Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imesema matukio ya ubabe, unyanyasaji, uonevu na matesi ya siri yanayoendelea mkoani Mtwara ni ishara ya serikali kushindwa kutafuta suluhisho la sakata hilo kwa njia ya amani.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati
Kuu ya chama kilichofanyika Julai 06 na 07, mwaka huu.
Kikao hicho kilijadili hali ya kisiasa nchini na rasimu ya Katiba.
Alisema
kwa haraka hali ya Mtwara inaonekana ni shwari lakini kuna vitendo vya
uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na Polisi na wanajeshi kwa
kutumia silaha kuwakamata wananchi na viongozi wa kisiasa na kuwapeleka
kwenye kambi za jeshi kwa lengo la kuwatesa.
“Rais
Jakaya Kikwete alitangazie Taifa ‘hali ya hatari’ kwa mkoa wa Mtwara,
kama anaona ni hatari kiasi cha kutumia Jeshi la Wananchi (JWTZ),
kuzunguka mitaani na silaha za kijeshi, ili Taifa liweze kujua,”
alisema.
Aidha,
alisema CC imesema kama Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza majikumu
yake kwa mujibu wa sheria atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.
Mwenyekiti
huyo alisema pia serikali iunde Tume Huru ya kuchunguza matukio ya
mauaji, ubakaji, utesaji na ukiukwaji wa Haki za Binadamu yanayofanywa
na vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa mujibu wa
sheria.
Sakata
la gesi Mtwara, lilianza Novemba 16, mwaka huu, baada ya serikali
kutangaza mpango wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo hadi Dar
es Salaam, na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo,
kutangaza Bungeni msimamo wa serikali wa kuendelea na ujenzi wa bomba
hilo.
Watu
wanne wamefariki na wengine 15 wamejeruhiwa kwa risasi na 15 majeraha
yaliyotokana na kurupushani za kujiokoa dhidi ya vurugu za mwezi Mei,
mwaka huu.
JWTZ WAMJIBU MBOWE
NIPASHE
ilipomtafuta msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) Kanali
Kapambala Mgawe, kuzungumzia tuhuma hizo, alisema hazina ukweli wowote
na hataki kuendelea kuzungumzia suala la Mtwara kwa sababu limekaa
katika mlengo wa kisiasa.
“Jeshi
la Wananchi lina nia njema ya kuhakikisha amani inalindwa kwa wananchi
wote wakiwamo wa Mtwara na si vinginevyo, hakuna ukweli wowote kwamba
Wanajeshi wanawatesa wananchi wa Mtwara,” alisema na kuongeza:
“Nimefika
mahali nimechoka kuzungumzia suala la Mtwara, suala hili naliona liko
katika mlengo wa kisiasa zaidi wakati mimi siyo mwanasiasa na sitaki
kugombana na wanasiasa…sipendi tabia ya watu kutufanya kama vile hatujui
tunachokifanya, tunataka amani ilindwe na shughuli za kuendeleza uchumi
wetu zifanyike salama,” alisema.
NIPASHE
pia ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Advera Senso,
kuzungumzia juu ya mkakati wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kuendesha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake
kulinda Viongozi wao, alisema ni marufuku kufanya hivyo na wakithubutu
watachukuliwa hatua za kisheria.
Credit: mwanahabariuswazi.blogspot.com