MBUNGE
wa Jimbo la Kinondoni, jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya CCM, Idi
Azzan, amejilisalimisha' polisi na kutaka jeshi hilo, kufanyia uchunguzi
tuhuma za kuhusishwa na biashara za dawa za kulevya na iwapo itabainika
anahusika, hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Mbunge
huyo alifikia hatua hiyo jijini Dar es Salaam jana baada ya barua
zilizoandikwa na watu wanaodai ni wafungwa wa Tanzania wanaotukia adhabu
zao mjini Hong Khong, nchini China, kusambaa kwenye mitandao ya kijamii
zikimhusisha yeye (Azzan) kuwa amekuwa akifanya biashara hiyo
akiwatumia vijana hao. Wafungwa hao wanadaiwa kuwa wanatumikia adhabu
zao baada ya kupatikana na makosa ya dawa za kulevya.
Mbunge huyo alisema alienda kutoa taarifa hizo mwenyewe Kituo Kikuu cha Polisi Kati, jijini Dar es Salaa.
"Nimeamua kwenda kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa taarifa ili
ufanyike uchunguzi wa jambo hilo na ukweli ubainika na hatua za kisheria
zifuate juu yangu," alisema Azza, wakati akizungumza na gazeti hili kwa
njia ya simu jana.
Azzan alibainisha kuwa ameamua kwenda kutoa taarifa polisi ili waanze
uchunguzi wao. Alisema barua hizo ambazo hazina anuani ya eneo
zilipotoka wala majina ya waandishi wake zina lengo baya dhidi yake na
kutaka kuposha umma.
"Mimi sipo juu ya sheria itakapobainika najihusisha na tatizo hilo,
nichukuliwe hatua mara moja, na nitajiuzulu ubunge wangu," alisisitiza
Azzan na kuongeza;
"Wapiga kura wangu wa Kinondoni pamoja na wananchi kwa ujumla inatakiwa
waelewe kuwa barua hizo zina nia mbaya zenye lengo la kunichafua na kama
kweli wana ushahidi wangetaja majina yao."
Mwishoni wiki hii katika mitandao mbalimbali ya kijamii ziliwekwa barua
zinazodaiwa kuandikwa na wafungwa waliokamatwa na dawa za kulevya nchini
China zikimhusisha mbunge huyo na biashara hiyo.
Barua hizo pia zinawataja baadhi ya viongozi wa serikalini kuwa
wanajihusisha na mtandao wadawa za kulevya, lakini hazikuainisha majina
yao.
CHANZO: MATUKIO