
hakutakiwa kujibu mashitaka, kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa
kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka.
Upande wa
mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na
mshitakiwa alirudishwa rumande hadi Julai 24 mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
Credit: audifacejackson.blogspot.com